Mzozo mpya Somalia: Kitisho cha vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Na Mohammed AbdulRahman
- Nafasi, Mchambuzi
Umezuka wasiwasi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu baada ya mapigano makali ya risasi Jumapili na Jumatatu ya wiki hii, Kati ya majeshi yanayomuunga mkono Rais Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kwa jina la "Farmaajo", na makundi ya wanamgambo yanayowaunga mkono wapinzani wake.
Matukio hayo chanzo chake ni hatua ya kiongozi huyo kushindwa kuandaa uchaguzi mkuu mpya wa Rais na Bunge uliotarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka huu baada ya muhula wake kumalizika.
Badala yake aliamua kusaini sharia ya kurefusha kipindi chake cha kubakia madarakani kwa miaka miwili. Uamuzi wake ulitanguliwa na mazungumzo magumu ya miezi kadhaa na wapinzani wake ambayo hayakuzaa matunda.
Hofu iliopo ni kwamba mapigano yanaweza kuzagaa na nchi hiyo kutumbukia katika vita vyengine vya wenyewe kwa wenyewe. Dalili za uwezekano huo, zinafuatia baadhi ya wanajeshi wa waliowatiifu kwa Rais huyo, kujiunga na mahasimu wake.
Mapigano ya karibuni ni miongoni mwa yale mabaya kabisa kuwahi kuonekana katika mji mkuu wa Mogadishu. Wapinzani hao wanadai Farmajo anachukua hatua iliyo kinyume kabisa na katiba.
Ikisaidiwa na Jumuiya ya Kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa Somalia bila mafanikio imekuwa katika jitihada za kuwa na serikali imara ili iweze kupiga hatua ya ujenzi mpya, tokea ilipotumbukia kwenye dimbwi la machafuko na vita 1991, baada ya kuangushwa kwa utawala wa Mohamed Siad Barre.
Inaelekea lengo la Mohamed Abdullahi ni uchu wa madaraka na kuendelea kubaki madarakani baada ya kipindi chake cha miaka minne kumalizika.
Licha ya kuonywa na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Marekani ambayo imetishia kumuwekea vikwazo, kiongozi huyo hayatii manani na aliamua kuendelea na mpango wake.
Kitisho kikubwa cha mgogoro huu mpya nchini Somalia, siyo katika suala la amani ya Somalia pekee, lakini ni kwa mchakato wa amani na utulivu katika pembe ya Afrika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa Jumuiya ya Kimataifa itakuwa imechoshwa na Somalia ambayo baada ya miongo mitatu ya machafuko, haitomudu hata hivyo kuipa kisogo Somalia, kwani utakuwa ni mtihani mgumu pindi ikirejea tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Tatizo jengine ni kujiingiza kwa namna moja au nyengine kwa mataifa ya kigeni. Kwa mfano Eritrea inasemekana kumuunga mkono Rais Farmaajo na kuna ushawishi mkubwa wa Uturuki na Qatar.
Changamoto nyengine ni kubadilika kwa hali ya kisiasa katika pembe ya Afrika kinyume na matarajio ya wakazi wake.
Itakumbukwa alipoingia madarakani Aprili 2018, Waziri mkuu wa Ethiopia Dr Abiy Ahmed alijitolea kuanza jitihada za kuleta amani katika kanda hiyo, akianza na upatanishi kati ya nchi yake na Eritrea, uhasama uliodumu miongo miwili.
Pia akazipatanisha Eritrea na Djibouti na kusaidia kupatikana suluhisho la mzozo wa kisiasa Sudan baada ya kuangushwa utawala wa Rais Omar Hassan al Bashir 2019, kwa kuundwa serikali ya pamoja kati ya wanajeshi na raia kuongoza kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kidemokrasi.
Lakini kipindi hiki kifupi kisichozidi miaka mitatu mchache kimeibadili sura ya pembe ya Afrika kutoka kwenye matumaini hadi kwenye matatizo mapya yasiyotarajiwa.
