"Kuumaliza utawala wa Khamenei ni chaguo pekee la Israeli katika mgogoro wake na Iran" - Yedioth Ahronoth

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 8

Katika uchanganuzi wa magazeti ya leo, tutajadili makala kadhaa, ikiwemo inayosema kuwa chaguo pekee kwa Israeli katika mgogoro wake na Iran ni kuumaliza utawala wa Khamenei, na nyingine inahusu fursa inayopatikana kwa Iran na nchi za Kiarabu kuunda mfumo mpya, rahisi zaidi na endelevu wa kikanda, na hatimaye makala kuhusu mgawanyiko wa muungano wa Magharibi baada ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu kutoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu.

Tunaanza na gazeti la Israeli Yedioth Ahronoth na makala ya maoni iliyoandikwa na Jacob Nagel na Mark Dubowitz yenye kichwa cha habari "Chaguo la Pekee la Israeli kuhusu Iran ni kukomesha Utawala wa Khamenei." Mwandishi anaanza kwa kurejelea kauli ya awali ya kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei, ambapo alitabiri uharibifu wa mwisho wa Israeli ifikapo mwaka 2040.

Mwandishi anasema kwamba wakati Khamenei anapotangaza kwamba mpango wake ni kuiangamiza Israel wakati huo, bila shaka anafanya kila awezalo kufikia azma hii, kwa msaada wa wafuasi wa Iran nyumbani na nje ya nchi, na lazima tushughulikie suala hilo kwa umakini.

Mwandishi anaongeza kuwa Israel haipaswi kuridhika na mkakati wa kuzuia kushambuliwa kama lengo lake, badala yake inapaswa kubadilisha mkakati wake kabisa na kuhama kutoka ulinzi hadi mashambulizi ya vitendo, ili lengo la Israeli liwe kumaliza utawala wa Khamenei ifikapo mwaka 2030.

Mwandishi anaamini kuwa utawala wa Iran ndio mfadhili mkuu wa ugaidi duniani, na kuyumbisha Mashariki ya Kati, ikitamani kumiliki silaha za nyuklia, akibainisha kuwa Tehran imejihami na kuongoza kile anachokiita "makundi ya kigaidi", kama vile Hezbollah, Hamas, na Islamic Jihad kwa miongo kadhaa, kwa lengo la kuunda eneo la vita karibu na Israeli.

Mwandishi anasema kuwa kuiruhusu Iran kuendelea kuchochea mzozo huo sio suluhisho, na kutochukua hatua sio mkakati mzuri kwa Israel katika kukabiliana na tisho la Iran, na Israeli haipaswi kuendelea kuepuka vitisho vya Khamenei, badala yake inafaa kuondoa chanzo cha vitisho hivi.

Mwandishi anasema kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya kijeshi dhidi ya Hezbollah na Hamas, na uharibifu wa ulinzi wa anga wa Iran, inathibitisha kuwa jeshi la Israeli lina uwezo wa kumshinda mpinzani wa kisasa kama huyo, kwa kutumia akili sahihi, teknolojia ya hali ya juu, na operesheni sahihi za anga, na kwamba utaalam huu unaweza kuelekezwa kimkakati kuelekea kulenga maeneo ya nyuklia ya Iran.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bango linalomuonesha kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei limewekwa karibu na kombora la masafa marefu katika uwanja wa Baharestan mjini Tehran.

Mwandishi anaamini kwamba kwa kuchaguliwa kwa Donald Trump kama rais wa Marekani, operesheni ya pamoja ya Israeli na Marekani haiwezekani na iwapo itawezekana itaongeza sana fursa mafanikio, kwa kushirikiana na uendeshaji wa Israeli na mifumo ya kiteknolojia na nguvu za mashambulizi za Marekani na vikosi maalum, pamoja na diplomasia

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa maoni ya mwandishi, vita vya kiuchumi, bado ni moja ya zana zenye nguvu zaidi dhidi ya Iran, baada ya vikwazo vya awali kama sehemu ya kampeni ya shinikizo viliharibu vibaya mapato ya mafuta ya Iran na kupunguza uwezo wake wa kufadhili mtandao wake wa kivita wa nje.

Mwandishi anaamini kuwa juhudi za kidiplomasia zinapaswa kuzingatia kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiarabu, kusaini makubaliano ya amani na Saudi Arabia, na kujenga ushirikiano mpya, hasa kwa kuwa mashambulizi ya Iran, hasa kwa msaada wa Urusi, na vitisho vinavyoendelea kwa washirika wa Marekani katika Ghuba, vimeunda fursa mpya za kuunda ushirikiano dhidi ya Iran.

