Waridi wa BBC: 'Wanakijiji Walitamani nife kwa kuwa mlemavu'

W

Chanzo cha picha, ANNE WAFULA

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Anne Wafula Strike, anatoa mfano wa ujasiri, kujitolea na dhamira ambayo ni imara na ambayo imekataa kuishi na maoni potofu kuhusu hali yake ya ulemavu wa kutoka kiuno chake hadi miguuni .

Anne ni mama, mwanariadha, mwandishi, na balozi wa michezo ya magurudumu .

Anne anahimiza mafanikio na ubora katika anuwai ya hali ya maisha kupitia mazungumzo ya kutia moyo na kutetea haki za walemavu anahimiza wengine wanaoishi na ulemavu pia kuwa bora zaidi kuliko wanavyoonekana .

Anne strike Wafula alizaliwa mnamo Mei 8, 1969 katika kijiji kidogo kinachoitwa Mihuu Magharibi mwa Kenya. Alikuwa mtoto mwenye nguvu ambaye aliishi kulingana na jina lake la katikati (strike)lenye kumanisha nguvu lakini akiwa na umri wa miaka miwili tu, alikuwa tayari amepata pigo la ugonjwa wa kupooza wa polio.

Maelezo ya video, Waridi wa BBC: Je Anne Strike ni nani?

Alikua amepooza kutoka kiunoni kwenda chini hadi miguuni mwake. wengi ni wale katika kijiji chake ambao hawakuelewa ugonjwa huo na kulingana na mwanadada huyu wengi walidhania kuwa alikuwa muathiriwa wa ushirikina na uchawi.

"Unajua kila mara watu wanakosa kuelewa jambo, huwa wanaanza kuweka fikira yao ambayo wakati mwengine sio chanya , kwa hio nilipoanza kuugua na nikawa kilema ,baadhi ya wanakijiji walizungumza mengi mabaya kuhusu hali yangu ,kunyanyapaliwa kwangu kulianza ningali mdogo"anasema Anne

Aidha mwanamke huyu anasema kwamba wanakijiji walimtaja kama mtoto aliye laaniwa na kumtaja kama "nyoka " - hii ni kutokana na kuwa alikuwa anatambaa kwa tumbo alipokuwa anahitaji kusonga eneo moja hadi nyengine wengi walikuwa wanaona afadhali afe.

Familia yake ililazimika kukimbia kutoka kijijini walichokuwa wanaishi kwa usalama wa binti yao . Kuanzia hapo Anne alipelekwa shule maalum ya walemavu iliyokuwa mbali na nyumbani kwao.

Tukio la huzuni lilifanyika , wakati tu Anne alihitaji sana, mama yake , mama alifariki dunia ghafla akimuacha baba yake atunze watoto nane peke yake.

w

Chanzo cha picha, ANNE WAFULA

Maelezo ya picha, Anne akiwa na baba yake mzazi

"Mtu ambaye sitawahi kumsahau maishani mangu na ambaye nina muenzi sana ni baba yangu mzazi, alipambana sana na mimi wakati ambapo baadhi ya watu walikuwa wananiona sifai kuishi .

Baba alinipambania hadi akahakikisha nimejielewa na kujijua, ninampenda sana baba yangu sana "anasema Anne

Walakini, licha ya kuachwa na kutengwa na wengi, Anne aliendelea kupata matokeo mazuri ya masomo.

Mwanadada huyu alikuwa mtoto wa kwanza wa familia yake kwenda Chuo Kikuu ambapo alisomea taaluma ya ualimu.

Alifanikiwa kuwa mwalimu na ni wakati huo alikutana na barafu yake ya moyo mwanamume mwenye asili ya uingereza . walifunga ndoa na Anne kuanza maisha mapya nchini Uingereza

Maisha nchini Uingereza

Huko England, Anne alikaidi kile wataalam wa matibabu walikuwa wamesema hakiwezekani kwake kujifungua kama wanawake wengine kutokana na ulemavu wake. lakini Anne kwa ukaidi wake wa moyo alishika mimba na kujaaliwa mtoto wa kiume licha ya hali yake ya ulemavu.

baada ya kujifungua, alihisi kana kwamba kuna mengi ambayo anaweza kuyafanya maishani licha ya kuwa mke na mama.

