Kwa nini unafaa kutahadhari zaidi ukitafuta taarifa za Kim Kardashian mtandaoni

Chanzo cha picha, Getty Images
Iwapo unatafuta taarifa kuhusu kipindi cha karibuni zaidi cha Keeping Up With the Kardashians kuhusu maisha ya Kim Kardashian-West na jamaa zake, au pengine unatafuta za karibuni zaidi kuhusu Kanye West, au ukipenda YE, unafaa kutahadhari zaidi.
Mwigizaji nyota huyo wa vipindi vya uhalisia kwenye televisheni Kim Kardashian ndiye mtu mashuhuri ambaye ni hatari zaidi kutafuta taarifa kumhusu mtandaoni mwaka 2018.
Hii ni kwa mujibu wa kampuni ya usalama mtandaoni ya McAfee, ambayo ilichunguza matokeo ya kutafuta habari kuwahusu watu mbalimbali na hatari zilizopo.
Walibaini kwamba Kim Kardashian anaongoza kwa matokeo ya kutafuta habari zake kuwa na viunganishi vyenye virusi vya mtandaoni na programu za kudukua na kupora maelezo kuwahusu watu mtandaoni.
Mwaka uliopita, mwanamuziki Craig David ndiye aliyeshikilia nafasi hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamitindo Naomi Campbell ndiye wa pili kwenye orodha hiyo, naye dadake Kim, Kourtney Kardashian wa tatu.
Mwanamuziki Adele na mtangazaji wa kipindi cha televisheni cha Love Island Caroline Flack wanafunga orodha ya watu wa kwanza watano.
McAfee wanasema wadukuzi hutumia sana watu maarufu kujaribu kuwashawishi watu kubofya kwenye link ambazo zitaelekeza mtu kwenye mitandao au ukurasa wa mtandao usio salama.
Mitandao hiyo hutumiwa kuweka programu hatari kwenye kompyuta, kuiba maelezo ya kibinafsi ya mtu na pia kuiba maneno ya siri au nywila.
Wengine walioorodheshwa ni mwigizaji Rose Byrne, mshiriki wa Love Island Kem Cetinay, mwanamuziki Britney Spears, mwigizaji Emma Roberts na mwigizaji Ferne McCann.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtaalamu mkuu katika McAfee anasema katika ulimwengu wa sasa, watu wengi huhamasishwa na nyota wa uigizaji na muziki.
Anasema ni wengi sana hujaribu kuwaiga Kardashian.
Ili kuwa salama mtandaoni, McAfee wanasema mtu anafaa tu kucheza video kutoka kwenye mitandao inayofahamika, na pia kuzoea zaidi mitandao ya kulipiwa. Usibofye kwenye link za taarifa ambazo hauna uhakika nazo.
Kadhalika, hakikisha unatumia programu zenye maboresho ya karibuni zaidi, pamoja na programu za kukabiliana na virusi vya kompyuta.













