Fahamu operesheni maalum za kuwakamata au kuwaua Osama Bin Laden ,Saddam Hussein , Muamar Gaddafi

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
Unapokuwa kiongozi wa nchi au shirika ,huwa unapewa ulinzi na hadhi ambayo inakupa usalama katika maisha yako ya kila siku .Hata hivyo wakati mwingine ,kuna viongozi kadhaa ambao walijikuta wakisakwa kama wanavyosakwa wanyama porini.
Kila juhudi ziliwekwa na raslimali nyingi kutengwa kwa lengo la kukamatwa ama kuuawa kwao .
Hakuna anayeingia uongozini akitarajia kwamba siku moja atakuwa adui mkubwa wa kusakwa kwa udi na uvumba na hata zawadi ya mamilioni ya dola kutolewa kwa yeyote mwenye habari za kukamatwa au kuuawa kwao .
Marekani imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za miaka ya hivi karibuni kuwasaka kwa lengo la kuwakamata au kuwauawa wahalifu sugu ,washukiwa wakuu wa ugaidi na hata viongozi wengine wan chi ambao walitolewa madarakani .
Aliyekuwa rais wa Iraq Saddam Hussein,Rais wa zamani wa Libya Muamar Gadafi na aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al qaeda Osama Bin Laden ni miongoni mwa watu tajika waliojipata katika kuta za mashirika ya kujasusi ya Marekani kama wanaosakwa sana.Hizi ni oparesheni zilizoendeshwa na vikosi mbali mbali kuwakamata ama kuwaua
Operesheni dhidi ya Osama bin Laden
Marekani na idara zake za usalama na ujasusi ilianzisha mpango wa kumkamata au kumuua Osama Bin Laden aliyekuwa akiliongoza kundi la Al qaeda linaloshtumiwa kwa shambulizi la septemba tarehe 11 mwaka wa 2001 .
Operesheni hiyo ilipewa jina Operation Neptune Spear . Ilipangwa kwa miezi kadhaa lakini ilichukua dakika chache kuitekeleza mei 2011
Katika shambulizi lililofanywa maili 120 (192km) ndani ya Pakistan, timu ya vikosi maalum vya Marekani ilisafiri kutoka Afghanistan kwenda maficho ya Bin Laden usiku wa manane. Walitua kwa kasi kwenye kiwanja kimoja kwa helikopta, wakapitia majengo ndani ya boma hilo refu na kuwapiga risasi watu takribani watano akiwemo Bin Laden.
Karibu dakika 40 baadaye waliondoka, wakichukua mwili wa Bin Laden na mkusanyiko wa vifaa vya data vya kompyuta na habari zingine zilizokuwa na ujasusi kuhusu shughuli za al-Qaeda na Bin Laden.

Chanzo cha picha, Reuters
Waliacha nyuma watu wengine waliouawa , kati yao kulikuwa na mwanamke na mmoja wa watoto wa Bin Laden. Waliacha pia kikundi cha wanawake watatu na watoto 13 - wasichana wawili na wavulana 11 - wakiwa wamefungwa kwa kamba za plastiki.
Walakini, Mei 2 iliwasilisha usiku uliokuwa bila mwanga wa mwezi ambao ulifaa kwa shambulio hilo. Rais Obama alitoa rasmiidhini mapema asubuhi ya Ijumaa 29 Aprili.
Lakini licha ya upangaji wa kina, operesheni ilianza kwenda vibaa mara tu wanajeshi walipoanza kushuka kutoka juu
Ndege tano zilisafirisha timu mbili za wanajeshi kutoka kituo cha Marekani huko Jalalabad, Afghanistan, kwenda Pakistan. Helikopta tatu kubwa za Chinook zilizobeba timu ya wanajeshi 24 wa ziada ziliwekwa karibu na Mto Indus, mwendo wa dakika 10 kutoka kwa kiwanja.
Ndege nyingine mbili, helikopta za Black Hawk, zilisafiri kwenda Abbottabad. Ndani kulikuwa na wanajeshi 23, mtafsiri na mbwa wa kusaka anayeitwa Cairo. Wanajeshi watatu walikuwa wamepewa jukumu la kumtafuta Bin Laden.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mpango wa awali, moja ya helikopta ilifaa kuelea juu ya jengo kuu ili kuwaruhusu wanajeshi kuteremeka kwa kamba hadi paa la jengo hilo . Nyingine ilifaa kuwacha wanajeshi ndani ya uwanja uliomo katika jumba alilokuwemo Bin laden ili oparesheni yote ifanyike kwa kimya kikubwa bila kuwaamsha watu
Wakati CIA ilipozindua Operesheni ya kumuua au kumkamata Osama Bin Laden mnamo Mei 2011, Marekani iliamua kutoijulisha Pakistan wakati timu za wanajeshi wa kikosi maalum zilipotumia helikopta kuingia kwa siri katika anga ya Pakistan .
Waliogopa mtu angempa Bin Laden habari na kumfanya atoroke
Operesheni dhidi ya Saddam Hussein
Operation Red Dawn ilikuwa ya jeshi la Marekani iliyoifanywa tarehe 13 Disemba 2003 katika mji wa Ad-Dawr, karibu na Tikrit nchini Iraq, iliyopeleka kukamatwa kwa dikteta wa Iraq Saddam Hussein.
Oparesheni hiyo ilipewa jina hilo kutokana na filamu ya mwaka wa 1984 kwa jina film Red Dawn.
Baada ya vita vya vilivyopeleka kuondolewa kwake madarakani.Majeshi ya Marekani yalianza kumsaka Saddam Hussein na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa serikal yake .
Alikamatwa baada ya kutolewa kwa zilizowaelekeza wanajeshi wa Marekani kwenye shimo dogo, chini ya ardhi lililofichwa karibu na majengo ya shamba karibu na mji alikozaliwa wa Tikrit.

