'Walimpiga mwanangu kwa kukataa kupigana nchini Ukraine'

Sergei (sio jina lake halisi) anasema mtoto wake alipigwa bastola kwa kukataa kurejea mstari wa mbele.
Maelezo ya picha, Sergei (sio jina lake halisi) anasema mtoto wake alipigwa bastola kwa kukataa kurejea vitani.

Wakati mtoto wake alipelekwa kupigana nchini Ukraine, Sergei alimsihi asiende. "Una jamaa huko. Kataa tu, "Sergei anakumbuka akimwambia Stas, ambaye tayari alikuwa afisa wa jeshi.

"Lakini alisema anaenda. Aliamini ni sawa. Nilimwambia kwamba alikuwa hajielewi. Na kwamba, kwa bahati mbaya, maisha yangethibitisha hilo."

Sergei na Stas sio majina halisi ya baba na mwanawe huyu. Tumezibadilisha ili kulinda utambulisho wao.

Sergei ametualika nyumbani kwake ili kutusimulia hadithi yao.

"Basi alienda Ukraine. Kisha nikaanza kupokea ujumbe kutoka kwake akiuliza nini kingetokea ikiwa angekataa kupigana."

Stas alimwambia baba yake juu ya vita moja maalum. "Alisema wanajeshi [wa Urusi] hawakupewa ulinzi wowote; hakukuwa na taarifa za kijasusi; hakuna maandalizi. Walikuwa wameamriwa kusonga mbele, lakini hakuna aliyejua nini kitatokea.

"Lakini kukataa kupigana ulikuwa uamuzi mgumu kwake kuchukua. Nilimwambia: 'Bora kuuchukua. Hivi si vita vyetu. Si vita vya ukombozi.'

Alisema angeandika kukataa kwake. Yeye na wengine kadhaa ambao waliamua kukataa walinyang'anywa bunduki zao na kuwekwa chini ya ulinzi wenye silaha."

Sergei alifanya safari kadhaa kwenye mstari wa mbele kujaribu kupata kuachiliwa kwa mtoto wake. Aliwashambulia maafisa wa kijeshi, waendesha mashtaka na wachunguzi kwa maombi ya msaada. Hatimaye jitihada zake zilizaa matunda.

Stas alirudishwa Urusi. Alimsimulia baba yake kile kilichompata akiwa kizuizini: jinsi "kundi tofauti" la askari wa Urusi walijaribu kumlazimisha kupigana.

Kuna ripoti za wanajeshi wa Urusi waliohamasishwa waliofungiwa katika vyumba vya chini ya ardhi na vyumba vya chini kwa chini kwa kukataa kupigana nchini Ukraine

Chanzo cha picha, THE INSIDER

Maelezo ya picha, Kuna ripoti za wanajeshi wa Urusi waliohamasishwa kufungiwa katika vyumba vya chini ya ardhi kwa kukataa kupigana nchini Ukraine
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Walimpiga kisha wakamtoa nje kana kwamba wanataka kumpiga risasi, wakamlaza chini na kumwambia ahesabu hadi kumi, akakataa, wakampiga kichwani mara kadhaa kwa bastola.Aliniambia uso wake ulikuwa umejaa damu.

"Kisha wakampeleka ndani ya chumba kimoja na kumwambia: 'Unakuja pamoja nasi, vinginevyo tutakuua.' Lakini mtu fulani alisema wangemchukua mwanangu kufanya kazi katika ghala."

Stas alikuwa afisa anayehudumu wakati Urusi ilipozindua uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari.

Rais Vladmir Putin aliahidi kwamba ni wanajeshi wenye taaluma pekee ndio watashiriki katika "operesheni yake maalum ya kijeshi."

Lakini kufikia Septemba mambo yalikuwa yamebadilika. Rais alitangaza kile alichokiita "uhamasishaji wa sehemu", akiandika maelfu ya raia wa Urusi katika vikosi vya jeshi.

Wanajeshi wengi wapya waliohamasishwa walikuwa wepesi kulalamika kwamba walikuwa wakitumwa kwenye eneo la vita bila vifaa vya kutosha au mafunzo ya kutosha.

Kutoka Ukraine kumekuwa na ripoti nyingi za wanajeshi wa Urusi waliohamasishwa kuzuiliwa - katika visa vingine, wamefungwa kwenye vyumba vya chini vya ardhi na vyumba vya chini - kwa kukataa kurudi kwenye mstari wa mbele.

Mwanamke

"Ni njia ya kuwafanya watu warudi kwenye umwagaji damu huo," anasema Elena Popova kutoka shirika la Urusi la Movement of Conscientious Objectors. "Lengo la makamanda ni kuwaweka askari chini pale.

Makamanda wanajua vurugu na vitisho tu. Lakini huwezi kuwalazimisha watu kupigana." Kwa Warusi wengine, kukataa kurudi kwenye mstari wa mbele kunaweza kuwa msimamo wa maadili.

Lakini kuna maelezo ya kawaida zaidi."Wale wanaokataa kupigana wanafanya hivyo kwa sababu wamekuwa na zaidi ya sehemu yao ya haki katika mstari wa mbele," anaelezea Elena Popova.

"Sababu nyingine ni njia chafu wanayotendewa. Wametumia muda kwenye mitaro, wakipigwa na baridi na njaa, lakini wanaporudi tu wanapigiwa kelele na kuapizwa na makamanda wao."

Mamlaka ya Urusi inapuuzilia mbali ripoti za askari waliokatishwa tamaa na vituo vya kuwazuial wanaokaidi amri kama habari za uwongo.

"Hatuna kambi zozote au vifaa vya kuwafunga, au mengine kama hayo [ya wanajeshi wa Urusi]," Rais Putin alisisitiza mapema mwezi huu.

"Haya yote ni madai ya upuuzi na ya uwongo na hayana msingi wowote."

"Hatuna matatizo yoyote na askari anayeachana na mapigano," kiongozi wa Kremlin aliendelea kusema.

Andrei, Luteni wa Urusi, aliacha kupigana. Alipelekwa Ukraine mnamo Julai, Andrei aliwekwa kizuizini kwa kukataa kutekeleza maagizo.

Alifanikiwa kuwasiliana na mama yake, Oxana, aliyerudi Urusi ili kumweleza kilichokuwa kikiendelea.

Kwa mara nyingine tena, tumebadilisha majina yao. "Aliniambia alikuwa amekataa kuwaongoza watu wake kwenye kifo fulani," Oxana ananiambia.

"Kama afisa alielewa kuwa ikiwa wangetangulia mbele, hawatanusurika kifo. Kwa hiyo walimpeleka mwanangu kwenye kituo cha kuzuilia watu.

Kisha nikapokea ujumbe mfupi ukisema yeye na maafisa wengine wanne walikuwa wamewekwa katika chumba cha chini cha ardhi.

Hawajaonekana kwa miezi mitano. “Baadaye niliambiwa jengo walilokuwemo limepigwa makombora na watu wote watano hawapo, wakasema hakuna mabaki yaliyopatikana, hadhi yao rasmi haipo kiutendaji, haina maana, ni upuuzi. Mwanangu aliteswa haikuwa tu kinyume cha sheria, ilikuwa ni unyama."

Aliporudi sebuleni kwake, Sergei ananiambia kwamba kilichomkuta Stas huko Ukraine kimewaleta karibu zaidi.