Mwanamke aliyeongoza kikosi cha wanawake wa IS ahukumiwa kifungo cha miaka 20

Chanzo cha picha, ALEXANDRIA SHERIFF'S OFFICE
Mwanamke wa Kimarekani ambaye alikiri kuongoza kikosi cha wanawake wote wa kundi la Islamic State (IS) amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Allison Fluke-Ekren, mwenye umri wa miaka 42 kutoka Kansas, alifanya vitendo vya kigaidi nchini Iraq, Syria na Libya katika kipindi cha miaka minane.
Pia alikiri kutoa mafunzo ya kijeshi kwa zaidi ya wanawake na wasichana 100, wakiwemo wengine wenye umri wa miaka 10.
Alikiri mashtaka hayo mwezi Juni. Kabla ya hukumu hiyo, waendesha mashtaka walisema hukumu hiyo - kiwango cha juu kinachoruhusiwa kisheria - haitoshi kumuadhibu lakini inapaswa kutolewa bila kujali.
Timu yake ya utetezi ilikuwa imetafuta hukumu fupi isiyojulikana, ikisema kwamba aliumizwa na uzoefu wake alipokuwa Syria iliyokumbwa na vita.
Mwalimu huyo wa zamani alikulia katika jumuiya ndogo ya Overbrook huko Kansas, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, na akawa mwanamgambo mkali ambaye alipanda safu ya IS.
Wakati wanawake wengine wengi walijiunga na IS - ikiwa ni pamoja na baadhi ambao walipigana au kufanya kazi nyingine kwa niaba ya kikundi - Fluke-Ekren ni kesi ya nadra ya mwanamke kuinuliwa kwenye nafasi ya uongozi katika kundi ambalo kitamaduni linatawaliwa na wanaume.
Kulingana na Idara ya Haki na rekodi za umma zilizoonekana na BBC, alihamia Mashariki ya Kati na mume wake wa pili - mwanachama aliyekufa sasa wa kundi la wanamgambo wa Libya Ansar Al-Sharia la IS mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati huo bado alitembelea Kansas mara kwa mara.
Alikuwa na jukumu gani ndani ya IS?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo mwaka wa 2012 au karibu na mwaka huo, alisafirishwa hadi Syria na kuwa mwanachama hai wa IS, akiolewa na wanamgambo wengine kadhaa baada ya mumewe kuuawa vitani.
Waume zake wawili waliofuata, akiwemo mtaalamu wa ndege zisizo na rubani wa Bangladesh, pia waliuawa wakipigania kundi hilo.
Takribani miaka minne baadaye, alikua kiongozi na mratibu wa Khatiba Nusayba, kikosi cha wanawake wote cha IS kilichoanzishwa katika mji mkuu wa kundi hilo wa Raqqa, Syria.
Maafisa wa Marekani wanaamini kuwa kazi yake ya msingi huko ilikuwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanawake hao, ikiwa ni pamoja na matumizi ya AK-47, maguruneti na mikanda ya kujitoa mhanga.
Pia anadaiwa kuwaajiri wahudumu kwa shambulio la kigaidi linaloweza kutokea nchini Marekani.
Katika hati ya hukumu, Msaidizi wa Kwanza wa Mwanasheria wa Marekani Raj Parekh aliandika kwamba Fluke-Ekren "aliwapa aliwafundisha wasichana wadogo kuua". "Alichonga njia ya ugaidi, akiwatumbukiza watoto wake mwenyewe katika kina kirefu cha ukatili kwa kuwanyanyasa kimwili, kisaikolojia, kihisia na kingono," aliongeza.
Watoto wake wawili kati ya 12 pia wamedai katika barua kwa mahakama kwamba aliwanyanyasa kingono.
Wakati akikiri jukumu lake katika IS, mawakili wa Fluke-Ekren walisema "anakanusha vikali madai" ya unyanyasaji.
Idadi kamili ya raia wa Marekani waliojiunga na IS bado haijafahamika, lakini utafiti kutoka Chuo Kikuu cha George Washington unaonesha kuwa takriban 300 walisafiri au walijaribu kusafiri hadi Syria au Iraq kufanya hivyo.
Mwishoni mwa mwaka 2020, mamlaka ya Marekani ilitangaza kuwa 27 walikuwa wamerudishwa makwao, ikiwa ni pamoja na 10 kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi.
Pamoja na jukumu aliloshukiwa kuwa nalo nchini Syria, Bi Fluke-Ekren pia alishtakiwa kupanga mipango ya kushambulia vyuo nchini Marekani.
Pia alidaiwa kuwaambia mashahidi wake kuhusu nia yake ya kufanya shambulio kwenye duka kubwa kwa kutumia vilipuzi, na aliripotiwa kusema kuwa itakuwa ni kupoteza raslimali iwapo halitawauwa watu wengi.