Mwandishi anaamini kwamba ushirikiano huu lazima ufanye kazi sio tu kuizuia Iran, lakini pia kudhoofisha na kumaliza utawala wake, wakati wa kuimarisha juhudi za kuvuruga ratiba ya nyuklia ya Iran, kuwalenga wanasayansi wake wa nyuklia na viongozi wa jeshi la mapinduzi la Iran, kutumia vita vya kielektroniki vya Israeli, na kuzingatia vipengele muhimu vya udhaifu katika utawala wake.

Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema kuwa Israel haipaswi kusubiri hadi 2040 wakati Khamenei anapanga kuiangamiza. Kama hilo ndilo lengo lake, basi jukumu la Israel ni kuuangusha utawala wake.

Ushindi ndio chaguo pekee, na hii inamaanisha kuhakikisha kuwa utawala wa Khamenei unakuwa kitu cha zamani, muda mrefu kabla ya ratiba yake kukaribia tarehe yake ya mwisho.

"Utaratibu Mpya wa Mkoa"

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Iran (kulia) akiwatazama maafisa wa Saudi Arabia wakisimama karibu na bendera ya Saudi Arabia katika jengo la wizara ya mambo ya nje mjini Tehran.

Tukiangazia gazeti la Asharq Al-Awsat lenye makao yake London na kipande cha maoni kilichoandikwa na Nadim Koteich chenye kichwa "Fursa ya Irani na ya Waarabu kwa mfumo mpya wa kikanda," mwandishi anaanza kwa kuhoji: Je, mahusiano ya Irani na nchi za Kiarabu yana fursa mpya katikati ya matukio ya kijiografia na kuharakisha mabadiliko ya ndani na nje? Anaona fursa adimu ya kurekebisha uhusiano wa kikanda na kwenda zaidi ya muktadha unaosababisha kuendelea kwa migogoro na usawa.

Mwandishi anasema kwa bahati nzuri, au kutokana na ufahamu wa kisiasa, mabadiliko katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia mnamo Machi 2023 yalitarajia kungekuwa na vita vya Gaza kwa karibu miezi 6, kupitia upatanishi wa China ambao ulimaliza mgawanyiko wa miaka mingi na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Riyadh na Tehran.

Mwandishi anaongeza kuwa baada ya vita vya Gaza, mkutano kati ya rais wa Milki za Kiarabu (UAE), uliofanyika kando ya mkutano wa kilele wa BRICS mnamo Oktoba 2024, na mwenzake wa Iran, Masoud Pezeshkian, huko Kazan, Urusi, uliashiria hatua ya kushangaza ya kidiplomasia katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Vile vile, Bahrain, ambayo imekumbwa na mvutano wa muda mrefu na Iran, ilianza mazungumzo na jirani yake mnamo Juni 2024 kwa lengo la kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha uwazi wa kisiasa kati ya mataifa ya Ghuba na Iran.

Oktoba 2024 tukio lisilo la kawaida, lilishuhudiwa pia mwezi Oktoba 2024 kwani ilitangazwa kuwa Saudi Arabia itashiriki katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika bahari ya Shamu pamoja na Iran, Oman na Urusi.

Baadaye, ujumbe wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Saudi Arabia ukiongozwa na mkuu wa majeshi ya Saudi Arabia uliitembelea Iran na kukutana na maafisa wa kijeshi wa Iran, husasn mkuu wa majeshi ya Iran.

Mwandishi anaamini kwamba mikutano hii inapata umuhimu zaidi kwa kuzingatia kuzorota kwa sheria za ushirikiano kati ya Iran na Israeli, na harakati zao kuelekea uwezekano wa mapambano ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili, baada ya mfululizo wa mashambulizi makali.

Kubashiri kwao pia kumewezekana zaidi kutokana na mashambulizi ambayo yamesababishwa na washirika wa Iran katika eneo hilo, Hamas na Hezbollah.

Mwandishi anaamini kuwa kudhoofisha makundi haya mawili, na kutumia uwezo wa Iran wa kutumia makundi haya mawili ya ushawishi wa kisiasa na kijeshi katika eneo hilo, kuna uwezo wa kuisukuma Iran kuimarisha uhusiano wake na nchi za Kiarabu na kukabiliana na mabadiliko ya mienendo ya kikanda.

