'Zaidi ya muujiza', hivi ndivyo Man Utd walivyoshinda kwa njia ya ajabu dakika za lala salama

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika dakika ya 109 kwenye Uwanja wa Old Trafford wakati mshambuliaji wa Lyon, Alexandre Lacazette, alipoonekana kuhitimisha msimu wa Manchester United. Ulikuwa usiku wa mchezo mtamu wa Europa League.

Maelfu ya mashabiki walianza kuondoka uwanjani wakiwa nyuma kwa mabao 4-2 usiku huo, na 6-4 kwa jumla. Zilibaki dakika 11 tu. Mchezo umeisha.

"United wanahitaji zaidi ya muujiza," alisema Rio Ferdinand, beki wa zamani wa United aliyekuwa akitoa maini yake kupitia kituo cha runinga cha TNT Sports.

Kisha muujiza ukatokea.

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Zikisalia dakika 11, Lyon walionekana wangeweza kuongeza magoli, kuliko United kurejesha bao hata moja

Lakini kama wimbo maarufu unavyosema, "Man Utd hawatakufa kamwe." Ni kweli hawafi na wakifa hawafi kirahisi.

Bruno Fernandes, labda mchezaji pekee wa United aliyeonekana kuwa katika kiwango bora msimu huu, alipunguza pengo la magoli kwa mkwaju wake wa penalti baada ya Casemiro kuchezewa vibaya katika eneo hatari. Dakika sita zikiwa zimebaki.

,

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bruno Fernandes alifunga penati muhimu na kuokota mpira kukimbilia kati kuokoa muda

Katika dakika ya 120, mchezaji wa akiba Kobbie Mainoo alifungfa bao zuri. Imekuwa kampeni ngumu kwa kiungo huyo chipukizi wa England baada ya kung'aa msimu uliopita, lakini huu ulikuwa wakati unaoendana na ubora wake.

Mechi sasa ilikuwa sare usiku huo na kwa matokeo ya jumla. Kila mtu alikuwa anasubiri uamuzi wa mikwaju ya penati, ikiwa ni wiki sita tu zimepita tangu walipotolewa kwa penati katika Kombe la FA.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Goli la pili kwa msimu huu kwa Mainoo, linatabaki kwenye kumbukumbu ya muda mrefu kwa mashabiki wa United

Lakini Harry Maguire alisema hapana, beki ambaye mara nyingi huwa mhanga wa lawama katika anguko la taratibu la United, aliibuka tena katika wakati huu muhimu. Muda mfupi tu baada ya bao la Mainoo, Maguire alifunga kwa kichwa na kusherehekea kwa shangwe kubwa. Uwanja ulilipuka kwa mashabiki waliosalia uwanjani.

Kizaazaa kikazuka.

"Sijawahi kuona kitu kama hicho kama mtazamaji. Ilikuwa ya kushangaza sana. Tuliona mashabiki wengi wakiondoka uwanjani matokeo yalipokuwa 4-2 na waliamni mchezo umekwisha," alisema Rio Ferdinand.

"Nilisema kwenye maoni kuwa ingetakiwa zaidi ya muujiza kurudi mchezoni – sasa naamini (miujiza imetokea) kwa sababu hilo lilikuwa la ajabu."

'Sijawahi kuona kitu kama hiki'

Kipa wa zamani wa England, Paul Robinson, pia alishangazwa sana alipozungumza na BBC Radio 5 Live.

"Mandhari ndani ya Old Trafford ni ya kipekee. Sijawahi kuona kitu kama hiki. Kizaazaa. Walinzi wako uwanjani, mashabiki wapo uwanjani na hata wafanyakazi. Andre Onana anazunguka uwanjani akisherehekea. Old Trafford haijawahi kuona hali kama hii kwa miaka mingi," alisema.

"Sidhani kama nimeshawahi kuona mechi kama hii. Walionekana kufa kabisa. Sijawahi kuona kitu kama hiki kutoka kwao msimu huu. Sina maneno ya kusifu zaidi."

Hakujawahi kushuhudiwa magoli matano yakifungwa katika muda wa nyongeza kwenye mchuano wa hatua ya mtoano Ulaya kabla ya hapo. Kurejea kwa United mchezoni na kufunga mabao hayo kulikuwa kama ndoto – lakini Old Trafford mambo ya ajabu huweza kutokea.

,

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maguire akifungwa bao muhimu katika dakika ya 120+1, ikiwa ni dakika moja baada ya goli la Mainoo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Umewahi kuona mambo maalum yakitokea hapa. Nakumbuka lile goli la Ole Gunnar Solskjaer dhidi ya Liverpool mwaka 1999. Hii ilinikumbusha kidogo, japo ile ilikuwa 2-1 na hii ni 5-4," alisema Paul Scholes kupitia TNT Sports.

"Kila mara nikihisi tukipata bao moja hapa – kuna uwezekano."

Labda beki wa United, Leny Yoro, aliliweka vizuri zaidi:

"Kwa kweli sielewi kilichotokea. Ilikuwa jambo la uwendawazimu! Mashabiki walitusaidia. Unapowasikia mashabiki, hata ukiwa nyuma 4-2, unajua tunaweza. Tuliamini, usipoamini huwezi kushinda. Haya ndiyo mashabiki wanastahili, wanatoa kila kitu kila mechi."

United kwa sasa ni wa 14 kwenye ligi kuu England na wako mbioni kumaliza msimu wakiwa na pointi chache zaidi katika historia ya EPL.

Lakini sasa wana kitu cha kupigania. Wakiichapa Athletic Bilbao kwenye nusu fainali mwezi ujao, watafuzu fainali ambayo itapigwa San Mames, uwanjani kwa Bilbao.

Na kama watatwaa kombe hilo, licha ya kuwa nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi, watafuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Lakini mashabiki hawatawaza hayo sasa watakuwa wakikumbuka tukio la Old Trafford kwa miaka mingi ijayo.

Matokeo mengine ya Robo Fainali – Europa League na Conference League

Europa League

- Bayer Leverkusen 1-1 West Ham (Leverkusen 3-1 kwa jumla)

- Atalanta 2-2 Liverpool (Atalanta 3-2 kwa jumla)

- Roma 2-1 AC Milan (Roma 3-1 kwa jumla)

- Man Utd 5-4 Lyon (Man Utd 9-8 kwa jumla)

Conference League

- Aston Villa 1-1 Lille (Villa walishinda kwa penalti)

- Fiorentina 2-0 Viktoria Plzen (Fiorentina 2-0 kwa jumla)

- Club Brugge 3-0 PAOK (Brugge 3-0 kwa jumla)*

- Olympiacos 2-1 Fenerbahce (Olympiacos walishinda kwa penalti)*

Michezo ya Nusu Fainali

Europa League

- Manchester United vs Athletic Bilbao

- Bayer Leverkusen vs Roma

Conference League

- Aston Villa vs Olympiacos

- Fiorentina vs Club Brugge