Stena Impero: Meli hiyo ya Uingereza imeanza kuondoka Iran baada ya kuachiliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Meli iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza sasa inaondoka nchini Iran baada ya kukamatwa kwa zaidi ya miezi miwili.
Mmiliki wa meli ya Stena Impero ambaye ni raia wa Sweden amesema kuwa ipo safarini kutoka bandari ya Bandar Abbas , ambapo ilikuwa imeegeshwa tangu mwezi Julai.
Meli hiyo ilikamatwa na wanajeshi wa Iran katika mkondo wa Hormuz baada ya kuishutumu kwa kuvunja sheria za baharini.
Maafisa wanasema kwamba iliondoka na kuelekea katika maji ya kimataifa saa moja unusu saa za Afrika mashariki siku ya Ijumaa alfajiri.
Erik Hanell, afisa mtendaji wa Stena Bulk amesema kwamba meli hiyo itaelekea Dubai ambapo wafanyakazi wake watazungumziwa na kufanyiwa vipimo vya matibabu.
''Familia za wafanyakazi wa meli hiyo zimeelezwa kwamba kampuni hiyo kwa sasa inafanya mipango ya kuwarudisha makwao wafanyakazi wake haraka iwezekanavyo'', alisema katika taarifa.
Kukamtwa kwa meli hiyo tarehe 19 mwezi Julai kunajiri wiki mbili baada ya meli moja ya Iran kuzuiwa Gibraltar kupitia usaidizi wa wanamaji wa Uingereza.
Meli hiyo ilituhumiwa kukiuka vikwazo vya muungano wa Ulaya nchini Syria , lakini liachiliwa mwezi Agosti.
Operesheni dhidi ya Sterno Impero ilionekana kama kisasi cha jukumu la Uingereza katika kusaidia kuikamata meli hiyo ya Iran madai ambayo Iran imekana.
Kwa nini meli hiyo ilikamatwa?


Tukio hili limefanyika wakati kukiwa na mvutano kati ya Uingereza, Marekani na Iran.
Jeshi limesema meli hiyo imekamatwa kwa kuvunjwa kwa sheria tatu: kuzima GPS; Kuingia kwenye mpaka kupitia njia ya kutokea badala ya kuingilia; na kupuuza onyo.
Taarifa zinasema hakuna taarifa zozote kuhusu majeruhi na usalama wa wafanyakazi ni jambo la kwanza kwa wamiliki na mameneja.
Tarehe 9 mwezi Julai, Uingereza ilieleza tishio la usalama katika maji ya Iran kwenye Ghuba ni ''kubwa''.














