Mzozo wa Ukraine: Je wanajeshi wa Urusi walipigwa risasi baada ya kujisalimisha?

.
Maelezo ya picha, Mwanajeshi asiyetambulika akiwa amesimama na wnegine wakiwa wamelala ardhini

Video imeibuka kutoka mstari wa mbele wa vita mashariki mwa Ukraine ikionyesha kujisalimisha kwa kundi la wanajeshi katika tukio ambalo linaonekana kumalizika kwa vifo vyao.

Urusi imejibu kanda hiyo, ikiishutumu Ukraine kwa kuwanyonga wafungwa wa kivita wa Urusi, jambo ambalo lingekuwa uhalifu wa kivita. Ukraine bado haijajibu madai hayo.

BBC haijaweza kubainisha madai ya Urusi kutokana na video hiyo pekee, lakini tumekuwa tukichunguza kanda hiyo, tukijaribu kuunganisha kile ambacho kingeweza kutokea.

.
Maelezo ya picha, Ramani ya eneo la Soverodonetsk

Tukio hilo lilitokea Jumamosi au kabla ya tarehe 12 Novemba huko Makiyivka, kijiji kilicho mstari wa mbele katika mkoa wa Luhansk.

.
Maelezo ya picha, Eneo la tukio

Picha za ndege zisizo na rubani zilionekana baadaye siku hiyo na siku ya Jumapili kwenye tovuti zinazounga mkono Ukraine zikionyesha miili ya wanajeshi kadhaa waliovalia sare ikiwa imelala chini kwenye ardhi.

.

Chanzo cha picha, twitter

Maelezo ya picha, Wanajeshi waliotekwa waliagizwa kulala chini

Sehemu ya video kutoka eneo hili pia inaonekana katika video iliyowekwa mtandaoni na Wizara ya Ulinzi ya Ukraine kuhusu operesheni za kijeshi katika eneo la Makiyivka.

Baadhi ya machapisho kwenye mitandao ya kijamii yanadokeza kwamba shambulio la kufyatua risasi lilifanyika.

Lakini toleo hilo la matukio limepingwa na vyombo vinavyounga mkono Urusi vinavyodai kuwa wanajeshi hao walipigwa risasi na wafanyakazi wa kikosi cha 80 cha mashambulizi ya anga ya Ukraine.

Kisha tarehe 17 Novemba kanda zaidi za video ziliibuka, wakati huu zilirekodiwa kutoka ngazi ya chini na mtu aliyekuwepo kwenye eneo la tukio, na kelele zinaweza kusikika kwa lugha ya Ukraine kwa yeyote aliyejificha ndani ya kibanda kutoka nje.

Wanajitokeza mmoja baada ya mwingine na kulala chini.

.
Maelezo ya picha, Huu ndio wakati mtu aliyevalia magwanda meuzi anajitokeza na kufyatua risasi

Sauti zinaweza kusikika zikiuliza ikiwa kila mtu yuko nje.

Watekaji wanazungumza kwa lugha ya Ukraine kwenye video, wakati sare za mateka zinaonekana kuwa za Kirusi na sio za wanajeshi wa Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Urusi na vyombo vya habari pia vimesema wafungwa hao ni Warusi.

Kisha video hii inaonyesha mwanamume aliyevalia mavazi meusi akiibuka. Anaonekana kuwa na silaha na kufyatua risasi huku akipiga hatua mbele.

Hatuwezi kujua kutoka kwa video kama mwanamume huyo ni Mrusi au ni wa Ukraine na ni nini anachokifyatulia risasi.

.
Maelezo ya picha, Ufyatuaji risasi katika eneo la Makiyivka

Kisha kamera inaanguka huku milio ya risasi ikilia. Video inaisha kwa kuchanganyikiwa kwa ukungu.

Picha za angani (kutoka kwa ndege isiyo na rubani) na video iliyorekodiwa ardhini inaonekana kufanana na eneo hilo.

Lango la kuingilia - lenye kile kinachoonekana kama nguzo iliyolala juu yake - linaonekana katika picha zote mbili (zilizoangaziwa kwa rangi ya zambarau) na vile vile kinachofanana na gari jekundu la kutembelea shambani (kilichoangaziwa kwa rangi ya chungwa).

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wizara ya ulinzi ya Urusi imeshutumu kile kilichotokea kama "mauaji ya kimakusudi na ya kidesturi" kwa kuwapiga risasi wanajeshi zaidi ya 10 wa Urusi wasio na uwezo wa kujisaidia.

Inaendelea kusema kuwa "sio uhalifu wa kwanza na sio uhalifu wa kivita pekee" wa vikosi vya Ukraine.

Kuua au kumjeruhi mpiganaji ambaye ameweka silaha chini na kujisalimisha ni uhalifu wa kivita.

Urusi imeshutumiwa kwa uhalifu mwingi wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia huko Bucha - ambayo pia tumechunguza.

Kujisalimisha na kubadilishana wafungwa wa vita kimekuwa kitu muhimu katika vita hivi vilivyodumu karibu miezi tisa.

Katika ripoti ya wiki hii, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine uliripoti unyanyasaji wa wafungwa unaofanywa na pande zote mbili. Idadi kubwa ya wafungwa wa Ukraine walioachiliwa waliozungumza nao walisema waliteswa na kutendewa vibaya na watu tisa walikufa.

Wikendi iliyopita kuliibuka video ya kutisha ambayo ilionekana kuonyesha kifo cha mamluki mikononi mwa kundi la Wagner la Urusi.

Picha ambazo hazijathibitishwa zilionyesha Yevgeny Nuzhin, 55, akipigwa kichwani

Bosi wa Wagner Yevgeny Prigozhin baadaye alimshtumu kwa kuisaliti Urusi na wenzake.

.

Chanzo cha picha, Yuri BUtosov and Youtube

Maelezo ya picha, Yevgeny Nuzhin alifanya mahojiano na mwandishi wa habari wa Ukraine mnamo Septemba

Nuzhin, muuaji aliyepatikana na hatia, alikuwa ameonekana kwenye video ya Ukraine baada ya kunaswa, akitangaza kuwa amebadilisha msimamo wake .

Jinsi tu alivyoishia mikononi mwa Urusi haijulikani, lakini maafisa wa Ukraine walisema hakujisalimisha kwa hiari hivyo hakuzingatiwa kama mtu ambaye angeweza kubadilishwa.

Mabadilishano ya wafungwa wa vita yalifanyika tarehe 11 Novemba lakini Nuzhin hakuwa mmoja wao.

Anaonekana kushambuliwa mjini Kyiv kabla ya kukamatwa na watu waliomuua.