Uchaguzi Tanzania 2020: Jamii ya kimataifa yatoa maoni yake

Chanzo cha picha, James Duddrige/Twitter
Maoni tofauti yanaendelea kutolewa duniani kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu nchini Tanzania .
Uchaguzi huo uliomtangaza mshindi kwa asilimia 84 rais John Pombe Magufuli ulizongwa na madai ya wizi wa kura na kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani.
Kulingana na taarifa iliotolewa na Uingereza na kuchapishwa tarehe mosi mwezi Novemba, Taifa hilo sasa linajiunga na mataifa mengine katika kuitisha uchunguzi huru ufanywe ili kuondoa wasiwasi unaozidi kuenea katika taifa hilo la Afrika mashariki.
Waziri wa masuala ya Afrika James Duddridge amesema kwamba Uingereza inashangazwa na ripoti za ghasia na kiwango cha juu cha maafisa wa polisi katika vituo vya kupigia kura ikiwemo suala zima la kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Amesema kwamba Uingereza pia ina wasiwasi kuhusu madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi huo, kujazwa kwa kura katika masanduku ya kupigia kura na kuzuiliwa kwa mawakala wa vyama vya upinzani kuingia katika vituo vya kupigia kura.
Vilevile taifa hilo limeshangazwa na madai ya ripoti za ghasia na kiwango kikubwa cha maafisa wa polisi katika vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi, ikiwemo kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani.
Kulingana na taarifa hiyo , Uingereza imesema kwamba kwa Tanzania kuwa dhabiti na kustawi katika siku za usoni , itahitaji mchakato wa kidemokrasia ulio huru na wa haki, unaoungwa mkono na vyombo vya habari vilivyo huru.
Vilevile imewataka wote waliohusika kusimamamia zoezi hilo la kihistoria ikiwemo vikosi vya usalama kuchukua hatua ili kupunguza kiwango cha hali ya wasiwasi iliopo.
Taarifa hiyo ya Uingereza inajiri siku chache baada ya ubalozi wa Marekani pia kutaka masuala yalioangaziwa na upinzani kushughulikiwa.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulizitaka mamlaka za taifa hilo la Afrika mashariki kushirikiana na wadau mbalimbali kushughulikia kwa uwazi malalamiko yanayotolewa kuhusu uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Ubalozi huo kupitia tamko lake lililotolewa Oktoba 29, mwaka huu unasema kufanya hivyo kutarejesha imani na kutekeleza azma ya kuheshimu utawala wa sheria na dhana ya utawala bora.
Moja ya malalamiko yaliyotajwa na ubalozi huo ni kuhusu uwepo wa kura feki katika uchaguzi huo
Hatahivyo uchaguzi huo umepongezwa na baadhi ya viongozi wa Afrika.
Rais mpya wa Burundi Evariste Ndayishimie amempongeza rais magufuli kwa ushindi wake huku akiwapongeza raia wa Tanzania kwa kufanya uamuzi wa amani na kuonesha ukomavu wa kidemokrasia.
Hatua ya rais huyo inajiri siku chache tu baada ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kumtumia salamu za heri rais John Pombe Magufuli kwa kushinda uchaguzi huo.
Rais Kenyatta amesema kuchaguliwa tena kwa Magufuli ni ishara ya upendo na imani waliyo nayo Watanzania kwa uongozi wake.
"Kwa niaba ya Watu, Serikali ya Kenya na Mimi mwenyewe nampongeza ndugu yangu, Dkt John Pombe Magufuli kwa ushindi wako na wa Chama Cha Mapinduzi, katika uchaguzi uliomalizika", alisema rais Kenyatta.
Aliongeza kuandika: ''Nchi ya Kenya inatarajia kuendelea kufanya kazi na Utawala wako kwa faida ya watu wa mataifa yetu mawili, kwa ustawi wa Afrika Mashariki na kwa amani, utulivu na ukuaji wa bara la Afrika.
Rais Kenyatta pia amemtakia rais mwenzake wa Tanzania afya njema na ufanisi anapojiandaa kuhudumu kwa muhula wa pili madarakani na kumhakikishia ushirikiano wa Kenya na kwa utawala wake.
Lakini Je NEC imesemaje kuhusu madai yaliowasilishwa na upinzani?
Tume ya taifa ya uchaguzi imesema kwamba malalaimishi hayo hayana ukweli kupitia kwa mwenyekiti wake, Jaji Kaijage.
''Kuna taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa masanduku ya kura feki katika majimbo ya Kawe Dar es Salaam, Pangani Tanga na Buhigwe Kigoma',' alisema Bw. Kaijage.
Aliongeza kuwa taarifa ya madai hayo jumla na ambayo sio rasmi hayajathibitishwa na hayaelezi ni vituo vipi vilihusika na matokeo hayo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema haijapokea taarifa ya madai kama hayo.














