Kwa nini ndege za kivita za Uingereza zililazimika kuielekeza uwanja mwengine ndege ya Kenya Airways?

Chanzo cha picha, AFP
Polisi wa Uingereza wamethibitisha kuwa ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Heathrow mjini London iliamriwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Stansted kaskazini-mashariki mwa London.
Ndege ya Kenya Airways KQ 100 ilielekezwa kutua katika uwanja mwengine wa ndege na ndege mbili za kijeshi za Uingereza za Raf Typhoon kwa sababu za usalama mchana wa Oktoba 12.
Sababu ya hatua hiyo ilisemekana kuwa tishio la usalama, huku vyombo vya habari vya ndani vikiripoti kuwa vikosi vya mabomu vilionekana kukimbilia huko.
"Kwa sasa tunakabiliana na hali katika Uwanja wa Ndege wa Stansted. Ndege kutoka Nairobi kuelekea Heathrow ilielekezwa Stansted mchana wa leo (Alhamisi 12 Oktoba). Uwanja bado uko wazi," ilisema taarifa iliyotumwa na Essex Police kwenye tovuti ya X.
Taarifa hiyo pia ilisema kulikuwa na tishio lililosababisha ndege hiyo kuelekezwa kinyume.
Jana usiku, Kenya Airways ilitoa taarifa ambayo haikuwa tofauti sana na hiyo.

Chanzo cha picha, PA Media
“Utawala wa KQ unaofanya kazi na maafisa wa usalama wa serikali ya Kenya na Uingereza umefanya tathmini ya kina kuhusu tishio hilo.
Wafanyakazi kwenye ndege wamearifiwa, na hatua zote zinazohusiana zimechukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu na abiria," ilisema sehemu ya taarifa iliyoandikwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ndege hiyo ilinaswa angani na ndege za kivita za Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) baada ya kufahamishwa mara moja. Inaaminika kuwa onyo lilitumwa wakati ikiruka juu ya anga ya Ufaransa.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi alisema: "Ndege za kivita kutoka kwa Jeshi la Wanahewa la Kifalme lililoko Coningsby zilitumwa kama tahadhari mchana wa leo kuchunguza ndege ya raia inayokaribia Uingereza".
"Ndege hiyo ya kiraia ilikuwa inawasiliana na wafanyakazi wa udhibiti wa usafiri wa anga nchini, na ilisindikizwa hadi Uwanja wa Ndege wa Stansted ambako ilitua salama."
Data ya Flightradar24, tovuti inayofuatilia usafiri wa anga wa kimataifa, pia ilisema kuwa Boeing 787-8 Dreamliner ilipaa kutoka Nairobi saa 09:18 asubuhi, baada ya kuchelewa kwa dakika 13.
Ndege hiyo ilikuwa ikiruka kwa mwendo wa futi 17,000 juu ya Uingereza kabla ya kushuka na kuelekea kaskazini kando ya pwani ya mashariki ya Kent.
Ndege hiyo iliendelea kuteremka kwenye ufuo wa Bahari ya Kaskazini na kisha Essex, na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Stansted saa 4:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
"Sote tulizingirwa na polisi. Wote walikuwa wamebeba bunduki, wamevalia mashati meusi, na walikuwa wakituomba kitambulisho. Nahodha hakusema lolote," alisema mwanamke mmoja kwenye ndege.
Siku ya Jumatatu kwa mujibu wa BBC Somali ndege nyingine ya shirika la ndege la Kenya Airways inayosafiri kati ya Nairobi na London Heathrow ilihitaji usaidizi wa dharura wa matibabu baada ya mmoja wa abiria hao kuugua, kulingana na kampuni hiyo.
"Wafanyikazi wa ndege hiyo wakisaidiwa na madaktari wawili na muuguzi mmoja, walimsaidia mgonjwa huyo kwa kutoa msaada wa matibabu, na nahodha akatangaza kuwa msaada wa haraka wa matibabu unahitajika wakati akizungumza na idara ya udhibiti wa ndege," taarifa ya kampuni hiyo ilisema.












