Je, wakati umewadia kwa DRC kuzungumza na waasi?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Wanyama wa Chebusiri
- Nafasi, BBC Africa, Nairobi
Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinasema kuwa watu 11 wameuawa usiku wa kuamkia leo katika wimbi jipya la mashambulio katika eneo la Beni mashariki mwa nchi hiyo.
Mauaji hayo yanafikisha idadi ya watu 33 kuuwawa na waasi waliojihami chini ya saa 24.
Viongozi wa eneo hilo wanadai kuwa waliohusika na mauaji hayo ni wanamgambo wa kundi la waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kutoka nchi jirani ya Uganda.
Wanawake 13 ni miongoni mwa watu 22 waliouawa na waasi wa ADF usiku wa Jumamosi.
Mauaji ya wanavijiji hao ni msururu wa ukatili na vifo vinavyoendelea kuwapata raia wasiokuwa na hatia katika mkoa wa Kivu kaskazini, licha ya serikali kuanzisha operesheni mahsusi ya kijeshi ya kutokomeza makundi ya waasi yaliyo na ngome zake eneo hilo.
Zaidi ya raia 180 wameuwawa tangu mwezi Oktoba mwaka huu wakati jeshi lilipotangaza operesheni dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha wanaotuhumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia.
Wanamgambo hao wanadaiwa kuwalenga wanavijiji kama hatua ya kuwazuia wasiwasaidie wanajeshi.
Mashambulio ya hivi karibuni yamezua hasira na maandamano makali miongoni mwa wakaazi amabo wanalaumu vikosi vya kulinda usalama vya umoja wa mataifa kwa kutowahakikishia usalama.
Jambo linalozua mjadala ni kwamba rais Felix Tshishekedi amezuru eneo hilo mara kadhaa na kutoa ahadi za kufanya kila liwezekanalo kuwalinda raia na mali zao.

Chanzo cha picha, Reuters
Kitovu cha mapigano Beni
Mji wa Beni, wenye idadi ya watu laki mbili ndio umelengwa sana na mashambulizi ya waasi.
Beni ni mji ambao pia umekumbwa na mlipuko wa homa hatari ya Ebola ambayo imesababisha vifo vya watu 2000.
Operesheni za jeshi la taifa na za vikosi vya umoja wa mataifa vya kulinda amani zina ngome zake katika mji huu wa Beni.
Mnamo mwezi Novemba mwaka huu, raia wenye hasira waliandamana mjini Beni baada ya mauaji ya kinyama ya watu wanane na kuwashtumu askari wa umoja wa mataifa kwa kutowalinda dhidi ya mashambulizi ya waasi.
Ofisi ya meya wa mji huo pia ilichomwa wakati wa maandamano hayo.
Mara kadhaa Meya wa Beni bwana Masumbuko Nyonyi Bwanakawa anapohojiwa na BBC huwa anajibu kuwa, kinachojitokeza bayana ni kwamba waasi wanaonekana kuwashinda maarifa wanajeshi wa serikali na wale wa Umoja wa Mataifa ambao wametumwa kuwasaka wapiganaji wa kuvizia hasa wale wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda, ambao wananyoshewa kidole kwa mauaji ya kikatili dhidi ya raia yanayoendelea kwa sasa kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kuzungumuza na waasi?
Tangu mwanzo wa mwezi Novemba jeshi la DR Congo limekuwa likisisitiza kuwa linafanya kazi peke yake kukabiliana na waasi wa Allied Democratic Forces au ADF.
Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilitengwa na vimekuwa vikisaidia kutoa taarifa za kiintelijensia na kuwaondoa maafisa wanaojeruhiwa vitani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa jeshi la Congo halikutaka operesheni hiyo ichunguzwe kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini kutokana na ghasia za siku ya Jumatatu katika mji wa Beni ambazo zilichangiwa na kokosa kuwalinda raia, rais Felix Tshisekedi ametoa wito wa kufanyika kwa operesheni ya pamoja.
Katika miezi iliopita kundi la ADF lilidhaniwa limefifia- baada ya wapiganaji wake kadhaa kuuwawa.
Lakini limethibitisha bado liko hai kutokana na mfumo wao wa mashambulizi ya kuvizia ambapo walitumia mapanga kuwaua raia 80.
Mmojwapo ya mapendekezo ambayo yametolewa katika juhudi za kujaribu kupata suluhu la kiuslama la kudumu ni serikali kufanya mazungmzo na wapiganaji hasa wale wa kundi la ADF.
Mchanganuzi wa maswala ya kisiasa na kijamii katika mji wa Goma bwana Apollo Msambia anaamini kwamba wakati umewadia kwa serikali ya Kinshasa kuanzisha mazungmzo ya amani na utawala wa rais Yoweri Museveni wa Uganda kuhusu waasi wa ADF.
"Rais Tshishekedi anatakiwa kuanzisha mazungmzo na mwenzake Museveni na kuona jinsi waasi hawa wa ADF wanavyoweza kutoka kaskazini mwa DRC na kurejea Uganda, kwa vile sasa imeonekana kwamba wameshindwa kukabiliana nao kijeshi" asema bw. Msambia.

Chanzo cha picha, WIZARA YA MAMBO YA NJE UGANDA
Ushirikiano wa kijeshi wa mataifa jirani unahitajika
Katika kukabiliana na makundi ya waasi yenye ngome zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ushirikiano wa kijeshi wa mataifa jirani kama vile Uganda, Rwanda na Burundi unahitajika.
Yafaa serikali za mataifa haya zijitolee kwa hali na mali na kuwashirikiana na serikali ya rais Tshishekedi katika kukabiliana na waasi.
Waasi wanaishi na kujumuika na jamii na hivyo basi inakuwa vigumu kuwatofautisha na raia wema.
Kwa hivyo, yafaa vikosi vya usalama kujenga uhusiano mwema na wa kuaminika na raia ili watoe taarifa za kijasusi kuhusu mipango ya waasi.
Yafaa pia serikali kuchunguza na kuchukuwa hatua madhubuti kuhusu madai kwamba baadhi ya wanajeshi na wanasiasa wanafadhili na kuunga mkono makundi ya waasi.
Wasaliti wa kijeshi na wa kisiasa wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa vita dhidi ya waasi vitafaulu.
Lakini je, unaamini kwamba kuanzisha mazungumuzo ya amani na waasi wa ADF, pamoja na serikali ya Uganda kutaleta suluhu la kudumu kuhusu suala la ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo?













