Raia wa Zimbabwe walivyokwama uwanja wa ndege miezi mitatu Thailand

Wazibabwe walioishi katika uwanja wa ndege kwa miezi mitatu

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wazimbabwe waliokuwa wamekwama huko Bangkok

Umewahi kulalamika kuhusu kulazimishwa kulala kwenye uwanja wa ndege baada ya ndege kuchelewa, au kituo cha mabasi na ukadhani ulikuwa umeteswa sana?

Huenda ukafikiria vingine kwani kuna familia moja kutoka Zimbabwe ambayo ilikwama uwanja wa ndege wa Bangkok kwa miezi mitatu.

Walikuwa hawawezi kutoka uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi.

Familia hiyo ya watoto wanne wenye chini ya miaka 11 na watu wazima wanne hapo mwanzo waliwasili Bangkok mwezi Mei.

Na walipojaribu kuondoka mwezi Oktoba mwaka jana kuelekea Uhispania, hawakuwa na hati ifaayo ya kusafiria.

Na hawakuwa na uwezo, kisheria, wa kuingia tena nchini Thailand kwani walikuwa wamepitisha muda wa hati zao za kuishi kama watalii nchini humo, na walilazimika kulipa faini.

Lakini pia walisema hawangeweza kurudi nyumbani Zimbabwe kwani wangekamatwa na kuadhibiwa na serikali.

Hali ya familia hiyo ilijulikana wazi baada ya mfanyakazi mmoja wa uwanja huo wa ndege kupakia mtandaoni picha yake na mtoto mmoja wa familia hiyo mwezi Desemba akisema alikuwa akiishi katika maeneo ya uwanja wa ndege ''kutokana na shida ambazo hazijatatuliwa'' kinyumbani.

Maafisa wakati huo walieleza kwamba walijaribu kuwasaidia kutafuta mbinu za usafiri kwa shirika la ndege la kimataifa la Ukraine ili wasafiri kupitia Kiev kuelekea Dubai na katika nchi ya tatu kuepuka sheria za uhamiaji barani Ulaya.

Lakini kulingana na msemaji wa Shirika la ndege la Ukraine (UIA) , familia hiyo ilifutilia mbali tiketi zao katika dakika za mwisho kabla ya safari yao, hayo iliyosababisha kurudishwa kwao kutoka Dubai hadi Bangkok.

Familia hiyo iliomba usaidizi kwa Umoja wa Mataifa, wakisema walihofia kuhukumiwa nchini Zimbabwe baada ya hali ya wasiwasi iliyokuwepo mwezi Desemba mwaka jana iliyosababisha kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa miaka mingi Robert Mugabe.

Uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi wa Bangkok

Umoja wa Mataifa ulisema wakati huo kwamba ulikuwa "ukitafuta njia" za kutatua tatizo hilo.

Thailand haina sheria maalum ya kushughulikia wahamiaji na wanaotafuta hifadhi.

Wakati huo wote familia hiyo iliishi katika eneo la watu wanaosafiri huku wakipata ulinzi kutoka kwa wafanyakazi wa shirika hilo la ndege.

Kulingana na msemaji wa afisi ya uhamiaji wa Thai, familia hiyo iliondoka Bangkok siku ya Jumatatu mchana.

Kanali wa Polisi Cherngron Rimphadee aliambia Idhaa ya BBC ya Thai kwamba familia hiyo ilikuwa imeelekea Ufilipino.

Kuna kambi ya wakimbizi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi (UNHCR) huko lakini haijabainika iwapo huko ndio walikoelekea.

Msemaji wa UNHCR aliambia mtandao wa Coconuts kwamba shirika hilo halina uwezo wa kuzungumzia kisa kuhusu watu binafsi.