Kwanini uwezo wetu wa kunusa unatofautiana?

fg

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Thomas Germain
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Huenda uwezo wako wa kunusa unahusiana sana na wewe ni nani na unatoka wapi.

Casey Trimmer, mwanasayansi na mtafiti kuhusu mfumo wa kunusa kutoka kampuni ya bioteknolojia, iitwayo DSM-Firmenich, yenye makao yake nchini Switzerland, anasema:

"Mambo kama umri, jinsia, na ukoo pia yanaweza kuathiri jinsi tunavyonusa harufu fulani, pamoja na tofauti za kitamaduni na uzoefu."

Kuna utafiti ambao unaonyesha tofauti za kushangaza katika uwezo wa kunusa kati ya watu tofauti, ndani jamii moja na katika jamii tofauti.

Uwezo wa kunusa

fd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vinasaba, utamaduni, uzoefu na mazingira, vyote vinaweza kuwa na athari kubwa kwenye hisia yako ya kunusa

Kuna ukweli kwamba wanawake wana hisia kali zaidi ya kunusa kuliko wanaume, tafiti zinaunga mkono hilo. Hata hivyo, kuna ushahidi mdogo wa kuunga mkono wazo maarufu kwamba mimba huongeza hisia za kunusa. Lakini tofauti za kijinsia sio jambo pekee linatofautisha uwezo wa kunusa.

Wapo baadhi ya watu ambao kiasili kupitia jeni wanaweza kunusa harufu zaidi kuliko wengine. Kwa mantiki hiyo hiyo, tofauti za kijeni huwafanya baadhi ya watu kutokuwa na uwezo wa kunusa vizuri na wengine kunusa vizuri.

"Tuna mkusanyo wa zaidi ya vipokea harufu 400 tofauti katika pua zetu, lakini sio kila mtu ana mkusanyiko sawa wa vipokea harufu," anasema Julien Wen Hsieh, daktari na mtaalamu wa harufu na magonjwa ya pua katika Hospitali za Chuo Kikuu cha Geneva nchini Switzerland.

Anasema, “na hilo ndilo hueleza kwa sehemu kubwa kwa nini kuna tofauti juu ya uwezo wa kunusa harufu miongoni mwa watu."

Uwezo wetu wa kutambua harufu na harufu hizo zikawa ni kali au za kupendeza - hilo hutegemea jinsi vigunduzi hivyo vinavyofanya kazi katika pua zetu. Tunapata harufu nzuri kama ya maua pale kemikali iitwayo beta-ionone ya ua hilo inapokutana na kinasa harufu kinachojulikana kama OR5A1.

Lakini karibu nusu ya watu, kinasa harufu hicho hakifanyi kazi. Mtu wa ina hiyo hataweza kamwe kunusa kemikali ya beta-ionone, haijalishi ni kiasi gani cha maua yako kwenye bakuli mbele yake.

Utamaduni na mazingira

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika utafiti mmoja, wanafunzi wanaopitia mafunzo ya kunusa mvinyo, uwezo wao wa kunusa ulikuwa mkubwa
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jeni sio sababu pekee. Kwa baadhi uwezo wao wa kunusa hutegemea mafunzo. Wataalamu wa mvinyo wako bora zaidi katika kutofautisha harufu tofauti kuliko mtu wa kawaida ambaye hawajafunzwa.

Uchunguzi uligundua kuwa mishipa yao ya kunusa ni mikubwa zaidi na hivyo kuongeza uwezo wao wa kunusa. Utafiti huo ulichukua mwaka mmoja na nusu kwa wanafunzi waliokuwa wakifunzwa utaalamu wa kunusa mvinyo.

Watu wa Jahai, jamii ya wenyeji kutoka peninsula ya Malay, wana orodha ndefu ya maneno ya harufu. Hivyo watu wa Jahai wako vizuri zaidi katika kutambua harufu kuliko watu wengine. Watafiti wanaamini, kuwa na maneno ya kuelezea harufu huongeza uwezo wetu wa kunusa.

Kuna sababu zingine ambazo tamaduni zinaweza kuwa na mchango katika kunusa. Utafiti wa 2014 ulilinganisha jamii tatu; wakazi wa Visiwa vya Cook, Wazungu, na Watsimané ambao ni wenyeji kutoka msitu wa mvua wa Bolivia.

Wakazi wa Visiwa vya Cook walikuwa na uwezo mzuri zaidi wa kunusa kuliko Tsimané, lakini vikundi vyote viwili vilikuwa bora zaidi katika kunusa kuliko Wazungu.

Hapo awali, watafiti walidhani kuishi maisha ya ardhini na msituni huboresha hisia zako za kunusa. Utafiti huu ulipinga wazo hilo. Wakazi wa Visiwa vya Cook walikuwa ni wanusaji bora zaidi, licha ya kuwa visiwa hivyo vimeendelea, hata katika viwanda kama nchi yoyote barani Ulaya, na Watsimané wanaishi kwa kujikimu kwa kilimo na kuwinda.

Lakini watafiti walisema uchafuzi wa hewa unaweza kuharibu kwa kiasi kikubwa hisia zako za kunusa. Na wanaona kuwa Visiwa vya Cook viko katika eneo la Pasifiki, mojawapo ya maeneo yaliyo na uchafuzi mdogo zaidi duniani, wakati ubora wa hewa wa msitu wa mvua wa Bolivia ni bora zaidi kuliko wa Ulaya. Viwango vya uchafuzi wa hewa viliendana na mpangilio wa uwezo wa kunusa.

Tafiti zaidi zinahitajika

edf

Chanzo cha picha, Getty Images

Hakuna jibu rahisi kwa nini baadhi ya watu hunusa bora kuliko wengine. Uwezo wa kunusa harufu unaweza kutofautiana hata miongoni mwa watu wanaoishi sehemu moja.

Utafiti wa 2012 ambao uliangalia watu 391 kutoka New York, Marekani, ulipata tofauti za kushangaza katika kunusa. Waasia katika utafiti walikuwa na uwezo bora zaidi wa kunusa kuliko Wazungu, na vikundi vyote viwili vilikuwa na uwezo wa kunusa zaidi kuliko Wamarekani weusi. Tofauti hizi zilikuwa vivyo hivyo hata kwa kuzingatia jinsia, umri, tabia za kuvuta sigara na aina ya mwili.

Tofauti hizi husababishwa na nini? Inaweza kuwa jeni, utamaduni au, ubora wa hewa kwa mtu mmoja mmoja katika mazingira yake.

Nchi na tamaduni zinaonyesha tofauti kubwa katika uwezo wa kunusa harufu fulani. Ndio maana tafiti zaidi, zinahitajika.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah