WARIDI WA BBC : 'Sikulala usingizi kwa miezi sita mfululizo'

Annabelle Nduta

Chanzo cha picha, Annabelle Nduta

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Annabelle Nduta anakumbuka jinsi soni au kuona haya kulivyomkumba kwa muda mrefu tangu utotoni, kutokana na mahangaiko ya ugonjwa wa akili ambao uligundulika baadaye maishani mwake.

Mwanamke huyu anasema kwa muda mrefu aliogopa kuzungumza yake mbele za watu kwa kujiona kama ambaye hakuwa sawa , wakati mwingine kuongea sana au kuzungumza mambo ambayo sio uhalisia wa kawaida wa watu , ila miaka mingi baadaye amekubali kwamba anaishi na ugonjwa wa kiakili .

Annabelle ni mwanamke wa miaka 30 na mama wa mtoto mmoja kutoka nchini Kenya , ni mama ambaye ameishi na ugonjwa wa akili ambao huathiri umakini wa mtu katika kutekeleza majukumu ya kila siku kwa utaratibu hadi mwisho wake , hali hii inafahamika kama Attention deficyt neurodevelopment disoders of childhood (ADHD).

Alivyoanza kupoteza usingizi

Mwanadada huyu anasema kwamba hali hii ilianza kumuathiri akiwa binti wa miaka tisa , watu wazima waliokuwa karibu na yeye wallikuwa wanamueleza kwamba hakuwa na umakini wa kutosha katika kutekeleza jambo lolote kwani alijipata akiwa katika shughuli tofauti kwa wakati mmoja na asiweze kukamilisha kwa ubora wake , hilo lilipelekea yeye kuwa mtoto wa kusahau kwa haraka.

''Hadi nilipoanza kuwa na ufahamu , nakumbuka nikiwa mtoto ambaye hakuwa anatulia kimawazo , nikiwa darasani waalimu walikuwa wananikumbusha kuwa makini kwani ilikuwa wazi kwamba akili yangu haikuwa kwenye shughuli zilizokuwa zinaendelea sehemu nilipokuwa ”anakumbuka Nduta.

 Mwanamke huyu anasema kwamba ni jambo ambalo liliathiri masomo yake sana , kutokana na kwamba akili yake haikuwa na uwezo wa kutulia kwa muda matokeo ya mitihani aliyokuwa anaifanya ilikuwa inayumba wakati mmoja alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wanafanya vizuri sana katika matokeo yao na wakati mwingine alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wako chini sana.

Annabelle Nduta

Chanzo cha picha, Annabelle Nduta

''Nilikuwa ni mtoto wa kusahau sana , na wakati mwingine wazazi wangu walikuwa wananiadhibu sana , kwa mfano nilikuwa nikitummwa jikoni kuchukua sahani , nami ninasahau na kupeleka kijiko kwa hiyo nilikuwa nasahau mno nilikuwa nahisi ninashinikizo kubwa sana hivyo basi kujiona kama ambaye sikufaa ” anakumbuka Nduta.

''Wakati mwingine wanafunzi wakiandika insha kuhusu jinsi walivyotembelea mbuga ya wanyama , na kuwaona wanyama wa aina mbalimbali , mimi nilikuwa ninaandika kwa mfano jinsi nilivyomuona simba ambaye alikata ua na kuanza kufukuza , kisha baadaye tukakutana na mnyama mmoja mdogo tukamtupia huyo Simba , kwa hiyo mawazo yangu yalikuwa ya ajabu sana na yalitengana na hali halisi ”anakumbuka Nduta.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ila anasema kwamba pindi miaka ilipoendelea kusonga hali hiyo ya kiakili iliendelea kuwa sugu na hakuna yeyote aliyegundua kwamba kulikuwa na kasoro yeyote , wazazi wake pamoja na walimu walimhimiza kuwa bora zaidi na kuacha kuwa na ‘ndoto za mchana’ kwa kifupi mawazo yake yalikuwa mengi na tofauti .

Alipogundua kwamba hali yake ilikuwa inawashangaza watu waliokuwa karibu naye , alianza kujitenga na watu , kuwa mkimya na pia kuficha mengi aliyokuwa anapitia , kitu kilichompa sonona ya utotoni . Kwa hivyo kwake shule ilikuwa kama gereza ama sehemu ambayo alihisi kana kwamba uhalisia wake haukuwa unakubalika kama kitu cha kawaida .