Wanajeshi walikuwa karibu kutupa guruneti ndani ya shimo hilo, wakati Saddam Hussein alipoibuka na kujisalimisha, Kanali James Hickey aliyeongoza oparesheni hiyo alisema.
Sehemu hiyo muhimu ya habari ilipatikana kutoka kwa mtu ambaye alikuwa amekamatwa siku iliyopita huko Baghdad, alisema.
Ingawa eneo hilo lilikuwa limetafutwa hapo awali, inawezekana Saddam Hussein hakuwapo, kwani alifikiriwa alikuwa akikwepa sehemu moja hadi nyingine baada ya kupashwa habari
Hakuna simu za rununu au vifaa vingine vya mawasiliano vilivyopatikana, ikidokeza kwamba Saddam Hussein alikuwa akitoa "msaada wa maadili" na hakuwa akiratibu tena harakati za mapigano ya wanamgambo wa Iraq, Meja Jenerali Odierno aliongeza.
Kamanda wa juu wa jeshi la Marekani nchini Iraq, Luteni Jenerali Ricardo Sanchez alisema dikteta huyo wa zamani alikuwa "akizungumza sana na alishirikiana nao' na hakuwa na majeraha -alikuwa na afya njema.
Wanajeshi walipata pesa taslimu $ 750,000 kwa noti za dola 100, bunduki mbili za AK-47 na mkoba wa nyaraka.
Teksi ya rangi nyeupe na machungwa ilikuwa imeegeshwa karibu na eneo hilo.
Muammar Gaddafi
Wakati upepo wa uasi ulipoanza kuvuma katika ulimwengu wa Kiarabu kutoka Tunisia mnamo Desemba 2010, Libya haikuwa juu ya orodha ya watu wengi wa "nani afuataye".
Gaddafi kwa wengi alikuwa akionekana kama mtawala wa kimabavu ambaye alivumiliwa kwa miaka zaidi mingi kuliko idadi kubwa ya raia wake wanavyoweza kukumbuka. Lakini hakutambuliwa sana kama kibaraka wa magharibi kama viongozi wengine wa Kiarabu, walioshutumiwa kwa kuweka masilahi ya nje mbele ya maslahi ya watu wao wenyewe.
Kadiri maasi yalilivyoenea, na uzito wa tishio kwa utawala wake kuonekana, Gaddafi alionyesha kuwa hakuwa amepoteza unyama wowote ulioelekezwa dhidi ya wapinzani na waliotoroka nchi miaka ya 1970 na 1980.
Wakati huu miji mizima na vijiji vililengwa kwa ukatili wake ambapo watu walikuwa wamethubutu kurarua mabango yake na kutoa wito kumalizika kwa utawala wake . Wanajeshi wa kawaida na mamluki karibu wangewazidi nguvu waasi ambao hawakuwa na mafunzo ya kutosha , wakiwemo wanajeshi waliotoroka vikosi vya Gaddafi chini ya mwavuli wa Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC).

Kuingilia kati kwa Nato kwa upande wa waasi mnamo Machi, baada ya kuidhinishwa na azimio la UN lililotaka ulinzi wa raia, ulizuia maangamizi yao ambayo yalionekana kuwa karibu - lakini ilikuwa miezi kabla ya kugeuza hali hiyo kuwa faida kwao.
Kisha Tripoli ikaatekwa na waasi na Gaddafi akakimbilia mafichoni bado akidai watu wake walikuwa nyuma yake na kuahidi mafanikio dhidi ya "wavamizi" na "washirika". Utawala wake wa kidikteta ulikuwa umeporomoka, lakini wengi waliogopa kwamba angebaki huru ili kupanga uasi.
Alikutana na mauti yake kwa njia ya aibu na mbaya, wakati vikosi vya NTC vilipompata akijificha kwenye handaki kufuatia shambulio la ndege za Nato kwenye msafara wake alipojaribu kuondoka kutoka ngome yake ya mwisho, jiji la Sirte, ambapo yote yalikuwa yameanzia
Mazingira haswa ya kifo chake hayajawahi kufahamika iwapo "aliuawa katika ufyatulianaji wa risasi, aliuawa kwa kupigwa risasi , au aliuawa kwa kushambuliwa na umati kisha kuburuzwa mitaani na wapiganaji walioshangilia ushindi wao'
Utawala wake wa miaka 42 ulikomea hapo kwa njia ambayo wengi hawakuitarajia kwani mwanapinduzi huyo alikuwa ameingia madarakani kwa kishindo na kuongoza kimabavu bila kujali kwamba mauti yangempata kwa hali kama hiyo akiomba kusamewhewa na waliomkamata wengi wao wakiwa hata hawakuwa wamezaliwa wakati Gaddafi alipokuwa akipindua serikali kuchukua uongozi wa Libya