Mwandishi anaamini kwamba kurudi kwa Donald Trump katika ikulu ya White House, ingawa inaonekana kuwa sababu ya kuongezeka kwa mvutano na Iran, kunafungua fursa za uhusiano katika mahusiano mema na Iran. Katika wakati ambapo mataifa ya Ghuba, hasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, yanatafuta kuepuka kuhusika katika kuzidisha uhasama kwa eneo lolote linalohusiana na sera za Marekani dhidi ya Iran, kwa njia ambayo inatishia miradi yao mikubwa ya maendeleo.

Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema kuwa kupitishwa kwa sera za kuongeza nguvu dhidi ya China kutasababisha mataifa ya Ghuba kuongeza mara mbili dau lao juu ya kuimarisha ushirikiano wao na kuimarisha usalama wa kikanda, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mazungumzo na Iran.

Anaamini kuwa eneo hilo linakabiliwa na fursa ya ushirikiano ambao huenda sio zaidi ya kutuliza tu mvutano wa nchi mbili, bali ni pia fursa ya kuanzisha mfumo mpya wa utawala wa kikanda ambao ni rahisi zaidi na endelevu.

"Janga kwa Israel na tatizo kwa muungano wa mataifa ya magharibi"

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya akaunti ya mtandao iliyo na jina la waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na maneno Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa nyuma.

Tunahitimisha uchanganuzi wetu na gazeti la Uingereza, la Financial Times, na kipande cha maoni kilichoandikwa na Gideon Rachman chenye kichwa cha habari "Israeli itagawanya muungano wa Magharibi."

Mwandishi anaanza kwa kusema kwamba kutolewa kwa waranti ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita dhidi ya waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Galant kwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita ni janga kwa Israeli, na pia inaleta shida kubwa kwa muungano wa Magharibi.

Israel ina uungwaji mkono kamili wa pande zote mbili nchini Marekani, na inataka kuondoa mashtaka ya ICC dhidi ya waziri mkuu wake na waziri wa zamani wa ulinzi, lakini serikali nyingi katika Umoja wa Ulaya, pamoja na Uingereza, Australia na Canada, zina uwezekano wa kuheshimu mashtaka hayo na zitasita kumkamata Netanyahu ikiwa atakanyaga ardhi yao. Mwandishi anasema.

Mwandishi anaamini kuwa utawala wa Trump utashinikiza vikwazo dhidi ya mwendesha mashtaka na wafanyakazi wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, na pia kuna mazungumzo katika duru za Republican kuhusu kuilenga mahakama, labda kwa kutishia kuziadhibu nchi zinazofadhili. Japan, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ni wafadhili wakuu wanne wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).

Si Israel wala Marekani zinazoonekana kuwa na nia ya kujihusisha na mashtaka hayo, ambayo yanajumuisha shutuma kwamba Israel iliua raia na kutumia "njaa kama njia ya vita." Badala yake, Trump anakubaliana na madai ya Netanyahu kwamba ICC ina chuki dhidi ya Wayahudi. Kwa upande mwingine, ukweli kwamba mahakama pia imemshtaki Rais wa Urusi Vladimir Putin, Hamas na viongozi kadhaa wa Afrika watapuuzwa, na lengo litakuwa ni kuitangaza mahakama hiyo na wasaidizi wake wa Ulaya kama kuwa wenye chuki dhidi ya Wayahudi.

Mwandishi anasema kwamba baadhi ya nchi za EU, kama vile Ujerumani, zimejitolea kwa Israeli kwa uhakika kwamba zinaweza kukiuka Mahakama ya kimataifa ya uhalifu licha ya kutambua uhalali wake, lakini azma ya nchi nyingi za Ulaya itakuwa kukunga mkono kwa kile wanachokiita haki ya Israeli ya kujitetea.

Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kubainisha kwamba mapambano yanayoibuka kati ya Marekani na washirika wake juu ya Israeli ni sehemu ya mjadala mpana zaidi juu ya mustakabali wa mfumo wa kimataifa. Kama taifa lenye nguvu zaidi ulimwenguni, Marekani inaweza kuhisi kuwa changamoto ya sheria za kimataifa na taasisi za kimataifa ni kitu ambacho wanakihitaji ni watu dhaifu wa Ulaya wanaokihitaji.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah