Safari ya siku 11 ya mpiga picha kuitoroka Sudan iliyokumbwa na vita

Mohamed Zakaria

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

    • Author, Barbara Plett Usher
    • Nafasi, Mwandishi BBC Africa

Mkesha wa safari hatari ya kutoroka nchini mwake mwezi uliopita, mwandishi wa habari wa Sudan Mohamed Zakaria aliacha vifaa vyake vya kazi kwa rafiki yake, bila uhakika kama angeviona tena.

Alikuwa akitoroka el-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Kaskazini la Darfur, ambalo linakabiliwa na makabiliano makali kati ya jeshi la Sudan na wanajeshi waasi wa Rapid Support Forces (RSF).

Mohamed alikuwa akishirikiana na BBC kuangazia eneo hili la vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 15. Lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, aliamua kutoroka.

RSF iliimarisha juhudi za kuuzingira mji wa El-Fasher mwezi Mei, ikilenga kituo cha mwisho cha jeshi huko Darfur.

Muda mfupi baadaye nyumba ya Mohamed ilishambuliwa kwa kombora, alipokuwa akijaribu kuwapeleka majirani waliojeruhiwa hospitalini. Watu watano waliuawa na 19 kujeruhiwa - Mohamed bado ana vipande vya mabaki ya kombora hilo mwilini mwake, huku kaka yake akipoteza jicho.

Gari

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Gari hii liliharibiwa wakati wa shambulizi dhidi ya nyumba ya Mohamed

Wiki mbili baadaye Mohamed aliwasaidia mama yake na kaka zake watatu kukimbilia usalama wao nchini Chad, jirani ya Sudan upande wa magharibi. Alibaki nyuma kuendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kujikimu kimaisha, anasema.

Lakini kadri wapiganaji wa RSF walivyoendelea kukaribia ndivyo, raia walinaswa katika eneo la vita la mashambulizi ya kiholela ya makombora na mashambulizi ya anga ya jeshi, huku usambazaji wa chakula ukikatizwa.

"Sikuweza kuenda kokote, sikuweza kufanya kazi," anasema. "Unachofanya sasa el-Fasher ni kukaa tu nyumbani kwako na kusubiri kifo ... baadhi ya wakazi walilazimika kuchimba mitaro kwenye nyumba zao."

Ilikuwa hatari kusalia mjini humo, lakini pia ni hatari kukimbia. Mwishowe aliamua kuelekea Sudan Kusini na hatimaye Uganda.

Alifikiri safari hii ingekuwa salama zaidi kwake kuliko kujaribu kuungana na familia yake nchini Chad, na ingemruhusu kufanya kazi mara tu atakapofika anakoenda.

Kutoka el-Fasher hadi Sudan Kusini, Mohamed alipitia vituo 22 vya ukaguzi, vitano vikiwa na jeshi na 17 na RSF.

Wakati mwingine alikabiliwa na maswali magumu, lakini alifanikiwa kuficha utambulisho wake kama mpiga picha ambaye aliwahi kuangazia taarifa za vita.

A vehicle with its bonnet up

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mohamed alibadilisha gari mara kadhaa kusafiri hadi Darfur ili kuelekea mpaka wa Sudan Kusini
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kituo cha kwanza walichofika, tarehe 10 Juni, kilikuwa kambi ya wakimbizi ya Zamzam viungani mwa mji wa El-Fasher.

Mohamed na msafiri mwenzake, binamu yake Muzamil, walikesha. Hapa alificha kamera yake na zana zingine za kazi.

Lakini alikuwa amebeba rekodi ya thamani ya picha na video zake - zilizohifadhiwa kwenye kadi za kumbukumbu - pamoja na kipakatalishi chake na simu.

"Tatizo kubwa nililokabiliana nalo barabarani lilikuwa jinsi ningeweza kuzificha," alisema.

“Kwa sababu hivi ni vifaa hatari. RSF au askari yeyote akikuona navyo, huwezi kueleza."

Katika mkondo wa kwanza wa safari, Mohamed alivificha vifaa vyake chini ya kanyagio la gari, bila kumwambia dereva.

Yeye na Muzamil walizuiliwa kwenye kizuizi kimoja na wanajeshi wa Sudan kwa kushukiwa kuelekea katika eneo la RSF kujiunga na adui. Lakini walifika mji ulioashiria mwisho wa udhibiti wa jeshi, bila tukio.

Hapa waliungana na wasafiri wengine - msafara wa magari sita kuelekea kijiji cha Khazan Jadid.

