Ijue historia ya Ligi Kuu ya England

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aubameyang na Harry Kane
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Msimu mpya wa 2024/25 wa Ligi Kuu ya England umeng’oa nanga wiki iliyopita. Timu 20 zinawania kuchukua taji la ligi hiyo. Mwisho wa msimu timu tatu zitashuka daraja na nyingine tatu zitapanda.

Soka ya kisasa ilianzia Uingereza katika karne ya 19. Michezo ilikuwa ikichezwa katika miji na vijiji kulingana na kanuni na sheria za eneo husika. Na sasa soka linachezwa duniani kote kwa kanuni na sheria zinazofanana katika kila nchi.

Licha ya soka kuwa mchezo mkubwa kwa sasa, hapo awali ukuaji wa soka nchini Uingereza ulitatizika kutokana na ukuaji wa viwanda na miji, na kupunguza kiwango cha muda na nafasi ya kucheza, pamoja na historia ya marufuku kutokana na vurugu zilizokuwa zikitokea.

Turudi katika ligi ya sasa ya England: Manchester City ndiye bingwa mtetezi kwa sasa. Timu hiyo imeshachukua mataji nane na manne kati ya hayo, imeshinda mfululizo – kati ya msimu wa 2020/21-2023/24. Toka msimu wa 2017/18 City imegeuka kuwa mashine ya kufyatua makombe chini ya Muhispania, Pep Guardiola.

Kawaida ya msimu wa ligi kuu huanza mwezi wa August na kumaliza Mei, na mechi nyingi huchezwa mwishoni mwa wiki. Vilabu 51 vimeshashiriki katika ligi hiyo tangu kuanzishwa kwake 1992. 49 kutoka England na viwili kutoka Wales.

Timu nne zinazoongoza kwa pointi kila mwaka hufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya (UEFA), ambayo inazikutanisha timu za juu kutoka ligi za Ulaya na kuwania taji la kila mwaka la klabu bora Ulaya.

Pia unaweza kusoma

Mafanikio ya EPL

poo

Chanzo cha picha, ICON SPORT

Maelezo ya picha, Mashabiki wa ligi kuu ya England

Hii ndio ligi yenye kutazamwa zaidi duniani, ikikadiriwa kila mechi hutazamwa na watu milioni 643 kupitia runinga. Na siku za mwisho wa wiki timu zinapokutana, viwanja hujaa mashabiki.

Fauka ya hilo, ndio ligi tajiri zaidi. Kwa lugha nyingine, ndio ligi yenye pesa nyingi. Mikataba ya televisheni na wadhamini yamepandisha mapato kwa ligi na vilabu. Mechi zinaonyeshwa katika zaidi ya nchi 180.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kupanda kwa thamani ya Ligi Kuu ya England kulifanya timu kuwa tajiri na wachezaji wa kigeni na mameneja kuagizwa kutoka nje kwa kiwango kikubwa hadi sasa.

Wakati inaanza kulikuwa na wachezaji 11 tu wasiokuwa Waingereza au kutoka Irish. Lakini msimu uliopita pekee, kulikuwa na wachezaji wa kigeni kutoka mataifa sitini na nane, na hadi sasa wachezaji kutoka mataifa 123 wameshacheza.

Mwanzoni ligi hiyo ilikuwa na vilabu 22, lakini baada ya msimu wa 1994/95 kumaliza, ndipo utaratibu wa kuwa na vilabu 20 ukaanza ambao ndio upo hadi sasa.

Mchambuzi wa michezo kutoka Italy, Gab Marcotti anasema, “mafaniko ya EPL yanatokana na mambo mengi, urithi kwamba mchezo wa soka ulivumbuliwa Uingereza, lugha ya Kiingereza ambayo imeenea ulimwenguni na mazingira yanayounga mkono biashara ambayo hurahisisha uwekezaji wa kigeni.”

Marcotti pia anaongeza, “uongozi thabiti, ukubwa wa soko lake, utayari wa kukumbatia utaalamu kutoka nje ya nchi wakiwemo wachezaji, makocha, wamiliki na watendaji pia na soko la ndani ambalo liko tayari kutumia pesa kwa ajili ya vilabu vyao.”

Watu wenye historia kubwa EPL

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alan Shearer

Mwingereza Alan Shearer ndiye mfungaji mwenye magoli mengi, 260 tangu kuanza kwa ligi. Alichezea vilabu vya Blackburn Rovers na Newscatle United na kustaafu 2006.

Wafungaji wengine mashuhuri wenye magoli mengi ni Harry Kane 213, Wayne Rooney 208, Andrew Cole 187, Sergio Agüero 184, Frank Lampard 177, Thierry Henry 175, Robbie Fowler 163, Jermain Defoe 162 na Mohamed Salah 159.

Mwamuzi wa kwanza mweusi kwenye Ligi Kuu ya Engaland alikuwa Uriah Rennie. Alisimamia zaidi ya mechi 300 za ligi kuu kati ya 1997 na 2008. Tarehe 26 Disemba 2023, Sam Allison akawa mwamuzi wa pili mweusi kuchukua jukumu la kuchezesha mechi za Ligi Kuu, akianza kuchezesha kati ya Sheffield United na Luton Town.

Sir Alex Ferguson, kocha mstaafu wa Man Unite ndiye kocha mwenye mafanikio zaidi. Aliteuliwa kuwa meneja wa Manchester United Novemba 1986. Makombe yote United yamepatikana chini ya ukufunzi wa mtaalamu huo na katika kmiaka yake 26 akiwa na United ameshinda mataji 38, yakiwemo 13 ya Ligi Kuu England.

Timu zenye mafanikio zaidi

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kikosi cha Manchester United mwaka 2011

Timu yenye mafanikio zaidi kwa wingi wa makombe ni Manchester United, imebeba ndoo mara 13. Makombe hayo yalipatika katika msimu wa 1992/93, 1993/94, 1995/96, 1996/97, 1998/99, 1999/00, 2000/01, 2002/03, 2006/07, 2007/08, 2008/09, 2010/11 na 2012/13.

Kiwanja cha Old Trafford cha United ndicho kikubwa zaidi miongoni mwa viwanja vya vilabu vya Ligi Kuu England. Kiwanja hicho kina uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 70,000.

Kuna vilabu saba tu ndivyo vimeshinda mataji toka 92, Manchester United mataji 13, Manchester City 8, Chelsea 5, Arsenal 3, Blackburn Rovers 1, Leicester City 1 na Liverpool 1.

Na vilabu sita ndivyo vimecheza misimu yote tangu ligi kuanza: Arsenal, Chelsea, Everton, Liverpool, Manchester United na Tottenham Hotspur.

Ligi inapoanza kila timu hukutana mara mbili (nyumbani na ugenini) katika msimu. Michezo 380 huchezwa kwa jumla. Alama nyingi za timu katika msimu mmoja ilikuwa ni pointi 100, zilizokusanywa na Manchester City katika msimu wa 2017-18.

Msimu wa 2003/04 uliingia katika historia kwa Arsenal, ambao walicheza msimu mzima wa ligi bila kufungwa, na kushinda mara 26 na sare 12, na kushinda taji hilo kwa tofauti ya pointi 11 mbele ya Chelsea. Wakati huo timu ikiwa chini ya Arsene Wenger.

Pia unaweza kusoma

Imehaririwa na Seif Abdalla