Hata baada ya kukamilisha shule ya upili bado alipitia mahangaiko mengi sana ya hali ya kwamba hakuna aliyefahamu ni kipi kilichokuwa kinatendeka katika akili yake .

Kipindi alichokamilisha shule ya upili ndipo hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi kwa miezi sita alikosa kupata usingizi kama watu wengine , kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kwake , anakumbuka akigeukia vileo pamoja na mihadarati kama njia ambayo alidhani ingemsaidia kulała.

Ila anasema kwamba alikuwa tu analala kwa saa mbili kisha anarudi palepale ambapo hakupata usingizi.

Annabelle Nduta

Chanzo cha picha, Annabelle Nduta

Baada ya miezi hiyo sita ya kukosa usingizi mwanamke huyu anasema kwamba siku moja akiwa jijini Nairobi baada ya shughuli za siku, akiwa anatembea barabarani alihisi kana kwamba alikuwa anaona giza kila upande alihisi kana kwamba aliishiwa na nguvu.

Wakati huo aliamua kumpigia swahiba wake ambaye aliandamana na mama yake na akaanza kwa kupewa huduma ya kwanza .Tukio hilo lilikuwa mwanzo wa harakati za kutafuta tiba ya kilichokuwa kinasababisha tabia zake za kipekee .

Kilichofuata ni dada huyu kupelekwa katika kituo maalum cha wagonjwa wa akili , alipoishi kwa wiki mbili na nusu , aidha anasema kwamba kipindi hicho wataalamu walitumia muda kufuatilia matendo yake ya kila siku ili kutambua ni ugonjwa upi aliokuwa nao .

Madaktari wa afya ya akili walimueleza kuwa alikuwa anaugua ugonjwa wa akili ujulikanao kwa kitaalamu kama Attention deficit hyperactivity disorder (ADHD).

Annabelle Nduta

Chanzo cha picha, Annabelle Nduta

Wataalamu walimueleza kwamba hali hii ilimfanya awe mtoto na hatimaye mtu mzima ambaye alikuwa hatulii na hana nguvu ya kuwa makini. Ilikuwa rahisi kwake kuanza matibabu kwani kiini cha tabia zake kilikuwa kimeeleweka.

Mwanzo Nduta anasema kwamba alipewa dawa za kukabiliana na hali , ila baada ya miaka miwili alianza matibabu mengine yanayohusu kutenga muda kutafakari kama njia ya kufundisha mawazo yake juu ya kuwa na mawazo chanya na wakati mawazo hasi yanapo kuja jinsi ya kukabiliana na hali hiyo

Vilevile matibabu hayo yalimsaidia kuwa na uwezo wa kupata umakini wa kufanya jambo moja hadi mwisho.

Akiwa sasa na miaka 30 angali anaishi na hali hiyo ila tofauti na hapo awali amepata mikakati ya jinsi ya kuishi na hali hiyo kwa kuongeza mazoezi, vilevile kuhakikisha kuwa anakula vyakula ambavyo vitamsaidia kupunguza msongo wa hisia au wingi wa homoni zinaoongeza uwezekano wa ugonjwa alionao wa kiakili kuwa juu.

ADHD ni ugonjwa gani?

Wataalamu wa afya ya akili wanasema kwamba ADHD ni mojawapo ya matatizo ya kawaida ya ukuaji wa akili wakati wa utotoni.

Kawaida hugunduliwa katika utoto na mara nyingi hudumu hadi utu uzima.

Watoto walio na hali ya ADHD wanaweza kuwa na shida ya kuzingatia, kudhibiti tabia kwa mfano wanaweza kutenda bila kufikiria matokeo yatakuwa nini, au kuwa na bidii kupita kiasi.

Vile vile watoto wenye matatizo ya hali hii huwa na shida ya kuzingatia kitu kimoja kwa muda mrefu na tabia wakati mmoja au mwingine. Hali hii husababisha wanaoathiriwa kusababisha ugumu shuleni, nyumbani, au na marafiki.

Mtoto aliye na ADHD anaweza kuwa na ndoto za mchana sana kumaanisha anakuwa yuko kwenye ulimwengu wake , kusahau au kupoteza mambo mengi , mikono yake haitulii , kuongea sana, kufanya makosa na kutojali au kujiingiza hatari pia kuwa na ugumu wa kushirikiana na wengine