"Tulilipa askari wa RSF kwenda nasi," anasema Mohamed. "Ikiwa unataka kufika salama unahitaji kulipa RSF."

Madereva hao walikusanya pesa kutoka kwa abiria na kuzikabidhi kwenye kizuizi cha kwanza, ambapo mmoja wa wapiganaji wa RSF aliingia kwenye kila gari.

Wakati huu Muhammad alificha kadi zake za kumbukumbu kwenye karatasi ambayo aliiweka pamoja na nyaraka zingine.

Mtu akipumzika juu ya gari

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Watu waliokuwa safarini walipumzika popote pale walipoweza

Katika kituo cha basi huko Khazan Jadid, Mohammed alipata magari matatu pekee.

“Barabara ilikuwa hatari sana,” anasema, “na magari yote ya usafiri wa umma yalikuwa yamesitisha shughuli kabisa.”

Lakini walifanikiwa kupata moja ya kwenda katika jiji la el-Daein, mji mkuu wa Darfur Mashariki na walifika huko mapema alasiri ya 12 Juni.

Katika kituo cha ukaguzi katikati ya mji, wale wanaotoka el-Fasher waliwekwa upande mmoja, anasema Mohamed, kwa kushukiwa kuwa walifanya kazi na jeshi.

Hapa ndipo alipojipata matatani.

Alikuwa amefuta ujumbe, picha na programu zote kwenye simu yake ya rununu.

Lakini afisa huyo wa RSF alipata akaunti ya Facebook ambayo alikuwa amesahau kufuta, ikiwa kamili na machapisho aliyoshiriki kuhusu shambulio la bomu la El-Fasher na mateso wanayopitia wakazi wa jiji hilo.

Baada ya hapo kulifuata mahojiano kwa saa nyingi ambapo Mohamed alitenganishwa na Muzamil na kushutumiwa kuwa jasusi.

"Nilitishiwa kuteswa na kuuawa isipokuwa nifichue habari nilizokuwa nazo," asema.

“Nilihisi huo ulikuwa mwisho wangu. Ilikuwa ni hali mbaya sana. Kwa sababu kama alitaka kuniua, angeweza kufanya hivyo na hakuna mtu angejua. Nilihisi anaweza kuniua, kunipiga au kunifanyia chochote.”

Hatimaye Mohamed aliachiwa saa moja usiku baada ya kufanya mazungumzo ya malipo ya kiasi kikubwa cha pesa.

Wanaume wawili wakijaribu kutoroka Sudan

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mohamed na wenzake walikunywa maji ya mvua baada ya kukwamba msituni

"Huo ulikuwa wakati mbaya zaidi," anasema, akitafakari juu ya tukio hilo, "sio tu katika safari lakini nadhani wakati mbaya zaidi katika maisha yangu yote ... kwa sababu sikua na matumaini kabisa. Siamini nipo hapa.”

Mohamed alishuku aliyemhoji angetahadharisha kituo kingine cha ukaguzi barabarani ili kumkamata tena.

Yeye na Muzamil walikimbia hadi kituoni ili watoke nje ya mji haraka wawezavyo. Kulikuwa na gari moja tu, lori lilikuwa limejaa, lakini walifanikiwa kujipenyeza kwenye nafasi ndogo sehemu ya juu.

Walifika mpaka kwenye kijiji cha Abu Matariq, ambapo injini iliharibika na kuchukua siku mbili kurekebisha.

Baada ya kunusurika kukamatwa, Mohamed alikuwa na hamu ya kufika Sudan Kusini haraka iwezekanavyo. Badala yake, walisubiri kwa muda mrefu gari litengenezwe.

Wasafiri hatimaye waliondoka Abu Matariq tarehe 14 Juni wakielekea el-Raqabat, mji wa mwisho katika Darfur Mashariki kabla ya kufika mpakani. Njia ilipitia msitu wa el-Deim, eneo tambarare la nyasi na mchanga uliojaa miti yenye miba.

Watu wakisukuma gari

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mvua kubwa na matatizo ya kiufundi yaliyokumba gari lao ilifanya safari kuwa ndefu.

Mvua kubwa iliathiri safari yao, kwani gari la kubebea mizigo lilikwama kwenye matope.

"Ulikuwa mtihani mkubwa," anasema Mohamed.

"Tulikaa karibu siku sita bila maji ya kunywa na chakula. Tulitegemea zaidi maji ya mvua na tende.”

Kwa bahati nzuri, waliweza kununua kondoo wawili kutoka kwa wachungaji njiani.

