Anosmia: Utafanya nini ukijipata umepoteza uwezo wako wa kuhisi harufu?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Utafanya nini ukiamka siku moja ujipate umepoteza uwezo wako wa kuhisi harufu ya kitu chochote?
Ni harufu gani utakayoikosa zaidi maishani? Pengine huenda kwa mfano ukatamani kusikia harufu ya marashi mazuri yanayo pakwa na mtu unayependa, harufu ya maua katika bustani au harufu ya chakula kitamu.
Hebu sasa tafakari maisha ya mtu ambaye hajawahi kuhisi harufu ya kitu chochote na wala hajui iwapo kina nuka au kunukia tangu alipozaliwa.
Hayo ndio yamekuwa maisha ya Wambui Mwangi, 24 kutoka nchini Kenya ambaye ameishi na tatizo la kutosikia kabisa harufu tangu alipozaliwa.
Wamboi anasema maisha yake yamekuwa ya kubahatisha.
''Ni maisha magumu kwa sababu watu hawakuelewi ukiwaambia huhisi harufu. Tatizo langu kubwa ni uwezo wa kung'amua kama kitu kinanukia vizuri au vibaya.
Mara nyingi mimi huwa na wasi wasi kwa sababu sijui watu watasema nini kuhusu mazingira yangu''
Musa Kipingor, daktari bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT) mjini Nairobi anasema ni nadra sana kumpata mtu akitafuta matibabu ya ugonjwa wa kutosikia kabisa harufu maarufu kama Anosmia.
''Watu hufikiria ni jambo la kawaida kwa hivyo hawatafuti matibabu. Kwa mfano mwaka huu sijapokea kesi yoyote ya tatizo la kutosikia kabisa harufu.''
Bwana Kipingor anasema hakuna takwimu rasmi kuhusiana na hali hiyo lakini wanawake huathiriwa zaidi. ''Si unajua wanawake hupatia umuhimu kila kitu katika maisha yao? Uwezo wa kusikia harufu ya mafuta au marashi anayopaka au chakula anachopika bila shaka itamdhuru''.

Watu wengi wenye tatizo la kutosikia kabisa harufu kama Wamboi, huweza kutambua ladha ya vitu vya chumvi, sukari, vita vichachu na vichungu lakini hushindwa kuelezea harufu ya vitu hivyo.
Daktari Kipingor anasema uwezo wa kutambua tofauti ya ladha, hutegemea harufu, na si vipokezi vya ladha kwenye ulimi.
Watu wenye tatizo la kutosikia harufu, mara nyingi, hulalamika kuhusu kupoteza uwezo wa kutambua ladha.
Kutosikia harufu husababishwa na nini?
Sababu za kawaida kabisa ni pamoja na kuumia kichwa mara kwa mara (hasa watoto) au katika ajali ya gari.
Kuumia kichwa kunaweza kuharibu nyuzi za neva za kuvutia harufu - kuharibika kwa mishipa inayounganisha vipokezi vya harufu na ubongo, ambavyo hupita kwenye paa la tundu la pua.
Wakati mwingine kuumia huko kunajumuisha mpasuko wa mfupa wa cibriform plate ambao hutenganisha ubongo na tundu la pua.
Kuharibika kwa neva za kuvutia harufu pia kwaweza kutokana na maambukizi jirani na mfupa unaotenganisha ubongo na tundu la pua.
Sababu nyingine inayofahamika ni kuambukizwa kwa eneo la juu la kupumulia hewa hasa hasa mtu anapougua mafua.
Mafua yanaweza kuwa sababu ya hata robo ya watu wenye nusu ya tatizo la kutohisi harufu (Hyposmia) au hata wenye tatizo kamili la kushindwa kusikia harufu (Anosmia).
Magonjwa ya uzee na matatizo mengine yanayoleta udhaifu wa ubongo kama vile kukakamaa kwa tishu za mwili (multiple sclerosis) kwaweza kuharibu neva za kunusia harufu, jambo ambalo kwa kawaida husababisha mtu kupoteza harufu.

Chanzo cha picha, Media for Medical
Sababu zinazofahamika kidogo
Kwa mijibu wa wataalamu wa afya dawa pia zinaweza kusababisha tatizo la kushindwa kusikia harufu kwa watu ambao ni wepesi kuathirika.
Maambukizi ndani ya pua kama vile uvimbe, manundu ndani ya pua (polyps, tumors) na maambukizi mengine ndani ya pua, na mizio ya misimu (seasonal allergies) nayo huweza kutatiza uwezo wa kusikia harufu.
Mara nyingi, maambukizi mabaya ya tundu za pua au tiba ya mionzi dhidi ya saratani husababisha kupotea kwa harufu na ladha jambo ambalo hudumu kwa miezi kadhaa na kisha linakwisha au huwa la kudumu moja kwa moja.
Hali hizi huweza kuharibu au kuvuruga vipokezi vya harufu. Mchango wa tumbaku haufahamiki kwa uhakika. Wapo watu wachache wanaozaliwa bila kusikia harufu.
Dalili za kutambua ugnjwa wa Anosmia
Iwapo mtu amepata ajali na kuumia kichwa hivi karibuni.
Dalili za mfumo wa neva kushindwa kufanya kazi, kama vile udhaifu, kutoweza kusimama wima, au matatizo ya kuona, kusema na kumeza.
Dalili zote hizi kujitokeza ghafla.

Chanzo cha picha, ISSOUF SANOGO
Ni wakati gani wa kumuona daktari
Ukijiona na dalili hizi unapaswa kumuona daktari ndani ya siku moja au mbili.
Pia unashauriwa kumuona daktari pale inapowezekana lakini tathmini ya daktari isiwe ya haraka kama dalili nyingine hazijajitokeza.













