Kangi Lugola: Kwanini waziri hataki watuhumiwa wanyimwe dhamana wikendi Tanzania, sheria inasema nini?

Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola, amewataka polisi kukoma kuwanyima watuhumiwa dhamana hasa siku za mapumziko, kwa kisingizio kuwa si siku za kazi.
Waziri huyo alisema jambo hilo ni kinyume cha sheria na mtu yeyote anayestahiki kupewa dhamana anafaa kuhudumiwa katika chini ya saa 24 wakati wowote ule.
Bw Lugola alisema hayo katika kijiji cha Busanza wilayani Uvinza mkoani Kigoma siku ya Jumapili.
"Hii tabia sijui imetoka wapi na imejengeka kwa baadhi ya askari polisi. Eti mtu akiingia mahabusu siku ya Ijumaa ikifika Jumamosi na Jumapili hawatoi dhamana wakisema mpaka Jumatatu. Hii tabia sio sahihi na ife haraka iwezekanavyo," alisema Lugola, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi.
Waziri huyo alisema vituo vya polisi nchini humo huwa vinafanya kazi siku zote za wiki zikiwemo za mapumziko na haoni ni sababu gani inayoweza kuwafanya polisi kutompa mtuhumiwa dhamana.
Aliahidi kuchukua hatua dhidi ya askari yeyote atakayeshindwa kutoa dhamana kwa kosa ambalo linadhaminika.
Kwa mujibu wa waziri huyo, dhamana ni haki ya mtu endapo kosa lake linadhaminika.
Aidha, aliwataka wananchi watakaoombwa fedha ili wapewe dhamana kuripoti tukio hilo kwa maofisa wa ngazi za juu ili askari husika achukuliwe hatua za kinidhamu.
"Kuna tabia iliyozoeleka katika jamii, eti kuingia polisi ni bure ila kutoka ni fedha, hii kauli nataka ife kwa sababu nawajua polisi na hawanidanganyi kwa lolote," amesema.
Sheria inasema nini kuhusu dhamana?
Kwa mujibu wa maelezo katika tovuti ya jeshi la polisi Tanzania, dhamana ya polisi inatolewa bure.
"Hakuna malipo yoyote yanayotakiwa kutolewa ili mtuhumiwa au mshtakiwa akubaliwe dhamana," inasema tovuti hiyo.
Jambo la msingi ni mtuhumiwa kuomba apewe dhamana na kutimiza taratibu kwa muijibu wa sheria.
Vigezo vya kuzingatia kabla ya mtuhumiwa kupewa dhamana ya Polisi ni:
Polisi kujiridhisha kwamba mtuhumiwa atatimiza masharti ya dhamana atakayopewa, ikiwa ni pamoja na kufika siku na saa atakayoamriwa.
Hii ni pamoja na:
- historia yake na mshikamano wake na jamii au makazi, ajira na hali ya kifamilia na rekodi yake ya polisi, kama inajulikana, na
- mazingira ambayo kosa lilitendeka, asili na ukubwa wa kosa, uzito wa ushahidi dhidi ya mtu huyo na taarifa nyingine zinazohusiana na uwezekano wake wa kutoroka.
Kujua makazi,ndugu na jamaa, ajira na ikibidi hali ya maisha ya mtuhumiwa na familia yake, kumbukumbu za kihalifu kama zipo.
Umuhimu wa mtuhumiwa kuwa nje kwa dhamana, ili aweze kujiandaa kukabiliana na tuhuma zinazomkabili kabla ya hajafikishwa mahakamani mfano kupata msaada wa kisheria.
Hifadhi ya jamii, kwa maana ya uwezekano wa mtu huyo kuingilia ushahidi kwa kuwatisha mashahidi au kuzuia uchunguzi wa polisi kwa jinsi yoyote ile.
Aidha Mwanasheria Kheri Mbiro anasema kisheria kupewa dhamana ni haki ya kila anayekamatwa kwa makosa yanayodhaminika.
Sheria na haki ya dhamana havina wikiendi hivyo basi kama umekamatwa ndani ya saa 24 na haujapelekwa mahakamani, ni lazima dhamana itolewa uachiwe huru.