Mpatanishi Ethiopia sasa yenyewe ina mgogoro na Sudan aliojiunga na Misri kuhusu uamuzi wa Ethiopia kujenga bwawa kubwa kwa kutumia maji ya mto Nile na pia mgogoro wa mpaka. Ethiopia ilichukuwa hatua ya kijeshi kukandamiza jaribio la kujitenga jimbo lake la Tigray, kulikopelekea pia majeshi ya Eritrea kuingia katika jimbo hilo kupigana na waasi.
Si hayo tu, Desemba 2020 Somalia na Kenya ziliingia kwenye mzozo wa kidiplomasia na kuvunja uhusiano, baada ya Somalia kudai kwamba jirani yake anaingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na tangu wakati huo uhusiano wao haujawa mzuri.
Kenya ina karibu wanajeshi 3,600 kusini mwa Somalia katika kampeni dhidi ya wapiganaji wa Al-Shabab wakiwa sehemu ya kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika. Al Shabab wanayadhibiti maeneo makubwa ya kati na kusini mwa Somalia.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Somalia
Kuzuka kwa machafuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa mara nyengine tena kutasababisha mtihani mkubwa kwa Kenya katika suala zima la usalama katika mpaka wake wa kaskazini na Somalia. Al Shabab wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda , wamefanya mashambulizi mara kadhaa ndani ya Kenya, likiwemo lile baya kabisa 2013 dhidi ya kituo cha biashara cha Westgate mjini Nairobi ambapo zaidi ya watu 60 waliuwawa.
Kundi hilo la wanamgambo linayadhibiti maeneo ya kati na kusini mwa Somalia na kuhusika katika mashambulizi kadhaa dhidi ya serikali katika mji mkuu Mogadishu.
Kinachoisibu Somalia ni kuendelea kuwepo kwa hisia za kikoo na ushawishi wa koo hizo katika uongozi wa taifa hilo. Farmaajo aliyeshika hatamu za uongozi baada ya kuwashinda marais wawili wa zamani walioshindana naye 201, ameshindwa kuwapa Wasomali na Jumuiya ya Kimataifa lile walilolitarajia.
Raia huyo wa zamani wa Marekani alifikiriwa angechangia katika safari ya kuelekea katika utekelezaji wa utawala bora hatua kwa hatua, kwa kuandaa uchaguzi na kuondoka kwa heshima.
Mwanasiasa huyo amedhihirisha kuwa hana tafauti na wababe wa kivita waliomtangulia kama Mohamed Farah Aidid na mshirika wake Osman Hassan Ali Atto.
Baadhi ya wababe hao hawakuvitumia vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe kuwania madaraka, lakini pia kujilimbikizia utajiri. Wengi waliishia hatimae kwenda uhamishoni.
Jumuiya ya Kimataifa kwa mara nyengine tena inajikuta ikikabiliwa na tatizo sugu la kuitafutia suluhisho Somalia. Kiroja cha mambo Rais Farmaajo ameelezea kuwa tayari kuzungumza na wapinzani wake na wadau katika mzozo huo kisiasa , wakiwamo wafadhili, ili kutafuta suluhisho.
Amependekeza upatanishi wa Umoja wa Afrika na kuwasiliana na Mwenyekiti wa Umoja huo, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mgogoro ulipofikia, suluhisho pekee litakuwa ni yeye mwenyewe kubatilisha uamuzi wake wa kurefusha kipindi chake kubakia madarakani na hasa kwa kuwa Jumuiya ya Kimataifa ukiwemo Umoja wa Afrika zilimuonya dhidi ya hatua yake hiyo. Ameanza kupoteza pia imani ya raia, ambao wameandamana katika mji mkuu na kupambana na vikosi vya usalama.
Umoja wa Ulaya, Umoja wa mataifa na Marekani hazina budi kuacha kuyaonea haya mataifa yenye mkono wao katika mzozo wa Somalia wakiziunga mkono pande zinazohusika, zikiwemo Qatar na Umoja wa falme za kiarabu zinazosemekana kuisaidia serikali ya Farmaajo. Kwa upande mwengine, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kusaidia kuitafutia amani, lakini suluhisho bado limo mikononi mwa Wasomali wenyewe.












