Tuzo za Caf 2023: Je, Victor Osimhen anaweza kuwa jina kubwa kukosa tuzo?
Na Isaya Akinremi na Emmanuel Akindubuwa
BBC Sport Africa, Lagos

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambulizi wa Nigeria, Victor Osimhen anachukuliwa kuwa mstari wa mbele kutangazwa Mwanasoka Bora wa Afrika wa Mwaka Jumatatu, lakini mchezaji huyo wa Napoli anakabiliwa na ushindani kutoka kwa mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah na mlinzi wa Paris St-Germain Achraf Hakimi.
Nahodha wa Misri, Salah alishinda tuzo ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mwaka 2017 na 2018 - na alishika nafasi ya pili kwa Sadio Mane 2019 na 2022 - wakati beki wa kulia Hakimi alikuwa na jukumu muhimu katika kampeini ya kihistoria ya Morocco hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia la Fifa 2022.
Hata hivyo Osimhen alikuwa mchezaji wa daraja la juu zaidi wa Kiafrika katika kura ya Ballon d'Or kwa upande wa Wanaume 2023, akimaliza wa nane baada ya kufunga mabao 26 msimu uliopita na kuisaidia Napoli kutwaa taji lao la kwanza la Serie A ndani ya miaka 33.
Lakini, iwapo atapuuzwa, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 atajiunga na orodha ndefu ya wachezaji mashuhuri ambao walishindwa kushinda tuzo kubwa zaidi ya mtu binafsi barani.
BBC Sport Africa inawataja baadhi ya majina makubwa kutoka barani kote waliokosa tuzo ya Caf.
Jay-Jay Okocha (Nigeria)
Akichukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya mchezo huo, kiungo wa kati wa Super Eagles Okocha alifanikiwa kuorodheshwa kwenye orodha ya walioteuliwa na Caf mara tatu.
Alikuwa sehemu kuu ya 'kizazi cha dhahabu' cha Nigeria ambacho kilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1994 na medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki ya 1996, na kuzishinda Brazil na Argentina njiani.
Wakati mzuri zaidi wa Okocha ulikuwa kwenye Kombe la Dunia la 1998 nchini Ufaransa, akishangaza wengi na ustadi wake wa kucheza wakati Nigeria ikitoka katika hatua ya 16 bora, lakini alikosa kumpiku Mustapha Hadji wa Morocco kwenye tuzo za Caf mwaka huo kwa pointi mbili pekee.
Alitajwa tena kwenye orodha ya walioteuliwa mwaka wa 2003 na 2004 lakini alimaliza wa tatu mara zote mbili, huku Mcameroon Samuel Eto'o akipata tuzo licha ya Okocha kumaliza kama mfungaji bora wa pamoja na mchezaji bora wa shindano kwenye Afcon ya 2004.Wakati huo huo, kiungo wa zamani wa Chelsea John Obi Mikel alishika nafasi ya pili mwaka wa 2013 huku mshambuliaji wa zamani wa Everton Daniel Amokachi akimaliza jukwaani mwaka wa 1995 na 1996.
Michael Essien (Ghana)

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiungo mwingine mahiri kutoka Afrika Magharibi, Essien alikuwa mpambanaji katikati ya uwanja na alikuwa na ustadi wa kufunga mabao ya kuvutia ya umbali mrefu.
Essien alishinda mataji ya Ufaransa mfululizo akiwa na Lyon na alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligue 1 mwaka wa 2005 kabla ya kujiunga na Chelsea kwa ada iliyorekodi Afrika wakati huo ya pauni milioni 24.4.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana alikuwa mtu muhimu kwa The Blues kwa takriban muongo mmoja huko Stamford Bridge, na kuisaidia klabu hiyo ya London Magharibi kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu, manne ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa mwaka 2012.
Aliteuliwa kuwania tuzo za Caf kila mwaka kutoka 2005 hadi 2009, na alimaliza wa pili nyuma ya mshambuliaji wa Mali Frederic Kanoute mnamo 2007.
Mfungaji bora wa muda wote wa Ghana, Asamoah Gyan ni jina lingine maarufu la kukosa nafasi, akimaliza nyuma ya Eto'o mwaka 2010, huku beki wa kati wa Bayern Munich na Black Stars Samuel Kuffour akishika nafasi ya pili mwaka wa 1999 na 2001.
