Wafungwa 3 wanaohusishwa na ugaidi waliotoroka jela ya Kamiti Kenya walivyokamatwa

Mmoja ya wafungwa waliotoroka Jela ya kamiti nchini Kenya Ali Abikar

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mmoja ya wafungwa waliotoroka Jela ya kamiti nchini Kenya Ali Abikar
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wafungwa 3 wanaohusishwa na ugaidi ambao walitoroka jela ya kamiti nchini Kenya siku ya Jumatatu wamekamatwa.

Watatu hao Musharaf Abdalla maarufu Alex Shikanda , Joseph Ouma na Mohammed Ali Abikar walikamatwa katika eneo la Kitui.

Kwa sasa washukiwa hao wanasafirishwa kurudi jijini Nairobi.

Walitoroka kutoka jela inayolindwa zaidi baada kutoboa ukuta wa jela hiyo.

Baadaye walitumia nguo aina ya blanketi na waya kutengeneza kamba ambazo walitumia kupanda kuta mbili ndefu za jela hiyo.

Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya maafisa wa jela ya Kamiti kukamatwa kwa madai ya kuwasaidia wahalifu hao kutoroka

Baada ya kukamatwa walisafirishwa kwa ndege hadi katika jela ya Kamiti. .

kamiti

Chanzo cha picha, Wizara ya masuala ya ndani

Walikuwa wanaelekea msitu wa Boni

Maafisa wa polisi wamesema kwamba watatu hao walikuwa wanaelekea katika msitu wa Boni ambao unapakana na taifa la Somalia, wakati walipokamatwa na maafisa wa usalama katika kaunti ya kitui saa chache baada ya wakazi kuripoti kuwaona katika soko la Malalani .

Baada ya kukamatwa , maafisa wa usalama waliwazuilia kwa muda katika kituo cha polisi cha Mwingi wakisubiri usafiri wa ndege kuelekea Nairobi.

Baadaye walichukuliwa na kupelekwa katika kituo cha polisi wa kukabiliana na ugaidi katika eneo la Kanyonyo kaunti ya kitui kwa magari yaliokuwa na usalama wa hali ya juu.

Baadaye walisafirishwa kwa ndege hadi katika jela ya Kamiti kaunti ya Kiambu.

Katika kaunti ya Kiambu, Waziri wa masuala ya ndani Fred Matiangi na mkuu mpya wa Magereza Brigedia mstaafu John Warioba na maafisa wengine wa usalama walikuwa ndani ya jela ya kamiti wakiwasubiri.

Siku ya Jumatano, Rais Kenyatta alimwaagiza waziri wa masuala ya ndani Fred Matiangi kuhakikisha wanatumia kila mbinu kuwakamata wahalifi hao hatari.

Alivitaka vitengo vyote vya upelelezi kuwawajibisha maafisa wote waliodaiwa kuhusika na kutoroka kwao.

Wafungwa watoro wakitolewa katika ndege

Chanzo cha picha, Wizara ya masula ya ndani

Maelezo ya picha, Wafungwa watoro wakitolewa katika ndege

Kulingana na gazeti la Daily Nation, awali , vitengo vya usalama katika kaunti ya Kitui vilikuwa vimewekwa katika hali ya tahadhari baada ya wakaazi wa eneo hilo kuwaona wafungwa hao watoro.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei mapema Alhamisi alithibitisha kwamba vitengo vyote vya usalama katika eneo hilo, wakiwemo machifu na manaibu wao walikuwa wamewekwa katika hali ya tahadhari.

''Habari hiyo pia imesambazwa kwa wenzetu katika kaunti jirani ya Tanariver na Garissa'', bi Kithei aliambia Daily Nation.

''Iwapo ni kweli ni wao, bila shaka tutawakamata, ni muda tu kabla ya hilo kufanyika''.

Wakazi waliowaona wanasemaje?

Wakaazi wa eneo hilo waliripoti kuwaona watatu hao , ambao wanawashuku kuwa wahalifu wanaosakwa baada ya kutoroka jela siku ya Jumapili, katika kituo cha maduka cha Malalani katika kaunti hiyo kubwa.

Walisema kwamba watatu hao , walioonekana kuchoka na wenye kiu, walinunua maziwa mengi , na maji , mkate na biskuti kutoka kwa maduka ya eneo hilo na kuplipa pesa.

Kwa mujibu wa gazeti hilo wakaazi walianza kuwashuku baada ya kutaka kuoneshwa njia ya kuelekea msitu wa Boni huko kaunti ya Lamu.

Ndege ya polisi iliowabeba wafungwa hao ikishuka jela ya Kamiti

Chanzo cha picha, Wizara ya masuala ya ndani

Maelezo ya picha, Ndege ya polisi iliowabeba wafungwa hao ikishuka jela ya Kamiti

''Mmoja ya watoro hao alikuwa na kidonda katika mguu wake na alikuwa akichechemea pengine kwasababu ya kutembea mwendo mrefu. Walionekana kukanganyika na waliopotea, wasio na uelewa wowote wa eneo hilo''.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

''Walikuwa wanauliza jinsi wangeweza kuelekea Garissa au Tanariver kutoka eneo hilo'', alisema mfanyabiashara katika soko hilo ambaye alizungumza na Nation kwa makubaliano kwamba hatotajwa kutokana na sababu za kiusalama.

Mfanyabiashara huyo aliwaelezea watatu hao kama mtu mmoja mwembamba mwenye asili ya kisomali na wanaume wawili Waafrika , maelezo ambayo ni sawa na watoro hao.

''Hawakuwa wamebeba mzigo lakini mmoja wao alikuwa amebeba begi dogo na kile kilichoonekana kama nguo''.

Soko la Malalani lipo kilomita 100 mashariki mwa mji wa Kitui na karibu na mpaka na kaunti ya Tanariver.

Linapakana na Mbuga ya wanyama ya Kusini mwa Kitui ambayo imekuwa maficho kwa washukiwa wa ugaidi.

Agizo la Rais

Maafisa wa kukabiliana na ugaidi nchini Kenya walikuwa wameanzisha msako mkali dhidi ya watoro hao kufuatia agizo la rais kwamba watatu hao ni sharti wakamatwe kwa hali na mali.

Zawadi ya $535,000:£396,000 ilikuwa imetolewa kwa yeyote yule ambaye angetoa habari kuhusu watatu hao