Mtu asiye na pasipoti, viza wala tiketi aliwezaje kusafiri kwa ndege hadi Marekani?

Chanzo cha picha, REUTERS
Mwanaume mmoja alifaulu kuondoka Uwanja wa Ndege wa Copenhagen, Denmark, kwenda Los Angeles, Marekani, bila pasipoti, viza wala tiketi ya ndege.
Mwanaume huyo aitwaye Sergei Uchigawa alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Los Angeles nchini Marekani Novemba mwaka jana. Bila ya hati yoyote.
Ijumaa iliyopita, mahakama ya jimbo la California nchini Marekani ilimpata na hatia ya kuingia Marekani kinyume cha sheria kwa ndege.
Novemba 4, maafisa wa Marekani walimkamata Sergei katika uwanja wa ndege wa Los Angeles na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitano.
Alifikaje Marekani?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kulingana na waendesha mashtaka, Sergei alifanikiwa kupita kisiri kwenye uwanja wa ndege wa Copenhagen, Denmark, kwa kumfuata abiria.
Na siku iliyofuata, Sergei alifanikiwa kupanda ndege ya Scandinavia Airlines hadi Los Angeles bila kutambuliwa.
Akiwa kwenye ndege wahudumu wa ndege waligundua alibadilisha viti mara kadhaa.
Wakati wa safari ya ndege, mwanaume huyo aliagiza chakula kutoka kwa mhudumu wa ndege mara mbili
Mmoja wa wahudumu wa ndege alisema Sergi alikuwa akijaribu kuzungumza na abiria wengine kwenye ndege wakati wa safari, lakini hakuna aliyejibu.
Alipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Los Angeles Novemba 4, alisimamishwa na maafisa wa Uhamiaji na maafisa wa Ulinzi wa Mipaka kwa ajili ya kuhojiwa.
Maafisa wa Uhamiaji na Ulinzi wa Mipaka waligundua mwanaume huyo hakuwa kwenye orodha ya abiria wa safari ya ndege kati ya Denmark na Marekani.
Uchunguzi ulibaini hakuwa na stakabadhi zozote kama vile pasipoti, viza ya Marekani au tiketi.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Wakati wa upekuzi, begi la Sergei lilikuwa na kadi za utambulisho alizopewa na Urusi na Israel.
Hakuwaambia maofisa wa usalama uraia wake wa kweli, wala hakueleza kwa nini alisafiri hadi Marekani, wala hakueleza kwanini alikuwa Copenhagen, Denmark.
Alishtakiwa kwa kutoa "habari za uwongo na za kupotosha" kuhusu safari yake ya Marekani.
Awali, aliwaambia maafisa wa uwanja wa ndege, alisahau hati yake ya kusafiria kwenye ndege. Aliwaambia pia maafisa kuwa ana tiketi ya ndege, lakini hakuna kitu kilichopatikana kwenye ndege.
Kadhalika, alisema hakumbuki jinsi alivyoingia kwenye ndege. Yuko gerezani tangu kukamatwa kwake na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitano. Hukumu rasmi ya mtu huyu inatarajiwa kutangazwa Februari 5.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












