DRC: Kwanini wanamgambo wenye silaha wanaendelea na ukatili dhidi ya raia ilhali kuna kikosi cha MONUSCO?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Wanyama wa Chebusiri
- Nafasi, BBC Africa, Nairobi
Historia ya hivi karibuni ya Jamhuri ya Kidemokrsaia ya Congo imekuwa ya taifa lililozongwa na ukosefu wa usalama, licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa unaotoakana na madini na rasilimali.
Ukosefu huu wa usalama, ambao umekithiri sana mashariki mwa nchi hiyo, umetia doa historia nzuri iliaondikishwa mapema mwaka huu kufwatia uchaguzi kufanyika na rais kukabiliwa madaraka bila umwagikaji damu.
Alipochukuwa hatamu ya uongozi mnamo Januari mwaka wa 2019 rais Felix Tsishekedi alirithi majanga kadhaa, ikiwemo lile la homa hatari ya Ebola iliyotishia afya ya taifa zima la DRC, na pia mapigano yanayoendelea mashariki mwa taifa hilo hasa maeneo ya Beni, Butembo na mkoa wa Kivu kaskazini.
Mamia wameuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao.
Kutokana na ukosefu wa usalama, wakaazi wenye hasira katika miji ya Beni, Butembo na Goma wamekuwa wakiandamana tangu mwanzo wa wiki hii kulalamikia majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa maarufu kama MONUSCO kwa kutowalinda dhidi ya mashambulizi ya wanamgambo waliokita mizizi mashariki mwa taifa hilo.
Afisi ya meya wa Beni lilichomwa moto pamoja na kituo cha askari wa MUNUSCO wakati wa maandamano hayo.
Lakini swali kuu ambalo limesalia kwenye vinywa vya wengi ni je, kwanini wanamgambo wenye silaha wanaendelea na ukatili dhidi ya raia ilhali kuna kikosi cha MONUSCO chenye askari zaidi ya alfu sita?
Na je, inakuwaje operesheni mahsusi ya kijeshi iliyoanzishwa hivi karibuni na vikosi vya usalama vya DRC inaendelea huku raia raia wakiendelea kuwauwa kinyama na makundi ya wanamgambo mashariki mwa nchi hiyo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Nalo kanisa katoliki, lililo na ushawishi mkubwa katika maswala ya DRC, limetoa mwito serikali ya rais Tsishekedi kufanya kile iwezalo kukomesha mausaji ya raia.
Wachanganuzi wa maswala ya kiuslama wanasema kwamba yafaa majukumu ya vikosi vya umoja wa mataifa ndani ya DRC yabadilishwe.
Mmojawao ni George Musamali anayetoa tetesi kwamba wakati umewadia kwa MONUSCO kupigana vita.
"Umoja wa mataifa yafaa uchukuwe uamuzi wa haraka na kutoa idhini kwa wanajeshi wa kulinda amani waanze kupigana vita dhidi ya wanamgambo wenye silaha mashariki mwa DRC...wakishirikiana na wanajeshi wa serikali, watakabiliana vilivyo na wapiganaji waasi" anasema Bwana Musamali.
Kwa sasa wanajeshi wa MUNUSCO wanaweza tu kutumia silaha zao kujilinda iwapo wamevamiwa lakini hawaruhusiwi kwenda kwenye uwanja wa vita.
Wanamgambo kung'ang'ania madini
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni eneo lenye aina nyingi ya madini ikiwa pamoja na almasi na dhahabu.
Pia ni eneo lenye mchanga wenye rotuba na misitu ya nyanda za juu inayozalisha mbao za ujenzi zinazotafutwa sana na wafanyabiashara hata kutoka nje ya DRC.
Kutokana na rasimali hii, eneo hili la mashariki mwa DRC limegeuzwa kuwa uwanja wa vita miongoni mwa makundi ya wapiganaji wa ndani ya DRC na wengine kutoka mataifa jirani.
Inaaminika kwamba kuna zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo wenye silaha walio na ngome zao mashariki mwa DRC, lengo lao kuu ni kung'ang'ania madini na raslimali nyingine inayopatikana huko.
Waasi wa kundi la Mai Mai ndio wanaolaumiwa kwa ukosefu wa usalama katika mikoa mingi ya mashariki mwa DRC.
Vile vile kuna makundi ya FDLR kutoka Rwanda, ADF kutoka Uganda na CNRD/FNL kutoka Burundi ambayo ni miongoni mwa magenge haramu yanayochangia kukithiri kwa vita vya kiraia nchini DRC.
Mwingilio wa kisiasa
Kundi la Mai Mai lilianzishwa na kufadhiliwa na wanasiasa wanaotaka mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Inasemakena kwamba wanasiasa wengi nchini DRC wana magenge yao ya kibinafsi ambayo, baada ya kukamilika kwa msimu wa kisiasa, yanajihusisha na uhalifu na uporaji.

Mzozo wa kikabila
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekumbwa na mzozo wa muda mrefu wa kikabila kati ya wafugaji na wakulima.
Uhasama kati ya makundi haya mawili umekithiri kiasi kwamba makabila mengi hayaonani ana kwa ana.
Uasi ndani ya jeshi
Miongoni mwa sababu ambazo zimetajwa kulemaza juhudi za jeshi la taifa zisifaulu katika vita dhidi ya makundi ya waasi ni baadhi ya wanajeshi kuunga mkono kisirisiri wanamgambo.
Uasi wa kichini chini ndani ya jeshi unafanya wanamgambo kufahamu mipango yote ya operesheni dhidi yao na hivyo kulemaza harakati za vikosi vya taifa vya kutokomeza makundi ya wanamgambo.
Rais Felix Tsishekedi ametoa wito wa ushirikiano wa kikanda na kimatifa katika kupambana na makundi ya wanamgambo mashariki wa DRC.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema baadhi ya serikali za mataifa jirani zinanufaika kutokana na ukosefu wa usalama na huenda wasiitikie mwito wa kiongozi huyo wa DRC.
Jambo la kusikitisha ni kwamba raia ndio wanaoteseka na kuumia huku sakata ya ukosefu wa usalama ikiendelea kulikumba eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.














