Ongezeko la joto lahatarisha uwepo wa miji iliyopo pwani

Mji wa Mombasa pwani ya Kenya ni miongoni mwa maeneo yaliomo katika hatari ya kuangamia

Chanzo cha picha, Anadolu Agency

Maelezo ya picha, Mji wa Mombasa pwani ya Kenya ni miongoni mwa maeneo yaliomo katika hatari ya kuangamia

Kuna uwezekano wa kuwepo na mabadiliko makubwa ya tabia nchi hivi karibuni kama inavyoelezwa kwenye ripoti ya wanasayansi iliyozua mjadala unaoleta utata.

Katika kuelekea katika mkutano wa jopo la wanasayansi ambao utafanyika wiki hii huko Korea Kusini ukiangalia namna ambavyo dunia inakabiliana na ongezeko la joto kama itafikia nyuzi joto 1.5 katika karne hii.

Hali ambayo inaelezwa kusababisha nchi nyingi zilizopo karibu na bahari kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza miji yao iliyopo pwani.

Mwaka 2018 unatajwa kuwa mwaka wa nne kuwa na joto ukilingalinganishwa na miaka mingine ya karne hii ya 20.

Pemba na Mombasa katika hatari ya kuangamia

Mwanamazingira kutoka asasi ya Green Icon nchini Tanzania, Tajiriel Urioh anasema kama hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi haitapata muafaka wake basi itegemewe kuwa uwekezaji mkubwa ambao umewekwa katika nchi zetu utapotea.

Rasilimali kubwa inayopatikana katika miji ya utalii kama Mombasa kwa mfano ambao umetajwa kupotea baada ya miaka 20, utapoteza asili ya watu wake na bandari inayoongeza ukuaji wa uchumi kutokuwepo tena kama kina cha maji kitaongezeka kutokana na ongezeko la joto.

Tajiriel aliongeza kwa kusema kwamba mabadiliko hatuwezi kuyaona kwa siku moja bali huwa yanaanza taratibu na kuna sehemu nyingine ambazo athari tayari zimeanza kuonekana.

Kwa mfano Pemba katika kisiwa cha Panza , maji zaidi ya mita 100 yameingia nchi kavu na tayari Tanzania tumeshapoteza visiwa viwili kimoja kipo maeneo ya Tanga Pangani na kingine Rufiji'fungu la nyani'.

Pemba

Chanzo cha picha, Bojan Brecelj

Maelezo ya picha, Kisiwa cha Pemba

Fazal Issa kutoka Forum CC, anasema bado hatima ya tatizo hili halijapatikana licha ya kwamba kuna makubaliano ambayo yamekuwa yanawekwa kila wakati ila kila nchi inaangalia nani aanze kuchukua hatua au nani anapaswa kuchukua jukumu zaidi ya taifa lingine.

Ripoti ya tathmini ya awamu ya tano iliyotolewa na IPCC ilikuwa mwaka 2013 walisema wastani wa joto ridi ilikuwa ni nyuzi joto 0.85 na nchi zilizoendelea wanahitajika kuongeza kwa wastani wa joto ridi na kuwa 2.0 wakati nchi zinazoendelea zinataka ziwe 1.5

Fazal anasema tathmini ya mwaka 2013 ilionyesha ongezeko la bahari ni sentimita 19 kutoka nchi kavu ,namba inayoonekana kuwa ndogo wakati tayari katika kisiwa kilichomo Pemba kinachoitwa Tumbe mashariki zaidi ya mita 200 ya nchi kavu yameingiliwa na eneo la maji chumvi.

"Tanzania tumepunguza kiwango cha gesi ukaa kwa juu ya kiwango tulichokubaliana na bado athari zinaonekana upande wetu hivyo kunaulazima kwa kila taifa kuwajibika,kila nchi inatakiwa kutoa mchango wake.

Siasa za kiuchumi zinaathiri mafanikio ya jitihada zilizopo, kwa mfano China inatumia kiwango kikubwa sana ya gesi ukaa na ina idadi ya watu wengi lakini kihistoria China inatambulika kuwa ni nchi inayoendelea na sio iliyoendelea hivyo inaacha kuwajibika kulingana na athari inazozisababisha,ahadi zimekuwa nyingi bila utekelezaji na kujulikana nani anastaili kufanya nini ni changamoto" Fazal alieleza.

utafiti
Maelezo ya picha, Jiji la Dar es Salaam linaweza kuzama baada ya miaka 50

Fazal anasema mji wa Dar es Salaam ukiwa ni miongoni mwa miji ambayo haina miinuko na upo karibu na bahari unatajwa na wanasayansi kuzama katika miaka 50 ijayo .

