Mzozo wa meli ya Iran: Mafuta yauzwa licha ya vitisha vya Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Meli ya mafuta iliyokuwa ikishukiwa kujaribu kufikisha mafuta ya Iran nchini Syria licha ya vikwazo vya kimataifa hatimaye imeuza shehena iliyokuwa ikisafirisha.
Picha za satelaiti zinaonesha kuwa meli hiyo Adrian Darya-1, ilikuwa karibu na pwani ya Syria mpaka Ijumaa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran hata hivyo amesema meli hizo imefikisha mzigo baada ya kutia nanga kwenye "pwani ya bahari ya Meditterania."
Meli hiyo imekuwa katikati ya mzozo wa kidiplomasia baina ya Marekani na Iran, na ilikuwa imebeba shehena ya mapipa milioni 2.1 ya mafuta.
Picha za Setilaiti zilitolewa na kampuni ya Maxar ambazo ilisema kuwa zilionyesha eneo la Adrian Darya maili kadhaa kwenye ufukwe wa badanri ya Syria wa Tartus Ijumaa.

Chanzo cha picha, Maxar's Technolohies
Ilikamatwa na wanajeshi wa Uingereza karibu na pwani ya Giblatar mwezi Julai na kushikiliwa mpaka Agosti 15 baada ya Iran kutoa hakikisho kuwa meli hiyo haitaelekea Syria.
Marekani imeshatoa onyo la kumuwekea vikwazo vya kiuchumi yeyote atakayenunua mafuta hayo.
"Tutaendelea kuiwekea shinikizo Iran na kama Rais (Trump) alivyosema hakutakuwa na msamaha wa aina yeyote ka mafuta ya Iran," Afisa wa Hazina ya Marekani, Sigal Mandelker ameliambia shirika la habari la kimataifa la Reuters.
Wakati huohuo, meli ya mafuta yenye usajili wa Uingereza ambayo ilikamatwa na Iran katika kile wengi walichoona kuwa ni kulipiza kisasi inakaribia kuachiwa, wizara ya mambo ya nje ya Iran imeeleza.
Meli ya Stena Impero ipo katika hatua za mwisho za kisheria nchini Iran na itaachiliwa "hivi karibuni", msemaji wa wizara wa Iran Abbas Mousavi ameeleza.
Stena Impero ilitiwa nguvuni na mamlaka za Iran Julai 19, kwa kile kilichoitwa kukiuka sheria za bahari - na Iran imekanusha vikali kuwa imefanya hivyo kulipiza kisasi baada ya meli yake kukamatwa na wanamaji wa Uingereza.
Mzozo huu ulianza vipi ?

Chanzo cha picha, STENA BULK
Tukio hili lilitokea wakati kukiwa na mvutano kati ya Uingereza, Marekani na Iran.
Tarehe 9 mwezi Julai, Uingereza ilieleza tishio la usalama katika maji ya Iran kwenye Ghuba ni ''kubwa''.
Wakati huohuo, Marekani ilidai kuwa ilidungua ndege isiyo na rubani kwenye Ghuba, baada ya Iran kushambulia ndege isiyo na rubani katika eneo hilo mwezi Juni.
Raisi wa Marekani Donald Trump alasema atazungumza na Uingereza kufuatia madai kuwa Iran imeikamata meli iliyosajiliwa nchini Uingereza.












