Mashambulio ya mabomu ya 1998: Kenya na Tanzania zajipata katika kampeni ya vita dhidi ya ugaidi

ru

Chanzo cha picha, Reuters

Miaka 23 iliyopita mwezi kama huu tarehe saba ,mashambulizi mawili ya kigaidi yaliotekelezwa kwa wakati mmoja yaliikumba Miji ya Nairobi, Kenya na Dar Es Salaam Tanzania.

Mashambulizi hayo ya Agosti mwaka wa 1998, yalibadilisha kabisa hali ya usalama wa kanda hii na kuzitosa nchi hizo katika kampeni iliyojulikana kama 'vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi'.

Wiki hii tunakuletea Makala maalum kuhusu mashambulizi hayo ,wahusika wakuu na matokeo ya kampeni ya vita dhidi ya ugaidi na athari zake kwa nchi za Kenya,Tanzania ,Uganda na kanda nzima. Leo tunaangazia athari za shambulizi hilo na jinsi mataifa ya kanda hii yalivyochukua hatua zilizodhaniwa zitazuia mashambuklizi mengine ya kigaidi .

bb

Yalikuwa mashambulizi ya kushtua ambayo yaliacha mataifa ya Kenya na Tanzania katika hali ya mshtuko .

Kilichofuatia pindi baada ya ukubwa na maafa ya mashambulio katika nchi mbili kujulikana ni hali ya wasi wasi .Kwa Kenya ambayo iliathiriwa sana kwa vifo vingi na idadi ya juu ya watu waliojeruhiwa , serikali haikulewa jinsi uhasama kati ya makundi ya kigaidi na Marekani unavyoweza kufika hadi katika ardhi yake-mji wake mkuu .

Rais Daniel Moi alikuwa amechaguliwa tu mwaka mmoja uliotangulia na hili lilikuwa jaribio kubwa sana kwa muhula wake wa mwisho madarakani .

Serikali ya Kenya haikuwa na budi ila kuitegemea Marekani kwa msaada wa kung'amua kilichofanyika ,wahusika na njia za kuzuia mashambulizi yajayo.

Kundi la Al Qaeda halikuchukua muda kudai kuhusika na mashambulizi hayo na miezi kadhaa baadaye ,iligunduliwa kwamba mtandao huo ulikuwa na wanachama wake katika nchi mbali mbali za Afrika na hasa zinazopakana na Kenya .

Sudan na Somalia baadaye zilitambulika kama baadhi ya ngome za wapiganaji na viongozi waliokuwa wakiongoza harakati dhidi ya Marekani na nchi za magharibi .

Vita dhidi ya ugaidi

Ushirikiano wa kiusalama ulifuatia ambapo nchi za kanda hii pamoja na zile za magharibi zilianza kutengeneza vikosi maaluma vya kijeshi na kijasusi kuweza kubadilishana habari kuhusu shughuli za magaidi na washukiwa waliofaa kusakwa .

Kenya ilikuwa tayari imeanza safari yake ya kujiingiza katika vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi lakini athari ya hatua iyo ilibainika miaka michache iliyofuata.

AFP

Chanzo cha picha, AFP

Wakati Marekani ikiendelea kuwasaka na kuwatambua waliohusika na mashambulio hayo ,nchi nyingi za Afrika zilianza kupewa raslimali nyingi na mataifa ya magharibi katika uliokuwa mpango wa pamoja wa 'vita dhidi ya ugaidi' ili kumaliza tisho hilo .

Baadhi ya serikali hazikuelewa uamuzi huo utasababisha matokeo yapi na ripoti zikaanza kuibuka za vijana kujiunga na makundi yenye itikadi kali.

Wakati huo sio serikali nyingi zilizofahamu kilichokuwa kikitokea lakini mengine yaliyokuwa yakifanyika nje ya Afrika baadaye yalichangia kuhusika moja kwa moja kwa nchi kama Kenya katikati ya kampeni ya vita dhidi ya ugaidi .

Shambulio la Septemba 11

Miaka mitatu baaa ya mashambulio ya 1998 Afrika Mashariki - kundi la Al Qaeda lilitekeleza shambulizi kubwa zaidi katika ardhi ya Marekani.

Shambulio hilo la Septemba 11 mwaka wa 2001 liliingiza Kenya kikamilifu katika kampeni za vita dhidi ya ugaidi .

Ilikuwa wazi kwamba vitisho vya ugaidi havikukaribia kukomea hapo na shambulio dhidi ya nchi kama Marekani liliyatia hofu mataifa ya Afrika ambayo hayakuwa na uwezo wa kujibu mashambulio kama hayo .

get

Chanzo cha picha, Getty Images

Miaka mitano baadaye wakati msukosuko nchini Somalia ulipochukua mkondo mwingine ,mojawapo ya makundi yaliyoibuka na kutishia usalama wa kanda hii ni Al shabaab .Kufikia wakati huo oparesheni za serikali za kanda hii na ushirikiano wa nchi hizo na Marekani zilikuwa zimesababisha uhasama mkubwa na baadhi ya watu wenye itikadi kali za kidini ambao walikuwa tayari kuendeleza kampeini za 'kijihadi' katika eneo hili .

Al shabaab ilionekana kama chaguo na pindi zikatokea ripoti za wapiganaji kutoka nyingine za Afrika waliojiunga na kundi hilo mwaka wa 2012 wakati kundi hilo lilipojiunga na Al Qaeda .

Mamia ya vijana kutoka nchi za Afrika mashariki waliripotiwa kujiunga na kundi hilo wakati huo. Idadi kamili ya vijana kutoka nchi za Afrika mashariki waliokimbilia Somalia haijulikani lakini imebainika kwamba kundi hilo lilinufaika na raia kutoka kila nchi zinazopakana na Somalia na Kenya na Tanzania zilikuwa miongoni mwa nchi ambazo baadhi ya vijana wake walijipata Somalia .

Mbinu zilizozua mgawanyiko wa kidini

Wakati tishio la ugaidi lilipotoa wazi sura yake, nchi nyingi zilijibu kwa matumizi ya nguvu .Wakati huo hakuna serikali iliyotaka kujua mzizi wa chanzo cha vijana kutaka kujiunga na magaidi na mbinu ambazo zilikiuka sheria kama kukamatwa kwa watu na kuhojiwa kwa misingi ya kikabila au dini zao kulionekana kuzua hisia kali hasa kwa jamii ya Waislamu nchini Kenya .

kdf

Chanzo cha picha, EPA

Sheria zilizoundwa baadaye kupambana na ugaidi pia zilionekana kulenga baadhi ya jamii za Kenya hali ambayo ilivuruga sana uhusiano wa kidini miongoni mwa Wakenya .

Ripoti za baadaye za maimamu waliodhaniwa kuwa na misimamo mikali ya kidini kuuawa na kupotea kwa vijana waliodaiwa kuwa na itikadi kali za kidini pia ni jambo ambalo liliathiri uhusiano wa kidini miongoni mwa jamii za Kenya .

Marekani ikiendelea kuwasaka na kuwashtaki washukiwa wa kigaidi waliokuwa wakilenga maslahi yake kimataifa, Kenya ilijipata na 'vita vyake vidogo' dhidi ya ugaidi katika kanda hii katika kilichozihusisha nchi kama vile Ethiopia na Uganda na kujipata katika mkondo wa kuyapeleka majeshi yake nchini Somalia mwaka wa 2011. Hiyo ilikuwa tu hatua nyingine ya vita dhidi ya ugaidi .