Mji huu wa Dar es salaam unaweza kuathirika kutokana na ongezeko hilo la joto kama mvua nyingi zitanyesha na miundombinu kuendeea kuwa mibaya.

Jopo la kimataifa la wanasayansi 'Intergovernmental Panel on Climate Change' (IPCC) imetoa utafiti mpya ambao unataka kuonyesha hali halisi ya kisayansi kwa kila nchi kuangalia chanzo cha ongezeko la joto, matokeo yake na suluhisho la ongezeko hilo la joto.

SOPA IMAGES

Chanzo cha picha, SOPA IMAGES

Wakati wa makubaliano ya tabia nchi katika mkataba wa Paris disemba 2015 , mataifa yalikubali kuwa na mikakati ya utekelezaji ya muda mrefu ambayo kila nchi inabidi kuzingatia ikiwa ni pamoja na kupunguza shughuli za viwanda na kuweka jitihada za kukabiliana na ongezeko la joto kutozidi nyuzi joto 1.5.

Katika changamoto na matokeo ya kutunza nyuzi joto 1.5 kama Umoja wa Mataifa ulivyotaka IPCC kutengeneza ripoti maalum ambayo inazitaka nchi kuamua ni namna gani watakabiliana na ongezeko la joto huku wakiendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Ripoti hiyo imeeleza namna ambavyo maisha hayawezi kuwa sawa kwa kuzingatia ongezeko la watu na shughuli zinazotumia nishati chafu inayopelekea dunia kuathirika na ongezeko hilo.

Hivyo basi wakati ni sasa ya kila nchi kuchukua hatua.

Kiwango cha juu cha joto kuwahi kushuhudiwa katika eneo hili

ujoto duniani

Sorry, your browser cannot display this map

Chanzo: Robert A. Rohde/Berkeley Earth. Ramani imeundwa kwa kutumia Carto

Kwa nini ripoti hii ya jopo la wanasayansi inazua mjadala

Kama ahadi zote zilizotolewa za kupunguza matumizi ya nishati chafu kama walivyokubaliana katika makubaliano ya mabadiliko ya tabia nchi Paris basi tutaiona dunia ikiweza kubadilika na kuwa salama mwishoni mwa karne hii.

Baadhi ya wanasayansi wanaona kuwa hakuna muda wa kutosha ili kuchukua hatua ili kufikia malengo ya dunia yaliyojiwekea.

Licha ya kuwa kuna sayansi lakini siasa zinafanya utekelezaji kuwa mgumu,mataifa yaliyoendelea yanaona ugumu kuacha shughuli zilizowafanya wafikie kiwango walichopo cha uchumi huku mataifa yanayoendele yanaona kuwa ili waendelee inawabdi kutumia njia zilezile ambazo waliendelea walitumia.

Hakuna usawa miongoni mwa mataifa ya nani awajibike,katika kutoa usaidi wa fedha ,utaalamu na tekinolojia.

Vilevile mikutano au mipango inatajwa kuwa mingi zaidi ya utekelezaji ,tangu mwaka 1992 juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yalianza lakini kasi ya utekelezaji bado ndogo.

Mombasa ni miongoni mwa miji ambayo inatajwa kupotea baada ya miaka 20 kutokana na ongezeko la joto
Maelezo ya picha, Mombasa ni miongoni mwa miji ambayo inatajwa kupotea baada ya miaka 20 kutokana na ongezeko la joto

Nini kinahitajika kufanyika kuibadili hali basi?

Dkt. Aboud Jumbe kutoka kitengo cha mipango na utafiti katika idara a mazingira Zanzibar anasema kuna haja ya kuwa na juhudi na bidii za ziada za kitaifa kuanzia katika Mipango yote ya Kitaifa ya Uchumi kama nishati, viwanda, maji, uvuvi, kilimo, maliasili, madini, mafura na gesi, ardhi, bahari, makaazi, pamoja na elimu.

Kadhalika ameelezea haja ya kuiweka hatari ya mabadiliko ya tabia nchi katikati ya vipaumbele vipya vya karne ya 21 vya kupambana na hatari ya mabadiliko ya tabia nchi.

'Ni lazima tulione tatizo hili kama ni tishio la usalama wa taifa na maisha yetu' anasema Dkt Aboud.

Ameeleza kuwa ikiwa mataifa yote ulimwenguni pamoja na Marekani yatatekeleza maazimio ya makubaliano ya Paris na kupunguza utoaji wa gesi ya CO2 kufikia kiwango kilichokubaliwa, basi anasema kuna matumaini makubwa sana.