Estonia: Utamaduni wa kusafisha mwili na roho kupitia sauna

Chanzo cha picha, T Tuul
- Author, Hillary Millán
- Nafasi, BBC
Ni alasiri yenye jua - mwezi wa Machi huko Estonia lakini niko kwenye sauna ya moshi, nimelala kwenye benchi, nikiwa uchi kabisa.
Miguu yangu imeekwa juu ya boriti na kichwa changu juu ya matawi ya mti. Ni kitawi cha miti kinachokusudiwa kupura mwili wangu ili kupunguza seli zilizokufa katika ngozi na kuongeza mzunguko wa damu.
Majani yaliyokaushwa ni laini, baada ya kulowekwa ndani ya maji. Harufu ya majani na moshi vimejaa puani mwangu. Kuna unyevunyevu, na michirizi ya jasho imefunika mwili wangu.
Eda Veeroja, mmiliki wa sauna ya Mooska Smoke. Anaweka maji kwenye mawe ya moto
Anaimba huku mvuke ukipanda kutoka kwenye mawe.
Veeroja ametumia saa nane kuandaa sauna hii. Chumba cha mvuke kimejaa moshi, hewa moto inapanda hadi kwenye dari. Mara tu halijoto ilipopanda zaidi ya 80C, alifungua sehemu ndogo kwenye dari, kuruhusu hewa kwenye sauna kwa saa mbili kabla hatujaingia.
Historia ya Sauna

Chanzo cha picha, Veeroja
Tamaduni za sauna za moshi za Estonia ziko kwenye orodha ya Turathi za Utamaduni za Unesco. Sauna zimekuwepo kaskazini mwa Ulaya kwa maelfu ya miaka.
Uchimbaji wa ardhi katika miaka ya 1980 kaskazini mwa Estonia ulitoa kile kinachoonekana kuwa ushahidi wa kwanza wa kiakiolojia wa sauna iliyojengwa kati ya Karne ya 12 na 13.
Kufuatia mwisho wa kukaliwa Estonia na Muungano wa Sovieti mwaka 1991, Veeroja aligundua kuwa utamaduni wa sauna ulikuwa umebadilika kwa sababu ya kuongezeka kwa miji na ujio wa hita za umeme.
Lakini aliona sauna za moshi bado zina kitu cha kipee ambacho wengine walikuwa wamekipoteza kwa muda mrefu.
Kuanzia mwaka 2009, Veeroja aliongoza mpango wa kuanzisha sauna ya Võromaa iliyoorodheshwa na Unesco, mwaka 2014, iliongezwa kwenye orodha ya Turathi za Kitamaduni.

Chanzo cha picha, getty images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sauna za moshi zilitengenezewa makala ya video mwaka jana - iitwayo Smoke Sauna Sisterhood, iliyoongozwa na Anna Hints. Mzaliwa wa Võru.
Hints alitumia miaka saba kurekodi matukio ya kikundi cha wanawake walipotembelea sauna huko Estonia Kusini, ikiwa ni pamoja na Mooska.
Nilipozungumza na Hints juu ziara yangu kwenda Mooska, alinielezea jinsi kwenda kwenye sauna, hasa sauna ya moshi, na kusema inaweza kuwa mazoezi ya kiroho.
"Imekuwa ya matibabu, uchafu wa kimwili huanza kutoka na kisha uchafu wa kihisia. Bibi kila mara alikuwa akisema sauna huosha sio mwili wako tu, bali pia unaosha roho yako."
Nikiwa Mooska, ninasugua mwili wangu kwa majivu, jasho na kisha kujisafisha kwenye dimbwi lililofunikwa na barafu. Kisha kurudi kwenye sauna, ambapo ninajipiga kwa asali, napiga mwili wangu wote kutoka kwa nyayo za miguu hadi shingo yangu, kwa viht na tena kujitupa kwenye bwawa. Nilirudi kwenye sauna kwa mara nyingine tena, nilijilaza kwa tumbo ili Veeroja apeleke viht kwa mgongo wangu.
Manufaa ya Kiafya

Chanzo cha picha, Tõnu Runnel
Hapo awali, wakulima wa Estonia Kusini hawakuweza kupata madaktari ambao waliwatibu, kwa hivyo waligeukia sauna ili kuponya maumivu na huzini yao.
Siku hizi, watu wengi hutembelea madaktari wakiwa wagonjwa, lakini Veeroja, anaamini sauna inaweza kutumika kutibu magonjwa ya kiroho ya jamii ya kisasa.
Utafiti unaonyesha manufaa ya kimwili, ikiwa ni pamoja na kuboresha mzunguko wa damu na kinga ya mwili.
"Ikiwa mtu atapata faraja na kupenda kile tunachofanya katika sauna ya moshi, basi [sauna ya moshi] inaweza kuenea kama utamaduni wa yoga."
Kwa utambuzi wa kitamaduni uliotolewa na Unesco na umaarufu wa filamu ya Hints, Waestonia wanarudi kwenye mizizi yao na kutumia sauna ya moshi kupunguza maradhi ya kuungana tena na familia na asili huku wakitambua manufaa ya kiuchumi ya kuhifadhi utamaduni huu wa kale.
Katika ujana wake, Anti Konsap mwenye umri wa miaka 36 alitumia miaka miwili akiishi kwenye jengo la sauna na kaka yake mkubwa huku wazazi wake wakifanya kazi ya kumalizia ujenzi wa nyumba yao.

Chanzo cha picha, Silver Gutmann
Licha ya kukumbuka miaka hiyo kama wakati wa upweke na giza, Konsap hakuwahi kupoteza upendo wake kwa sauna. Hata wakati wa utumishi wake wa kijeshi, sauna zilitoa kitulizo kilichohitajiwa sana, kwani walikuwa wakifanya kazi mashambani hapo awali.
Mwaka jana, aliokoa kuta za sauna ya moshi iliyopangwa kubomolewa na akaajiri mjenzi kujenga upya sauna hiyo katika eneo la kusini mwa Võru. Sauna ya moshi ni mradi, ambao anatumai utaweza kutumika na wasafiri wanaokwenda Estonia.
Nilimuuliza Konsap ikiwa kumiliki sauna kunamfanya ahisi kuwa ameunganishwa na zamani. Anasema ndiyo, anaongeza, "Mimi si mtu wa dini sana, lakini nadhani sauna ni mahali pazuri ambapo unaweza kuzungumza na mizimu. Unafikiri kuhusu nyakati za kale na babu na watu ambao waliishi kabla yenu. Ni mahali pa kuungana na roho za zamani."
Katika giza la sauna huko Mooska, sizungumzi na mizimu. Siamini hilo, na kama ningefanya hivyo, ingekuwa Marekani, ninakotoka, si hapa Estonia.
Veeroja anaimba kwa Kiingereza, "You are whole; you are enough." Sijui kama nimeponywa yote yanayonisumbua, lakini ninahisi kuwa mzima na nipo katika mwili wangu na mahali hapa. Na hiyo inatosha.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