Mohamed Aboutrika (Misri)
Misri ilikuwa na nguvu isiyozuilika katika soka ya Afrika kati ya 2006 na 2010, ikinyanyua mataji matatu mfululizo ya Afcon na mtu mmoja katika moyo wa upande huo wa Mafarao walioshinda wote alikuwa ni Aboutrika.
Kiungo mshambuliaji mwenye jicho la kulenga lango, alikuwa na uwezo mkubwa kwa nchi yake na kwa klabu ya Al Ahly, ambapo alishinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na manne ya Caf Super Cup.
Aboutrika alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa CAF mara nne, alichaguliwa katika timu ya mwaka ya Caf mara nne na alichaguliwa katika Afcon Dream Team mara mbili.
Tamaa yake ya kutoondoka katika nchi yake kwa ajili ya kazi kwingine inaweza kuwa imeathiri nafasi yake ya kushinda tuzo kuu ya Caf, na nafasi ya karibu zaidi aliyoipata ni kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Emmanuel Adebayor mwaka wa 2008.
Mshambulizi wa Misri Hossam Hassan pia alikosa nafasi katika kipindi cha miongo miwili ya maisha yake ambayo ilimfanya kushinda mataji matatu ya Afcon na kumaliza kama mfungaji bora katika mashindano ya 1998.
Benni McCarthy (Afrika Kusini)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mfungaji bora wa pamoja kwenye Afcon ya 1998 akiwa na mabao saba (pamoja na Hassan) na mshindi wa Ligi ya Mabingwa akiwa na Porto mwaka 2004, McCarthy alikuwa mmoja wa washambuliaji hodari wa Kiafrika wa kizazi chake.
Ushirikiano wake na Shaun Bartlett ulifanya Bafana Bafana kuwa moja ya timu bora za bara na alishiriki katika Kombe la Dunia mnamo 1998 na 2002.
Hata hivyo, McCarthy alikosa kuchaguliwa katika vikosi vya Afrika Kusini vilivyoshinda Afcon 1996 katika ardhi ya nyumbani na kuandaa Kombe la Dunia la 2010.
Licha ya maisha yake ya soka nchini Uholanzi na Ureno, McCarthy hakuwahi kuingia kwenye orodha ya walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ya Caf.
Kwingineko kusini mwa Afrika, Christopher Katongo alipuuzwa mwaka wa 2012 baada ya kuwa nahodha wa Zambia kwa ushindi wa kushangaza wa Afcon - lakini fowadi huyo anaweza kujifariji kwa kuchaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika wa BBC wa Mwaka 2012, akishinda kwa zaidi ya 40% ya kura za umma.
Seydou Keita (Mali)
Kiungo huyo alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Pep Guardiola cha Barcelona ambacho kilishinda mataji matatu mfululizo ya La Liga kati ya 2009 na 2011, akiwa raia wa kwanza wa Mali kuiwakilisha klabu hiyo ya Catalan baada ya kujiunga nayo kutoka Sevilla mwaka 2008.
Alishinda Ligi ya Mabingwa, Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Barca mnamo 2009 na 2011, na pia alijumuishwa katika timu bora ya mwaka ya Caf kufuatia ushindi huo.
Keita alitajwa katika nafasi ya pili nyuma ya Yaya Toure kwa tuzo ya 2011, na aliendelea kuisaidia Mali kumaliza nafasi ya tatu katika matoleo ya Afcon 2012 na 2013.
Kalidou Koulibaly ni Mwafrika mwingine wa Magharibi ambaye amekosa tuzo ya mtu binafsi, ambayo haikutolewa mnamo 2020 au 2021 kwa sababu ya janga la corona.
Sasa akiwa na Al-Hilal ya Saudi Pro League, beki huyo wa kati alikuwa nahodha wa Senegal kutwaa ubingwa wa Afcon mwaka jana lakini aliwaona wachezaji wenzake wa Simba ya Teranga, Mane na Edouard Mendy wakiwa jukwaani na Salah badala yake.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












