Amri ya kutotoka nje yatangazwa mjini Beni mashariki mwa DR Congo

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza hali ya hatari na msako wa nyumba hadi nyumba kila siku kati ya saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi maeneo ya Beni.
Gavana wa mkoa wa Kivu kaskazini Charly Nzazu Kasivita, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kikao cha usalama kilichojumuisha wajumbe wa jeshi, polisi pamoja na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kutokana na msururu wa maandamano ya kulalamikia mauaji ya raia.
Licha ya serikali kusema kuwa hatua hiyo ni moja ya njia mbadala ya kubaini maficho ya maadui na pia kulinda usalama wa raia, baadhi ya watu hawajaridhishwa nayo.
Hatua hiyo imepokelewaje?Wanasema kuwa hatua hiyo inawanyima uhuru wa kutembea hasa wafanyibiashara wa usiku kama vile boda boda, migahawa pamoja na hoteli.
''Serikali ni bora ichukuwe mbinu nyingine na wala sio hii ya msako kwani itakuwa vigumu kudhibiti vilabu na pia raia wanaojificha vichakani'' anasema wakili Omari Kavota kutoka shirika la la kutetea haki la CEPADHO
Bwana Kavota anasema kuwa watu wanaogopa kutoka majumbani mwao kwa kuhofu ya usalama wao.Kikundi cha waasi wa Uganda kiliwauwa takriban watu 8 katika mji wa Beni usiku wa jana na kusababisha raia wenye hasira kali kuandamana katika mji huo kupinga mauaji hayo.
Waandamanaji walilalamikia vikosi vya jeshi la Congo pamoja na vile vya kulinda amani nchini DRC Monusco kushindwa kuwapa usalama.
Ofisi za Meya wa mji wa Beni, pamoja na zile za MONUSCO pia zilichomwa moto.

Chanzo cha picha, Reuters
Mapema leo wanafuzi wa chuo Kikuu mjini Goma walifunga barabara na kuelekea katika kambi za MONUSCO wakiwalalamikia kutotenda kazi zao vizuri huku wakiomba vikosi hivyo ambavyo vimekuwa na miaka 20 nchini humo kuondoka.Wanafunzi hao walifunga barabara na kuweka magurudumu njiani lakini polisi iliingilia kati na imefanikiwa kuwatawanya .Mwandishi wa BBC mjini Goma, anasema kuwa ameona mawe mengi yakiwekwa barabarani na waandamanaji wenye hasira na ambao wanasema kuwa jamii ya watu wa Beni.
Katika taarifa iliyotumwa kwa njia ya barua pepe, msemaji wa Monusco, Mathias Gillmann, alisema mashambulio dhidi ya kambi ya walinda usalama wa Umoja wa mataifa yaliathiri vita dhidi ya ADF.
"Monusco inaelezea hofu yake kuhusu kusambazwa kwsa taarifa za uongo na za kupotosha kushinikiza watu kufanya ghasia katika mitandao ya kijamii," iliongeza taarifa hiyo
Tangu mwanzo wa mwezi huu jeshi la DR Congo limekuwa likisisitiza kuwa linafanya kazi peke yake kukabiliana na waasi wa Allied Democratic Forces au ADF.
Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilitengwa na vimekuwa vikisaidia kutoa taarifa za kiintelijensia na kuwaondoa maafisa wanaojeruhiwa vitani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa jeshi la Congo halikutaka operesheni hiyo ichunguzwe kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini kutokana na ghasia za siku ya Jumatatu katika mji wa Beni ambazo zilichangiwa na kokosa kuwalinda raia, rais Felix Tshisekedi ametoa wito wa kufanyika kwa operesheni ya pamoja.
Katika miezi iliopita kundi la ADF lilidhaniwa limefifia- baada ya wapiganaji wake kadhaa kuuawa.
Lakini limethibitisha bado liko hai kutokana na mfumo wao wa mashambulizi ya kuvizia ambapo walitumia mapanga kuwaua raia 80.













