Vita vya Ukraine: Marekani yasema Iran sasa ndio 'msaidizi mkuu wa kijeshi' wa Urusi

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ukraine imeishutumu Iran kwa kutuma ndege zisizo na rubani nchini Urusi, jambo ambalo nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ilikanusha kisha ikakubali baadaye

Uhusiano wa Russia na Iran umeongezeka hadi kufikia ushirikiano kamili wa ulinzi, Marekani imesema.

Urusi inatoa msaada wa kijeshi ambao haujawahi kushuhudiwa, alisema msemaji wa baraza la usalama la taifa la Marekani John Kirby.

Marekani imeona ripoti kwamba nchi hizo mbili zinazingatia uzalishaji wa pamoja wa ndege zisizo na rubani hatari, aliongeza.

Australia imetangaza kuwawekea vikwazo Wairani watatu na biashara moja ya Iran kwa kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani za kutumia dhidi ya Ukraine.

Ushirikiano kati ya Urusi na Iran umeangaziwa hivi majuzi, huku Ukraine ikiishutumu Urusi kwa kutumia ndege zisizo na rubani za Iran katika mashambulizi yake.

Baada ya awali kukanusha kutuma ndege zozote zisizo na rubani nchini Urusi, nchi hiyo ya Mashariki ya Kati baadaye ilikiri kuwa ilikuwa imetoa baadhi ya ndege hizo kabla ya uvamizi wa Ukraine.

Bw Kirby alisema kuwa ushirikiano kati ya Iran na Urusi katika kuzalisha ndege zisizo na rubani utakuwa na madhara kwa Ukraine, majirani wa Iran na jumuiya ya kimataifa.

"Urusi inataka kushirikiana na Iran katika maeneo kama vile utengenezaji wa silaha, mafunzo," alisema, akiongeza kuwa Marekani inahofia kwamba Urusi ilikusudia "kuipa Iran silaha za hali ya juu za kijeshi" ikiwa ni pamoja na helikopta na mifumo ya ulinzi wa anga.

"Iran imekuwa mfadhili mkuu wa kijeshi wa Urusi..." alisema.

"Urusi imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani za Irani kugonga miundombinu ya nishati, na kuwanyima mamilioni ya Waukraine nguvu, joto, huduma muhimu. Watu wa Ukraine leo wanakufa kutokana na hatua za Iran."

Akijibu maoni ya Bw Kirby, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema kuwa Iran imekuwa mojawapo ya waungaji mkono wakuu wa kijeshi wa Urusi na kwamba uhusiano kati yao unatishia usalama wa dunia.

"Mkataba huo mbaya" kati ya nchi hizo mbili umeshuhudia Iran ikituma mamia ya ndege zisizo na rubani nchini Urusi, alisema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na Rais wa Iran Ebrahim Raisi mwezi Julai

"Kama hatua ya kuonyesha ushirikiano, Urusi inatoa msaada wa kijeshi na kiufundi kwa serikali ya Iran, ambayo itaongeza hatari inayoleta kwa washirika wetu katika Mashariki ya Kati na kwa usalama wa kimataifa," aliongeza.

Alisema Uingereza ilikubaliana na Marekani kwamba uungaji mkono wa Iran kwa jeshi la Urusi utaongezeka katika miezi ijayo huku Urusi ikijaribu kumiliki silaha zaidi, ikiwa ni pamoja na mamia ya makombora ya masafa marefu.

Ukraine iliishutumu Iran kwa kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani za "kamikaze" zilizotumika katika mfululizo wa mashambulizi ambayo yaliua takriban watu wanane tarehe 17 Oktoba.

Baada ya kukana hilo, Iran baadaye ilikiri kutuma "idadi ndogo" ya ndege zisizo na rubani nchini Urusi, "miezi mingi" kabla ya vita vya Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema huu ni uwongo na kwamba Ukraine ilikuwa ikidungua takriban ndege 10 za Iran zisizo na rubani kwa siku.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vinaendelea kuathiri miji na maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na Bakhmut katika Donbas

Siku ya Jumamosi, Penny Wong, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia alisema katika taarifa yake: ‘’Usambazaji wa ndege zisizo na rubani kwa Urusi ni ushahidi wa jukumu la Iran katika kuyumbisha usalama wa kimataifa. Orodha hii inaangazia kwamba wale wanaotoa msaada wa mali kwa Urusi watakabiliwa na athari zake.’’

Pia alitangaza hatua kwa watu wengine 19 na vyombo viwili, ikiwa ni pamoja na Polisi ya Maadili ya Iran, kwa kuwatendea kikatili waandamanaji wanaoipinga serikali kufuatia kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 kizuizini mapema mwaka huu.