'Nimezaliwa bila uwezo wa kunusa harufu, sijui chakula kina ladha gani?'

Chanzo cha picha, NAPPY
Inawezekana kuwa kila mtu ana harufu ambayo anavutiwa nayo, inaweza kuwa inamkumbusha mtu fulani au kumbukumbuku fulani au kutambua kuwa kuna chakula kizuri kinaandaliwa.
Sio kitu cha kawaida kwa watu wengi, ni asilimia 5 tu ya watu wanapatwa na hali hii.
Lakini kushindwa kunusa kunaweza kuwa na athari mbalimbali, athari za kihisia na kuonekana katika maisha ya mtu hii ni kwa mujibu wa tafiti mpya kutoka chuo kikuu cha Anglia mashariki.

Chanzo cha picha, Gabriella
Gabriella Sanders hajawahi kusikia harufu yoyote maishani mwake, na inaathiri sio tu pua yake.
''hata sijui chakula kina ladha gani, siwezi kuonja vitu vya moto au vitamu ama vyenye viungo. Gabriela 21 ameimbia Radio One.
''Sijawahi kusikia harufu ya aina yoyote, ni ajabu kwasababu hakuna mtu yoyote kwenye familia yetu ambayo amewahi kupata hali hii, ni mimi na dada yangu tu, inawekana labda ikawa ni wa kurithi''
Unawezaje kutambua kuwa husikii harufu?
Gabriella anakumbuka kuwa akihisi kama kutengwa katika kazi moja ya shule wakati yupo mdogo.
''ilikua ni kuhusu harufu, na kila mtu alikua akieleza kuwa anasikia harufu fulani.
''Hapo ndipo nilipogundua kuwa kumbe sisikii harufu yoyote, kila mtu alikua akitoa mfano wa harufu lakini mimi sikua nao''.

Chanzo cha picha, Gabriella
Imesababisha Gabriella kukutana na matukio mbalimbali utotoni mwake ambayo hakutarajia.
''Nilikua muoga sana wa moto, na nikawa na uoga kuwa inawezekana nyumba ikaungua lakini nisisikie harufu yake''
''Ilinisumbua sana wakati wa utoto lakini nimeshapitia hayo kwa sasa''
Athari za hali hii
Gabriella amekua na wasiwasi mkubwa hasa wa kutosikia harufu ya moshi au gesi,
''nakumbuka siku moja nilikua napika nyumbani, na mama akarudi nyumbani na kusema kuwa, nyumba yote inanukia Gesi, nilipata wasiwasi sana.
''Vitu kama hivyo nimekua huku nikiogopa sana, sasa nimekua na nachukua tahadhari sana''
Sio tu harufu kutoka maeneo ya nje, bali hata usafi wa mwili , utafiti uliofanyika na Falme za kiarabu umeonesha kuwa usafi binafsi ndio umekua aibu kubwa kwa walengwa kwasababu wamekua wakishindwa kujinusa wenyewe.
Lakini binti Gabriella amepata suluhisho.

Chanzo cha picha, Gabriella
"Wazazi wangu na mimi tumetengeneza jinsi ya kuwasiliana''
''Sasa kama nikija nyumbani na rafiki zangu, na nikawa na harufu mbaya, wataniambia kwa ishara kisha naenda kuoga haraka''
Gabriella kwasasa ni mcheza dansi.
''Kwa upande wa marashi ya kunukia , sijawahi kabisa kumiliki vitu hivyo, vitu kama maua, sijawahi kabisa kuvutiwa navyo''
''Lakini natumia manukato tuu, kwasababu ya kazi ya kucheza kila siku, inanibidi hata kama sipendi hayo mambo''
Unatakiwa kuwa muwazi na hali yako
Inaweza kuwa ni jambo la aibu kidogo, lakini Gabriella anasema kuwa kutoweza kunusa sio suala la aibu.
''Nadhani kuwa muwazi kwa marafiki na watu wa karibu ni suala la muhimu, na kuwaambia watu wawe huru kukueleza kuwa kama unanuka vibaya''
''Nimekua nawajulisha watu ambao wananizunguka kuwa mimi siwezi kusikia harufu, na nawaambia kuwa waniambie kama nanuka mimi sitosikia vibaya''
''Ni bora nijue kuliko kuwakosesha amani watu''
Lakini je Gabriella anatamani kuwa na uwezo wa kusikia harufu?
''sio kitu ambacho nakihitaji kwasababu sitokipata, na sijui napitwa na mambo gani''
''Lakini ningependa kusikia harufu, na kujua ile hali ya kusikia kitu''













