Boeing 777X: Ndege kubwa zaidi duniani ya injini mbili yakamilisha safari ya kwanza

Boeing 777X

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ndege ndefu ya abiria imechelewa kutolewa kwa sababu ya matatizo ya kiufundi

Kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing imefanikiwa kukamilisha majaribio ya kwanza ya safari ya ndege kubwa zaidi duniani ya mfumo wa injini mbili, ifahamikayo kama 777X.

Hatua hiyo inakuja wakati ambao kampuni hiyo inajaribu kusafisha sura yake baada ya Ndege zake aina ya 737 Max kupigwa marufuku kupaa baada ya ajali mbili zilizoua watu 346.

Ndege hiyo ilipaa karibu na jiji la Seattle na kufanya safari ya saa nne angani.

Majaribio mawili yaliakhirishwa wiki hii kutokana na upepo mkali. Majaribio zaidi yanahitajika kabla ya ndege hiyo kuanza kazi na shirika la ndege la Emirates mwakani.

Ndege hiyo ya abiria yenye urefu wa futi 252 ilikuwa izinduliwe rasmi mwaka huu lakini hilo limeshindikana kutokana na changamoto za kiufundi.

777X ni ndege kubwa na yenye ufanisi zaidi katika familia ya ndege za Boeing aina ya 777.

Sehemu zenye mabadiliko katika ndege hiyo ni pamoja na ncha za mabawa zenye kujikunja na injini kubwa zaidi kwa ndege ya abiria.

"(Ndege hii) inawakilisha mambo makubwa tunayoweza kufanya kama kampuni (ya Boeing)," amesema mkurugenzi wa masoko wa 777X Bi Wendy Sowers.

Boeing inasema tayari ishafanya mauzo 309 ya ndege hiyo -gharama yake ikiwa ni zaidi ya dola milioni 442 kwa ndege moja.

Ndege hiyo itaingia kwenye ushindani mkali na ndege ya kampuni ya Airbus chapa A350-1000 ambayo hubeba abiria 360.

Boeing 777X

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Majaribio zaidi yanahitajika kabla ndege hiyo haijaanza kutumiwa na shirika la ndege la Emirates mwaka ujao

Boeing ipo kwenye wakati mgumu toka ilipotokea mikasa ya 737 Max, ambapo ndege mbili za chapa hiyo zilianguka ndani kipindi cha miezi mitano- ajali ya kwanza nchini Indonesia Oktoba 2018 kisha Ethiopia mwezi Machi mwaka jana.

Kampuni hiyo kwa sasa inakabiliwa na mlolongo wa uchunguzi dhidi ya tuhuma kuwa haikutilia maanani usalama kwa kuharakisha utolewaji wa ndege hizo kwa wateja.

Kwa sasa Boeing inahaha kupata kibali cha kurudisha ndege hizo angani.

Kupigwa marufuku kwa 737 Max, ambayo ndiyo ilikuwa kinara wa mauzo Boeing kunakisiwa kuisababishia kampuni hiyo hasara ya zaidi ya dola bilioni 9.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya sauti, Familia zaomboleza mkasa wa ajali ya ndege Ethiopia