Uchaguzi Tanzania 2020: Marekani yaonya viongozi kuhusu uchaguzi wa Tanzania

Bendera ya Marekani

Marekani imeonya kuwawekea masharti ya usafiri wale wote watakaopatikana na hatia ya kukiuka haki za kibinadamu na kuingilia uchaguzi uliokamilika nchini Tanzania.

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kwamba nchi hiyo itashirikiana na washirika wake kuhakikisha kwamba wale waliohusika wanawajibishwa vilivyo.

''Tunashauri viongozi wa Tanzania wachunguze madai ya ukiukwaji wa sheria na vurugu zilizofanywa na vikosi vya usalama na kuhakikisha kuwa wahusika wote wa kisiasa wanapata haki ya kuangazia kwa amani mizozo ya uchaguzi,'' inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na naibu msemaji wa wizara Cole Brown.

Bwana Brown ameeleza kuwa Watanzania , kama raia wengine kokote kule wanastahili utawala wa uwazi na uwajibikaji, kutendewa sawa chini ya sheria, na uwezo wa kutekeleza haki zao bila hofu ya adhabu.

Rais John Pombe Magufuli ndiye aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais na tume ya uchaguzi nchini humo NEC baada ya kujizolea asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.

Hata hivyo upinzani umepinga matokeo ya uchaguzi huo na kutaka kurudiwa.

Kwa mujibu wa wapinzani, uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kufuatia visa vya udanganyifu wa kura na na kuzuiwa kwa mawakala wao kuingia katika vituo vya kupigia kura.

Madai hayo yamepingwa vikali na tume ya uchaguzi NEC inayosema kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Lakini katika taarifa yake, wizara hiyo ya msuala ya kigeni nchini Marekani imeendelea kusema kwamba licha ya raia wa Tanzania kushiriki katika shughuli ya kupiga katika uchaguzi huo: ''Walakini, tunaendelea kushangazwa na ripoti za kuaminika za ukiukwaji mkubwa wa zoezi hilo, kubanwa kwa mtandao, kukamatwa, na vurugu zinazotekelezwa na vikosi vya usalama nchini Tanzania Bara na kwa Zanzibar''.

Bwana Brown amesema kwamba makosa yaliofanyika katika uchaguzi huo wa kihistoria yanatilia shaka kujitolea kwa Tanzania kufuata maadili ya kidemokrasia.

''Huku Tume ya Uchaguzi ya Tanzania NEC ikimtangaza Rais Magufuli mnamo Oktoba 30 kama mshindi wa kinyang'anyiro cha urais, tunawasiwasi sana na athari za makosa na vurugu zilizotokea katika matokeo hayo.''

Taarifa hiyo pia imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu na uhuru wao wa kujieleza pamoja na ule wa kukongamana mbali na kufungua mitandao ya kijamii na kuhakikisha kuwa wote waliokamatwa wakati wa maandamno wanalindwa.

Wizara hiyo imeongezea kwamba kwa Tanzania na Marekani kuafikia malengo yake na kuendeleza uhusiano huo ,kutalazimu kwamba wadau wanawakilishwa vyema na wanaweza kuchukua majukumu yao katika demokrasia ya taifa la Tanzania.

Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Profesa Paramagamba kabudi kuzungumzia taarifa hiyo ya Marekani zinaendelea.

Lakini Je NEC iu madai yaliowasilishwa na upinzani?mesemaje kuhus

Tume ya taifa ya uchaguzi imesema kwamba malalamishi hayo hayana ukweli kupitia kwa mwenyekiti wake, Jaji Kaijage.

''Kuna taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa masanduku ya kura feki katika majimbo ya Kawe Dar es Salaam, Pangani Tanga na Buhigwe Kigoma',' alisema Bw. Kaijage.

Aliongeza kuwa taarifa ya madai hayo jumla na ambayo sio rasmi hayajathibitishwa na hayaelezi ni vituo vipi vilihusika na matokeo hayo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema haijapokea taarifa ya madai kama hayo.