'Bado watashinda ligi' - je, 'mgogoro mdogo' wa Man City umekwisha?

Chanzo cha picha, BBC Sport
Mgogoro mdogo wa Manchester City umekwisha, lakini sio kabla ya kupata hofu nyingine.
Msimu wenye changamoto kwa City ulikuwa ukikabiliwa na bahati mbaya wakati wa mapumziko ya mchezo wa Jumapili huko Luton, huku washindi wa mataji matatu mwaka jana wakiwa nyuma kwa bao 1-0 na kutarajia mechi ya tano mfululizo ya Ligi Kuu ya Uingereza bila kushinda.
Mabao mawili ya kipindi cha pili ndani ya dakika tatu kutoka kwa Bernardo Silva na Jack Grealish yaliwaokoa vijana wa Pep Guardiola, hata hivyo, na pambano la City lilitoa jibu kamili kwa yeyote anayetilia shaka sifa zao za kutetea taji jingine.
"Timu ilionyesha sifa yake, lakini hilo halikunishangaza hata kidogo," alisema beki wa zamani wa City Micah Richards, ambaye alitazama ushindi wao wa 2-1 kwenye Kenilworth Road kwa MOTD2.
"Wakati wowote watu wanazungumza vibaya juu yao, inawachochea tu.
"Sitasema Pep amekuwa bila mguso hivi karibuni, lakini ni kama anapokea ukosoaji huo na kwenda 'vizuri, ikiwa ndivyo unavyofikiria, tutakuonyesha', na timu nzima ina mtazamo huo pia.
"Wanaweza wasishinde taji, ingawa ninaamini watashinda, lakini watapambana hadi mwisho. Ikiwa mtu mwingine atawashinda, basi itakuwa karibu sana."
'Kuridhika sio neno sahihi'
Guardiola alimjibu Gary Neville baada ya sare ya wikendi iliyopita na Spurs, wakati mchambuzi wa Sky alipodai kuwa City walikuwa "wameridhika" baada ya kushinda mataji matatu mfululizo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Richards anaelewa kwa nini Pep hakufurahishwa na upande wake kupewa lebo hiyo, na anahisi haikuwa haki.
"Sidhani 'kuridhika' lilikuwa neno sahihi ambalo Gary alikuwa akitafuta," Richards alisema. "Nilitaka kuwa na uhakika, kwa hivyo niliitafuta kwenye kamusi ili kuwa na uhakika juu ya ufafanuzi wake kamili.
"Inamaanisha kuwa mtu wa kujitosheleza na kutojikosoa kwa sababu ya mafanikio hata haujaribu kwa bidii yako, na huyo sio Pep, au upande wa City ninaouona.
"Ninaweza kukosea, lakini sidhani hivyo ndivyo Gary alimaanisha. Nadhani alimaanisha tu kwamba, kwa viwango vyao vya juu, City wanaruhusu timu kurudi kwenye michezo , ambapo kwa kawaida watakuwa wakorofi na kuwamaliza.
"Ukiangalia mechi hizo walizotoka sare, dhidi ya Chelsea, Liverpool na Tottenham, walipata fursa ya kuzimaliza zote tatu - ikiwa, tuseme, Erling Haaland atachukua nafasi yake wakati City wakiwa mbele kwa mabao 2-1 dhidi ya Spurs, tusingeweza kuwa na mazungumzo haya.
"Hiyo haitokani na ukosefu wa hamu, ingawa, au timu kupunguza kazi yao. Sio hivyo."
Badala yake, Richards anahisi City wamekosa baadhi ya wachezaji wao wa kawaida wa kubadilisha mchezo, huku wapya waliowasili kama Mateo Kovacic na Matheus Nunes hawawezi kuleta matokeo sawa na ya wenzao katika mechi zenye ushindani.
"Watu wanafaa kukumbuka kuwa Kevin de Bruyne amekuwa nje tangu msimu huu uanze, na City ilipoteza Ilkay Gundogan na Riyad Mahrez msimu wa joto," aliongeza.
"Kitu nilichopenda kuhusu Mahrez ni kwamba hata kama hachezi vizuri, mara zote angemaliza mechi na kuwafanya City kuwa juu ya mstari katika nyakati muhimu.
"Gundogan na De Bruyne ni wazi walifanya hivyo sana pia, pamoja na kuwa sehemu muhimu ya jinsi City wanavyocheza. Bila shaka wanawakosa wote watatu kwenye safu ya kiungo.
"Nilidhani Kovacic alicheza vyema dhidi ya Luton lakini imekuwa vigumu kwake kuingia na kuzoea mfumo wa City, na ni vivyo hivyo kwa Nunes pia.
"Wamezoea kucheza kwa njia fulani lakini sasa wana wachezaji wa kati wanaoingia kwenye nafasi yao ya kiungo, na mabeki wa pembeni pia.
"Josko Gvardiol pia amepata ugumu, kwa sababu ni mmoja wa wachezaji wa kati wachanga bora zaidi duniani, lakini Guardiola anataka kumtumia katika nafasi ya beki wa kushoto. Sio kana kwamba anamtaka aingilie kati, pia" kwa sababu alikuwa akiruka mbele wakati wote dhidi ya Luton.
"Huyo ni Pep kwako - anaweka mfumo wa City mbele ya mchezaji yeyote - lakini najua mwenyewe kwamba kuuliza kiungo wa kati kwenda kwenye eneo la beki wa pembeni sio rahisi kujiondoa.
"Umbali unaoweka kwa wachezaji wa timu pinzani ni tofauti sana na unapokuwa katikati, na ni rahisi kufichuliwa katika hali moja moja kwa upana.
"Gvardiol ni mlinzi bora lakini hataki kuwa nje, akisimamisha krosi na hayo yote. Kama alivyopata dhidi ya Luton, inachukua kosa moja dogo tu kuongoza kwa bao."
Shida katika mpito pia

