Je, ni vyakula gani husababisha na kupunguza kiungulia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungulia ambacho kwa kawaida hujidhihirisha kama asidi inayounguza kwenye kifua, ni mojawapo ya dalili kuu za chakula kutosagwa vizuri na husababishwa na asidi ya reflux.
Dk Philip Woodland, mtaalamu wa magonjwa ya tumbo katika Hospitali ya Royal London na profesa wa Chuo Kikuu cha Queen Mary, London, anasema:
"Asidi hiyo hutokea wakati juisi ya tumbo, ambayo ni tindikali, inapopanda kutoka tumboni hadi kwenye koo, ambalo kwa kawaida halina vitu vyenye asidi,"
Vyakula gani husababisha kiungulia?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Sababu kuu ya kiungulia ni kula sana, kwani huongeza shinikizo kwenye tumbo," anasema Woodland.
"Vyakula vyenye mafuta mengi vinaweza kuwa vibaya zaidi katika kukuza aside ya relux. Pombe inaweza kusababisha kuongezeka aside hiyo. Kwa watu wengine, kafeini na chokoleti pia inaweza kuwa vichocheo."
Dkt James Kennedy, daktari wa magonjwa ya mfumo wa utumbo na mtafiti katika Hospitali ya Royal Berkshire na Chuo Kikuu cha Reading, anasema vinywaji vya kemikali pia ni kichocheo cha kiungulia.
Kuhusu vyakula kama chokoleti, tafiti zimeonyesha zinaweza kupumzisha misuli iliopo kati ya koromeo na tumbo, na hivyo kuruhusu yaliyomo ndani ya tumbo kupanda kwa urahisi zaidi.
“La muhimu ni kuondokana na vyakula vinavyokuletea kiungulia na kula vile ambavyo havikuletei matatizo, anasema Kennedy. Lakini anaonya: “Ni muhimu kutoacha kula kila kitu, ili usiache kula vyakula vya lishe.”
Unazuiaje kiungulia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Kwa bahati mbaya, hakuna vyakula maalumu vya kupambana na asidi ya reflux," anasema Woodland.
Ingawa inapendekezwa “kuepuka kula sana na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi, hasa wakati wa kulala. Hii itapunguza hatari ya kupata kiungulia.”
Woodland na Kennedy wanasema kuzuia kiungulia kupitia lishe ni bora zaidi kuliko kujaribu kuzuia dalili kupitia lishe.
"Mbali na kupunguza vyakula vya vinavyochochea kiungulia, kuna faida zingine za lishe bora ambazo zinaweza kuulinda mwili dhidi ya reflux…”
Kwa mfano, vyakula vya asili huwa na kiwango kidogo cha mafuta. Na vyakula hivi, mara nyingi havisababishi uzito wa kupindukia,” anasema Woodland.
"Kuna ushahidi kwamba vyakula vya matunda, mboga mboga, nafaka nzima, samaki na kuku vinaweza kupunguza hatari ya kupata kiungulia,” anasena Kennedy.
"Chai ya mnaa au mafuta ya mnaa, ni nzuri katika kupambana na shida za tumbo kama vile, tumbo kukaza, kuuma, kuvimba na gesi kwa sababu mnaa huifanya misuli ya tumbo kulegea…”
“Lakini hii inamaanisha kuwa italegeza misuli hiyo na itaruhusu asidi zaidi kupanda juu na kuzidisha kiungulia. Kwahiyo mnaa sio tiba sahihi kwa kiunguli,” anasema Kennedy.
Kuna watu wako hatarini zaidi?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kama ilivyo kwa mtu mnenen na mjamzito, kuna kuongezeka kwa asidi ya reflux kwa watu hao. Kwa bahati nzuri, asidi hii hupungua baada ya mtoto kuzaliwa,” anasema Woodland.
"Asidi hiyo huwepo mara kwa mara tunavyozeeka, lakini haina athari kubwa.” Lakini Kennedy anaonya dalili mpya zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
"Dalili mpya za reflux zinazoonekana baada ya umri wa miaka 55 hazipaswi kupuuzwa na unapaswa kumuona daktari - kwani zinaweza kuwa kwa sababu ya jambo kubwa zaidi."
Woodland anaeleza “kwa watu wengi, kupata kiungulia mara kwa mara ni kawaida na hazipaswi kusababisha hofu au mabadiliko makubwa ya maisha.”
"Jambo muhimu zaidi ni kujaribu kupunguza uzito kupita kiasi na kuacha kuvuta sigara. Ni muhimu kutumia kwa kiasi vyakula na vinywaji vya kuchochea asidi hiyo (hasa pombe)."
Epuka vyakula vyenye mafuta mengi, haswa karibu na wakati wa kulala, na ikiwezekana, jaribu kula masaa 3 hadi 4 chakula cha jioni kabla ya kulala.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