Alifahamu kuwa angeyaweza mengi kuyafanya maisha yake kuwa bora zaidi. ni wakati huo baada ya kumlea mtoto Anne alitafuta njia ya kupoteza uzito wa mwili na kujikwaa Kenya mbio za magurudumu ya watu wenye ulemavu.

Alibadilika na kuwa gwiji katika mchezo huo na muda mfupi baada ya kuuchukua, alishindania mchezo wa magurudumu wa walemavu Athene 2004 na kuwa mwanariadha wa kwanza wa magurudumu kutoka Afrika Mashariki kushindana kwenye mchezo wa Paralympics.

W

Chanzo cha picha, ANNE WAFULA

Kuanzia hapo Anne - aliendelea kushinda medali ya shaba kwenye Kombe la Dunia la Paralympic la 2007 BT huko Manchester Uingereza.

Ushindi wake katika mchezo huo ulimuwania safari ya kwenda kasri ya Buckingham kukutana na Malkia Elizabeth na katika kile kinachoonekana kuwa hatua ya kwanza tu katika nyota yake kung'aa. Anne alianza kuwakilisha uingereza katika michezo mbali mbali ya magurudumu.

Na je anazungumziaje hatua yake ya kuwakilisha uingereza badala ya nchi yake Kenya?

"Lakini uamuzi wa kutoka Kenya kwenda Uingereza haukuwa rahisi. Mwishowe, nilifanya hivyo ili niweze kukaa na familia yangu huko uingereza.

Ninampenda sana mume wangu na mtoto wangu na wananipenda sana. Kwangu kuwa uingereza kunaniruhusu kuwa karibu nao kila wakati. Kenya ilielewa kuwa kuhama kwangu kulikuwa kwa sababu za kifamilia na waliiunga mkono hilo. Ninaikumbuka familia yangu ya Kenya na baba yangu lakini najua kuwa wanajivunia nilipoafikia sasa na Nimefurahi sana kuwakilisha Uingereza". Anne alisema

Kisa cha kutamausha

"Mwanamichezo mwenye ulemavu wa miguu amelipwa fidia baada ya kujiendea haja ndogo kwenye gari moshi wakati choo cha walemavu kilikuwa hakifanyi kazi".

Hii ni baadhi ya nukuu mmoja katika vyombo vya habari vilivyoangazia tukio hilo na kulichapisha kwenye baadhi yamajarida uingereza . Hii ni kuhusu mwanamke huyu mshupavu - Anne Wafula-Strike, wakati huo alikuwa kwenye treni ya mida ya saa tatu kutoka mji wa Nuneaton hadi Stansted Uingereza , ni wakati akiwa kwenye treni aligundua kuwa choo cha walemavu kilikuwa hakifanyikazi , na hapo hakuwa na budi ila kujiendea haja ndogo.

Ni kisa ambacho shirika hilo la mashindano kilichokuwa kinahusika na usafiri wa treni hio walikubali na kumfidia kwa kosa katika upande wao. Ni visa kama hivi ambavyo Anne anadokeza kuwa humfanya kusukuma haki za walemavu .

Anne strike alitaja kisa hicho kama "kilichomdhalilisha mno "

Japo ni tukio lililoshughulikiwa hadharani ana amini matukio kama haya yanafanya watu wenye maumbile ya kawaida kuheshimu na kufikiria zaidi kuhusu shida na changamoo za walemavu kijumla.

Kwa hio kutengeneza miundo mbinu ambayo itarahisisha maisha ya walemavu sehemu yoyote walipo

w

Chanzo cha picha, ANNE WAFULA

Uandishi wa kitabu chake

Kitabu chake kwa jina "In My Dreams

Ni kitabu ambacho mwanamke huyu aliandika akiwa anadhamiria kuzungumzia safari ya maisha yake tangu alipozaliwa, ili kutoa mwanga na matumaini hasa kwa watu wanaoishi na ulemavu mmoja au mwengine.

"Ni kweli kitabu hiki kinasimulia juu ya maisha yangu, ni kitabu ambacho kinaibua hisia tofauti za huzuni za kero na hatimaye za ushindi" anasema Anne .

Mwanamke huyu anasema kuwa kitabu hiki ni zawadi yake kwa ulimwengu na kwa vizazi vijavyo kufahamu kuwa wakati mwengine huchagui matukio ya maisha lakini unachagua jinsi ya kukabiliana na matukio hayo .