Je, England kuingiza timu 7 Ligi ya Mabingwa Ulaya? Inawezekanaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Callum Matthews
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ligi kuu ya England ina uhakika wa kuingiza timu tano katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao baada ya Arsenal kuishinda Real Madrid katika mkondo wa kwanza wa robo fainali.
Uingereza inaweza kuwa na timu kama saba kwenye Ligi ya Mabingwa msimu wa 2025-26 ikiwa Aston Villa itashinda shindano hilo mwaka huu, lakini ikishindwa kufuzu kupitia Ligi Kuu ya England, na ikiwa Manchester United au Tottenham watashinda Ligi ya Ulaya.
Nafasi za ziada za Ligi ya Mabingwa
Kila ligi ya nchi hupata nafasi kulingana na jinsi timu zao zinavyofanya kazi katika mashindano matatu ya vilabu vya wanaume ya Uefa: Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Ulaya na Ligi ya Conference.
Pointi zilizopatikana na vilabu kutoka ligi ya ndani hujumlishwa na kugawanywa kwa idadi ya vilabu vinavyocheza ligi ya Ulaya.
Kwa mfano, kama Ligi Kuu ya England ingekuwa na pointi 100, hiyo ingegawanywa kwa idadi ya timu zinazocheza katika mashindano ya Ulaya (saba), na kuipa England mgawo wa 14.28.
Msimu huu, pointi za bonasi zinapatikana kwa vilabu vinavyocheza Ligi ya Mabingwa, jambo ambalo ni la manufaa kwa ligi zenye vilabu vingi vinavyoshindana, kama vile Ujerumani na Italia.
Nchi ambazo zitamaliza katika nafasi mbili za juu ya jedwali hupata nafasi ya ziada ya kuingiza timu katika Ligi ya Mabingwa kwa msimu unaofuata.
Nafasi hizo hutolewa kwa timu zinazomaliza katika nafasi ya kwanza chini ya kiwango cha mgao wa Ligi ya Mabingwa katika ligi hizo.
Katika Ligi ya England, vilabu vinne vya juu hufuzu moja kwa moja kwenda Ligi ya Mabingwa kupitia msimamo wa ligi, kwa hivyo nafasi yoyote ya ziada inaweza kwenda kwa timu iliyo ya tano.
Nafasi za ziada za Ligi ya Mabingwa 2024-25 zilitolewa kwa Bologna na Borussia Dortmund, ambao walimaliza wa tano kwenye Serie A na Bundesliga.
Washindi wa Ligi ya Ulaya
Uingereza inaweza kuingiza timu saba Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Washindi wa Ligi ya Ulaya, pamoja na Ligi ya Mabingwa, wamepewa nafasi.
Chini ya sheria za awali, ligi yoyote inaweza kuwa na vilabu vitano pekee kwenye Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, sheria hiyo imetupiliwa mbali.
Msimu huu, timu yoyote itakayoshinda Ligi ya Ulaya au Ligi ya Mabingwa lakini haijafuzu Ligi ya Mabingwa kupitia msimamo wa ligi ya nyumbani itaingia kwenye Ligi ya Mabingwa.
Ikiwa Aston Villa itashinda Ligi ya Mabingwa na kumaliza nje ya tano bora kwenye Ligi Kuu England basi hilo litazipa klabu za Uingereza nafasi kwa timu hiyo kuingia Ligi ya Mabingwa.
Pia, Manchester United na Tottenham, ambazo zote zinahangaika katika Ligi ya England, ziko katika robo fainali ya Ligi ya Ulaya na ikiwa mmoja wao atashinda kombe hilo itakuwa timu nyingine kutoka England inayoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.















