Waridi wa BBC:Mwanamke aliyeonesha ukakamavu kwa kuwa nahodha wa Feri

- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Huyu ni mwanamke ambaye amevalia koti la ujasiri na kuwa nahodha pekee wa kike katika kivuko huko pwani ya Kenya.
Amefahamika sana na jina lake kuvuma miongoni mwa wasafiri wa kila siku wanaotumia feri zinazounganisha Likoni na kisiwa cha Mombasa.
Mishi Iddi Omar anasema alihitaji ukakamavu mkubwa kuanza kazi hii.
''Kwa kweli imehitaji ukakamavu mwingi kujiamini , kuwekeza katika masomo na kutoa muda wangu mwingi kufanya kazi hii.
Nina furaha kwamba ndoto yangu ya kuwa nahodha wa feri ilitimia , sasa nadhani kwamba naweza kuwa nahodha wa meli kubwa ambazo tunapishana nazo baharini '' anasema Mishi .
Kikosi cha BBC kilichoshuhudia safari zake ndani ya feri kubwa zaidi kwenye kivuko hicho ikifahamika kama MV.Safari na kwa mara zaidi ya nane tulikuwa kwenye chumba maalum kilicho juu zaidi cha manahodha wa feri hizo kushuhudia kinachowafanya watu kumshabikia mwanadada huyu .
Kawaida ya siku nyingine zote utamkuta amevalia sare za kazi shati jeupe na suruali ya Samawati -sare rasmi za nahodha ambazo huandama na kofia ,pale juu Bi.Mishi anachukua usukani wa feri , chumba hicho kimezingirwa na vioo pande zote akiwa katikati ya maji anakuwa kwenye usukani kuhakikisha kuwa wote walio ndani wamevuka salama
Siku aliyojutia unahodha

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanamke huyu alisimulia kisa kiliochofanyika miaka miwili baada ya kuajiriwa kazi katika Shirika la Feri nchini ambapo alianza safari kutoka ng'ambo ya Mombasa akielekeza abiria na magari hadi Likoni .
Ghafla akiwa katikati mwa bahari sehemu ambayo ina kina kirefu chini ya chombo alichokuwa nahodha kilipoteza mitambo yake ya pande zote mbili.
Kilichofuata ni chombo kuanza kuvutwa na maji na upepo wa baharini , anasema kwamba hakuwa na la kufanya ila kutizama feri ikibebwa hadi umbali wa mitaa kadhaa kutoka sehemu maalum ya kuvukisha mizigo.
''Ninakumbuka siku hio nilijawa na hofu mno , kilichozidisha hofu ni kuwa watu walinifokea sana wakisema kwamba nilishindwa kudhibiti feri kwa wakati .
Nilidhalilika hata zaidi kutokana na kuwa mimi ni mwanamke na waliokuwa wananifokea kwa sauti walikuwa wanasema kwamba kama mwanamke ninafaa jikoni wala sio kujaribu sarakasi na chombo ambacho kinafaa kuwa mikononi mwa wanaume , nilihisi vibaya mno nusura nikate tamaa.''Mishi anakumbuka
Mwanadada huyo anasema kwamba alirejea nyumbani akihisi kama aliyefeli , wakati huo alizungumza na wakuu wake akitaka aondoshwe kwenye zamu za manahodha , lakini anasema kwamba wakuu wake hawaku tayari aondoke , anasema kwamba walimtia moyo kuwa kwenye bahari kuu mambo hugeuka kwa kasi mno na wakati mwengine changamoto za chombo kuwa na hitilafu za kimitambo hutokea bila kuzingatia kama ni nahodha mwanamume au mwanamke aliyekuwa anadhibiti feri.
Mwanamke huyu anasema alipata umakinifu na pia ukakamavu wa kukabiliana na hali zote katika maji makuu , na hata wakati chombo kinakuwa kwenye hatari ya kupoteza mwelekeo sasa ametambua mawili matatu ambayo anaweza kuyafanya .
Kulingana na shirika la feri nchini kwa sasa kuna manahodha 20 ambao ni wafanyikazi rasmi katika kivukio cha likoni , Mishi Iddi ndio mwanamke pekee katia ya wanaume 19, ila hilo halijamkatisha tamaa ya kuboresha unahodha wake hata zaidi .
Mishi anasema kwamba changamoto ya unyanyapaa ilikuwepo hapo awali , kuna wakati feri zilizokuweko nahodha alikuwa anakaa sehemu ambayo angeonwa na kila abiria kwani sehemu ya kuendesha chombo hicho ilikuwa haijafunikwa , kwa hio wakosoaji wake , na baadhi ya abiria ambao walihisi kuwa mwanamke kwa jinsia yake hawezi walimfokea na kumuita majina mengi , ila kwa sasa meli hizo zinasehemu maalum ya nahodha kuwa faraghani na kutathmini bahari na barababara yake taratibu.
“Kwa Sasa huwa hawajui ni nani nahodha , hasa kwenye meli hii nilipo leo ya MV Safari , hadi nizingumze hakuna abiria anayefahamu ni nani aliyeshika chombo hiki , hata Sasa nenda ukaulize hawajui na nadhani ni vyema ikiwa hivyo “ alisema Mishi
Safari ya kuwa nahodha

Mishi alieleza kuwa kwa miaka 12 kabla ya kuwa nahodha wa feri alitumika kama mfanyakazi wa kuegesha magari yanayovuka feri kuhakikisha kuwa yamepangwa kwa ustadi na mwelekeo uliyofaa , ila anasema kwamba kila wakati alitamani na kuwa na ndoto ya kwamba siku moja atahama kutoka afisa wa kuegesha magari na kuwa nahodha .
Mama huyu aliamua kusomea unahodha kwenye chuo cha bandari Mombasa kwa mwaka mmoja na kuchukua mazoezi ambayo yalimsaidia kujenga misuli ya uwezo wake wa kuwa kama manahodha wengine , anasema kuwa kutokana na njaa na ari ya kutaka kuwa bora kama nahodha ilikuweka kwenye nafasi ya ushindani hata kwa wafanyikazi wenzake wanaume .
“ Kazi hii inaweza ikawa rahisi au ngumu kulingana na matayarisho ambayo mtu binafsi anafanya , nimejitolea kuelewa feri na bahari sana , naipenda kazi yangu sana na najivunia kuwa nahodha nchini “
Mishi ni mama wa watoto watatu na pia ni mke, majukumu ya nyumbani ameyatenganisha na majukumu ya kuwa usukani wakati anaitwa nahodha wa ferry na anapovua vazi hili anayachukulia majukumu ya kuwa mama na mke kwa ustadi ule ule wa utaratibu kwenye kivukio cha likoni
Mishi Iddi alizaliwa eneo la Likoni , akapata masomo yake huko huko likoni Mombasa na cha ajabu kwa sasa yeye anaishi likoni na kwenye kivukio hicho cha likoni ndiko riziki yake ilipo .
Pamoja na vigezo vengine vya kuwa nahodha , Bado anaendelea kuwa bora hata zaidi, pale baharini yeye hupishana na meli kubwa zinazotoka nchi mbalimbali duniani, na matamanio yake ya siku za usoni ni siku moja kuwa Nahodha wa meli kubwa zinazoendeshwa kimataifa.