Chanzo cha picha, BBC Sport
City walikuwa na pointi moja kileleni mwa jedwali baada ya kuwalaza Bournemouth 6-1 mnamo Novemba 4, kabla ya sare tatu mfululizo na kushindwa Jumatano na Aston Villa uliwafanya kupoteza mwelekeo kwa wapinzani wao wa ubingwa.
Lakini Richards hafikirii uchezaji wao ulishuka sana wakati wa mbio hizo bila kushinda, na badala yake anadai kuwa hawajakuwa katika kiwango bora zaidi cha kujilinda msimu wote.
"Kumekuwa na mazungumzo makubwa kuhusu nini kimekuwa kibaya kwa City hivi karibuni, lakini kwa kweli hawajacheza vibaya hivyo katika wiki chache zilizopita," alielezea.
"Kinachonihusu, kwa sababu ninaitazama City kila wakati, ndivyo wanavyokuwa kwenye mabadiliko, wanapopoteza mpira - na sio katika mechi chache zilizopita pia.
"Wanaonekana kuwa hatarini zaidi msimu huu, na hiyo ndiyo wasiwasi kwangu. Ninawahisi mabeki kwa sababu mara tu wapinzani wanapomshinda Rodri, mara nyingi huwa watatu dhidi ya wawili, au wanne kwa watatu nyuma.
"Kwa kawaida wangeshughulikia hilo, kwa hivyo singesema ni ujinga, lakini City imekuwa ikiruhusu mabao mengi zaidi msimu huu.
"Nadhani kumpoteza John Stones, ambaye ameanza mechi nne pekee kati ya 16 za ligi kwa sababu ya majeraha, imekuwa pigo kubwa.
"Sio tu kwa upande wake kama mchezaji anayeweza kutumia mpira, lakini pia nje ya uwanja. Ni mtulivu katika hali kama hizo na pia ni mzuri katika kushinda mpira katikati ya uwanja. Inaleta mabadiliko makubwa kumrudisha katika timu."
Haaland hayupo, lakini Foden anaweza kustawi

Chanzo cha picha, BBC Sport
Wasiwasi wa hivi punde wa jeraha la City ni Haaland ambaye alikosa mechi ya Jumapili kutokana na jeraha la mguu, huku Guardiola akiwa hana uhakika ni lini hasa atakuwa sawa kurejea.
Ilikuwa ni mechi ya kwanza ya maana ya ligi ambayo mshambuliaji huyo mahiri wa Norway alikosa tangu Aprili 1, wakati City ilipoilaza Liverpool 4-1, lakini Richards anahisi uchezaji wao dhidi ya Luton unaonyesha bado wanaweza kumudu wakati hayupo.
"Ikiwa Haaland yuko nje kwa muda mrefu, basi sitakuwa na wasiwasi," Richards aliongeza. "Bado nina na matumaini kuhusu City, na napenda wanachofanya.
"Dhidi ya Luton, walibadilisha sura zao na kumruhusu Phil Foden kucheza katika nafasi ya 10. Ukiwa naye katikati, kila wakati utaunda kitu."
Je, itakuwa 'wakati wa sherehe' tena?
City wako pointi nne nyuma ya vinara Liverpool lakini kwa kweli wako karibu zaidi na kilele kuliko ilivyokuwa msimu uliopita, walipokuwa nyuma kwa pointi saba na Arsenal baada ya mechi 16, na bado waliishia kutwaa ubingwa wakiwa wamebakisha mechi tatu.
"Liverpool wameondokana nayo wiki hii, na washindi wawili waliochelewa," Richards aliongeza.
"Hakuna anayejua ni aina gani ya uchezaji utakaopata kutoka kwao kwa sasa, lakini kwenda mbele daima wanaonekana kama watazalisha wakati Mohamed Salah yuko kwenye timu.
"Ni sawa na Arsenal, ambao hawajakuwa katika kiwango bora kama msimu uliopita, lakini bado wamekuwa wakivuka mstari muda mwingi.
"Vilabu vyangu vingine vya zamani, Aston Villa, vimekuwa na wiki nzuri na siwezi kusema vya kutosha juu ya kazi ambayo Unai Emery ameifanya, lakini itakuwa ngumu sana kwao kuendeleza hilo kwa muda mrefu. .
"Ninawatazama na nadhani ni timu bora, lakini ikiwa watampoteza Ollie Watkins au John McGinn kutokana na jeraha basi timu yao ingekuwa tofauti kabisa.
"Tayari tumeona hilo likitokea kwa Tottenham, walipompoteza James Maddison na wachezaji wao wawili waliokuwa chaguo la kwanza la kati, ingawa Cristian Romero amerejea sasa baada ya kusimamishwa.
"Hiyo ndiyo tofauti kubwa kati ya timu hizo na City, ambao wanaweza kubadilisha wachezaji bila kuwaathiri sana.
“Inafurahisha kuwa na timu chache kwenye kinyang’anyiro hicho lakini bado naamini City wako kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa ligi, kutokana na ubora walionao kwenye kikosi chao.
"Nadhani watu husahau kwamba mara nyingi huwa na aina hii ya uchawi wakati huu wa mwaka, ambapo timu hupoteza pointi - lakini ikija mwisho wa msimu huwa ni wakati wa sherehe tena!"
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












