Victor Osimhen ashinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Victor Osimhen wa Nigeria ametawazwa Mwanasoka Bora wa Afrika 2023 katika hafla ya utoaji wa tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mjini Marrakesh.
Mchezaji huyo wa Napoli aliwashinda Mmisri, Mohamed Salah na Achraf Hakimi wa Morocco katika tuzo hiyo ya kifahari - hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mnigeria kutwaa taji hilo tangu Nwankwo Kanu mwaka 1999.
Nigeria ilifurahia mafanikio maradufu huku Asisat Oshoala akihifadhi tuzo ya upande wa wanawake - ikiwa ni mara ya sita kwa nyota huyo wa Barcelona kushinda tuzo hiyo.
Washindi hupigiwa kura na jopo linalojumuisha kamati ya ufundi ya Caf pamoja na wanahabari wa Afrika, makocha wakuu na manahodha. Vilabu vinavyoshiriki katika hatua ya makundi ya mashindano ya bara Afrika pia vina usemi kuhusu mshindi wa tuzo hiyo.
Ushindi wa Osimhen
Osimhen wa Napoli, 24, alipendekezwa kutwaa tuzo ya kifahari ya Caf kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka baada ya msimu mzuri wa 2022-23.
Alifunga mara 26 katika mechi 32, likiwemo bao muhimu lililoifungia Scudetto mwezi Mei na kushinda Napoli taji lao la kwanza la Serie A katika kipindi cha miaka 33.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Wolfsburg na Lille pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji Soka wa Italia mapema mwezi huu baada ya kuwa na msimu mzuri.
Osimhen mzaliwa wa Lagos alifunga mabao matano katika mechi nne za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchi yake ilipotinga fainali mwaka ujao.
Pia alikuwa Mnigeria wa kwanza kumaliza katika 10 bora ya kura ya Ballon d'Or na kumaliza katika nafasi ya nane na akafanywa kuwa Mwanachama wa Jamhuri ya Shirikisho katika nchi yake.

Chanzo cha picha, Reuters
Nyota wa Barcelona Asisat Oshoala, 29, aliufanya usiku wa kukumbukwa kwa Nigeria, kwa kushinda taji la Mchezaji Bora wa Mwaka kwa Wanawake kwa mara ya sita na kuzidisha rekodi.
Oshoala - ambaye alienda kwenye Kombe la Dunia nchini Australia na New Zealand mwaka huu - anahifadhi kombe aliloshinda mwaka jana.
Alifauku kukabiliana na ushindani kutoka Muafrika Kusini Thembi Kgatlana wa Racing Louisville na Mzambia Barbra Banda wa Shanghai Sengli.
Kutambuliwa kwa Kombe la Dunia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Desiree Ellis wa Afrika Kusini ametwaa tuzo yake ya nne ya Kocha Bora wa Mwaka wa Caf baada ya kuiongoza Banyana Banyana kwenye Kombe lao la kwanza la Dunia.
Tuzo ya wanaume imekwenda kwa Walid Regragui wa Morocco usiku wa kuamkia leo kwa Atlas Lions, ambao waliteuliwa kuwa Timu ya Taifa ya Wanaume ya Mwaka.
Ushujaa wao wakiwa Qatar 2022 - ambapo walikuwa timu ya kwanza ya Kiafrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia - pia walimsaidia Yassine Bounou kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka wa Wanaume.
Super Falcons ya Nigeria imeshinda Timu ya Taifa ya Mwaka ya Wanawake huku nyota wao wa Paris FC Chiamaka Nnadozie akitwaa tuzo ya golikipa bora wa wanawake.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilitawazwa Klabu Bora ya Mwaka ya Wanawake baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili.
Miamba wa Misri, Al Ahly, ambao walishinda taji la 11 la Ligi ya Mabingwa mwaka 2023, walishinda tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka ya Wanaume.
Katika usiku huo jijini Marrakesh, Caf pia ilifichua ni nani wachezaji wa Afrika waliwapiga kura katika safu ya XI Bora kwa wanaume na wanawake na Rais wa Senegal Macky Sall alichukua tuzo ya mafanikio maalum.
Washindi wa tuzo za Caf 2023:
Mchezaji Bora wa Mwaka (wanaume): Victor Osimhen (Napoli & Nigeria)
Mchezaji Bora wa Mwaka (wanawake): Asisat Oshoala (Barcelona & Nigeria)
Kocha Bora wa Mwaka (wanaume): Walid Regragui (Morocco)
Kocha Bora wa Mwaka (wanawake): Desiree Ellis (Afrika Kusini)
Timu ya Taifa ya Mwaka (wanaume): Morocco
Timu ya Taifa ya Mwaka (wanawake): Nigeria
Kipa Bora wa Mwaka (wanaume): Yassine Bounou (Al Hilal & Morocco)
Kipa Bora wa Mwaka (wanawake): Chiamaka Nnadozie (Paris FC & Nigeria)
Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka (wanawake): Nesryne El Chad (Lille & Morocco)
Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka (wanaume): Lamine Camara (Metz & Senegal)
Klabu Bora ya Mwaka (wanawake): Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
Klabu Bora ya Mwaka (wanaume): Al Ahly (Misri)
Mchezaji Bora wa Mwaka wa Interclub (wanawake): Fatima Tagnaout (AS FAR & Morocco)
Mchezaji Bora wa Mwaka wa Klabu (Wanaume): Percy Tau (Al Ahly & Afrika Kusini)
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa Ambia Hirsi