"Sheria inachokisema ni mtu akikamatwa inabidi apewe dhamana na sheria haijaeleza kuwa mtu akikamatwa na kuwekwa rumande ijumaa anatakiwa atoke jumatatu hivyo basi polisi kutotoa dhamana kwa kisingizio kuwa ni muda wa mapumziko walikuwa wanakosea kwa sababu, sababu zao hazipo kisheria", Mwanasheria Kheri Mbiro alifafanua .
Kuna sababu za kumnyima mtuhumiwa dhamana?
Kifungu cha 67 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai nchini Tanzania kinaeleza kwamba, mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa Polisi anaweza kukataliwa maombi yake ya kutaka apewe dhamana, Hii ni iwapo polisi watajiridhisha kwamba mtuhumiwa hajatimiza vigezo vilivyoelezwa hapa juu. Aidha, mtuhumiwa anaweza akafutiwa dhamana aliyopewa awali.:
Kufutwa kwa dhamana ya polisi
Baada ya mtuhumiwa kupewa dhamana ya Polisi na kuwa huru dhamana hiyo inaweza kufutwa na mkuu wa kituo , chini ya kifungu cha 68 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha uamuzi wakufuta dhamana ni:-
- Kubainika kwamba mtuhumiwa anapanga mipango ya kutoroka
- Kwa makusudi anakiuka au yu karibu kukiuka masharti ya dhamana.
Mtuhumiwa kama huyo hata hivyo atalazimika kupelekwa mbele ya hakimu kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria mapema iwezekanavyo, na haifai kuwa zaidi ya kikao cha kwanza cha mahakama katika sehemu ambayo inawezekana kumpeleka mtu huyo kwa dhumuni hilo.
Anayekosa dhamana ya polisi anaruhusiwa kisheria wakati wowote, kumuomba afisa polisi kumpatia nyenzo kwa ajili ya kufanya maombi ya dhamana kutoka kwa hakimu. Polisi anafaa kufanikisha hilo ndani ya saa ishirini na nne, au katika muda mwingine wa kutosha kadri inavyowezekana baada ya kufanya maombi, na kuhakikisha amempeleka mtuhumiwa mbele ya hakimu.
Mtuhumiwa atakuwa na haki ya kupata dhamana kama:
- Anaahidi kwa maandishi kuhudhuria mbele ya mahakama iliyotajwa katika muda na mahali palipotajwa, au katika muda mwingine na mahali kama atakavyoarifiwa na afisa polisi;
- Anaahidi kwa maandishi kuzingatia masharti yatakayotajwa kuhusiana na mwenendo wake wakati ameachiwa kwa dhamana, masharti yasiyohusiana na utoaji wa dhamana, kuweka fedha au kutaifisha fedha.
- Mtu mwingine anayekubalika na afisa polisi anakiri kwa maandishi, kwamba anamfahamu mtu anayeshitakiwa na anamtambua kuwa ni mtu anayewajibika ambaye anaweza kuhudhuria mahakamani kujibu mashitaka.
- Mtu anayeshitakiwa, au mtu mwingine anayekubalika kwa afisa polisi, anaingia kwenye makubaliano, akiwa na dhamana au bila dhamana, kutaifishwa kiasi cha fedha iliyotajwa iwapo mtu aliyeshitakiwa atashindwa kuhudhuria mahakamani kujibu mashitaka; au
- Mtu anayeshitakiwa, au mtu mwingine anayekubalika kwa afisa polisi, anaweka kwa afisa polisi, kiasi fulani cha fedha kilichotajwa kitakachotaifishwa iwapo mtu aliyeshitakiwa atashindwa kuhudhuria mahakamani kujibu mashtaka.
Adhabu ya kukiuka dhamana
Dhamana inayotolewa na Polisi kwa mtuhumiwa anayekabiliwa na kosa la jinai inapaswa kuheshimiwa. Kifungu cha 69 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kinatoa adhabu kali kwa mtuhumiwa na mdhamini au wadhamini wanapokiuka masharti ya dhamana waliopewa.















