Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 13.12.2023

Chanzo cha picha, Getty Images
Mazungumzo yatakayomwezesha kiungo wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi Donny van de Beek, 26, kujiunga na klabu ya Eintracht Frankfurt kwa mkopo yamepiga hatua. (Fabrizio Romano kwenye X)
Barcelona wanatazamia kumnunua kiungo wa Tottenham na timu ya taifa ya Argentina Giovani Lo Celso, 27 kwa mkopo dirisha la uhamisho litakapofunguliwa mweziJanuari . (90min).
Wamiliki wa Newcastle wanavutiwa na Jose Mourinho, huku kandarasi ya kocha huyo wa Roma mwenye umri wa miaka 60 ikitarajiwa kumalizika msimu ujao baada ya tetesi kuibuka kuwa klabu hiyo ya Serie A haina nia ya kusalia naye kama mkufunzi wao. (Gazzetta dello Sport - kwa Kiitaliano)

Chanzo cha picha, Getty Images
Getafe wanatumai kumnunua mshambuliaji wa Uingereza Mason Greenwood, 22, kutoka Manchester United na watafaidika kutokana na kipengele cha mauzo cha 20% ambacho kiliwekwa katika mkataba wake wa mkopo kwa klabu hiyo ya La Liga. (Athletic-Usajili unahitajika)
Arsenal wametoa ofa ya pauni milioni 17.2 pamoja na nyongeza kwa mshambuliaji wa Santos na Brazil wa chini ya umri wa miaka 20 Marcos Leonardo, 20. (Fichajes - kwa Kihispania).
Manchester City wanaweza kumnunua kiungo na mshambuliaji dirisha la uhamisho a wachezaji litakapofunguliwa mwezi Januari. (Football Insider)

Chanzo cha picha, Getty Images
Juventus bado wana nia ya kumsajili kiungo wa Manchester City na Uingereza Kalvin Phillips, 28, kwa mkopo mwezi Januari. (Gazzetta dello Sport - kwa Kiitaliano)
Chelsea wanamtaka mshambuliaji wa Sporting Lisbon na Uswidi Viktor Gyokeres, 25. (Ekrem Konur on X)
Kocha wa zamani wa Wolves na Uhispania Julen Lopetegui, 57, anawaniwa na klabu za Crystal Palace na Nottingham Forest. Mhispania huyo hajafanikiwa kupata kazi tangu aondoke Wolves mwezi Agosti. (Sun)
Beki wa Liverpool Mfaransa Ibrahima Konate, 24, ameanza mazungumzo ya kuongeza mkataba na The Reds, licha ya uvumi unaomhusisha na kuhamia Paris St-Germain. (le10sport - kwa Kifaransa)

Chanzo cha picha, Getty Images
Borussia Dortmund wamejiunga na Newcastle katika kinyang'anyiro cha kuwania saini ya Serhou Guirassy, mshambuliaji wa Stuttgart wa Guinea mwenye umri wa miaka 27. Guirassy tayari amefunga mabao 16 katika Bundesliga msimu huu. (Bild Sports - kwa Kijerumani)
Wasaka vipaji wa Ligi ya Premia kutoka Manchester United, Manchester City, Tottenham na Liverpool wanamfuatilia kiungo wa kati wa Middlesbrough Hayden Hackney, 21, kwa matarajio kwamba ataondoka katika klabu hiyo msimu ujao. (Mail)
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