Wakati wa safari, anasema Mohamed, hakupata shida ya chakula. Maeneo yanayodhibitiwa na RSF ambayo walipitia yalikuwa yameshuhudia ghasia mwanzaoni, lakini yalikuwa yametulia kidogo tangu wakati huo.

Masoko na mikahawa midogo ilikuwa ikifanya kazi. Chakula kilikuwa kinauzwa bei ghali, lakini si “ghali sana” kama ilivyokuwa huko el-Fasher, ambapo watu wengi walilazimika kuishi kwa mlo mmoja kwa siku.

People sleeping outside

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mohamed alichukua siku kadhaa kupita msitu wa el-Deim

Katika msitu huo, wanaume walilala popote, wakati mwingine kwenye mvua, wakati wanawake wawili na watoto wawili walilala ndani ya gari. Walichomwa na miiba miguuni mwao kwa kutembea bila viatu kwenye matope.

Hatimaye walisukuma gari la kubebea mizigo katika mazingira magumu. Lakini injini ilizima mara kwa sababu ya betri dhaifu. Na kisha ikaisha mafuta.

Kufikia hapa, wawili kati ya wanaume hao walienda kutafuta kijiji cha karibu. Ikawa ni mwendo wa saa tisa. Kwa faraja ya kila mtu walirudi mchana na mafuta ya ziada na gari lingine.

Kufika el-Raqabat, Mohamed na Muzamil walikuwa tu mwendo wa dakika 15 kutoka Sudan Kusini na usalama.

Lakini asubuhi iliyofuata kabla ya safari yao kuanza , walichukuliwa na kupelekwa katika ofisi kuu ya RSF na kuhojiwa kwa saa tatu.

Mtu mmoja alikuwa ameripoti kwamba watu wa jamii ya Zaghawa walikuwa wameingia mjini.

Zaghawa ni moja ya makundi yenye silaha yanayopigana pamoja na jeshi huko el-Fasher, na RSF inawachukulia kama maadui.

Mohamed alificha kadi zake za kumbukumbu, na vifaa vyake vingine na kumwambia afisa wa RSF kuwa yeye ni mhandisi wa kompyuta.

Kwa mara nyingine tena ililazimika kutoa malipo: dola 50 za Kimarekani kutoka kwa kila mtu. Mohamed na wanachama wengine wachache wa kikundi hicho walilipa ziada ili kumwachilia mtu mwingine ambaye alikuwa amekutwa na picha ya askari wa jeshi kwenye simu yake.

Kisha Mohamed na Muzamil wakapanda gari la kuanza safari ya kuelekea mpakani.

Mti wa Acacia

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mohamed hakuwasiliana wakati wa safari hiyo, kwa hiyo familia yake haikuwa na habari kama yuko hai.

Kuvuka hadi Sudan Kusini tarehe 20 Juni ilikuwa ni wakati "wa ajabu" kwa Mohamed.

"Nilipowaona wanaume wa Sudan Kusini, nilimshukuru Mungu na kusali," anasema. “Nilihisi niko hai. Kwa kweli sikuamini kwamba niko hai, kwamba niko hapa. Nilifika Sudan Kusini nikiwa na data zangu zote na kipakatalishi changu, ingawa nilikutana mara nyingi na RSF.”

Alimpigia simu mama yake mara tu alipoweza kununua kadi nyingine ya simu. “Hakuamini kwamba nilikuwa hai,” anasema.

Mohamed hakuwa mtandaoni kwa siku 11, na familia yake haikujua alikuwa wapi au nini kilikuwa kinamsibu wakati huo.

"Walikuwa na wasiwasi sana," anasema. "Wengi wao waliniambia ni hatari kusafiri barabara hiyo, usiende, huwezi kufika."

Lakini alikuwa amefanikiwa.

Alisimama katika mji wa Aweil nchini Sudan Kusini kwa siku chache, ambapo familia ya Zaghawa aliyokuwa akisafiri nayo ilimkaribisha nyumbani kwao.

Kisha akahamia mji mkuu wa Juba.

Muzamil aliamua kubaki huko, lakini Mohamed alisafiri hadi Uganda na kujiandikisha kama mkimbizi kwenye kambi iliyo karibu na mpaka kwa sababu pasipoti yake ilikuwa imeisha muda wa kutumia.

Watu wakitabasamu

Chanzo cha picha, Mohamed Zakaria

Maelezo ya picha, Mohamed (Kulia) na wasafiri wenzake walianza kutabasamu kwa furaha walipovuka mpaka na kuingia Sudan Kusini

Siku 23 baada ya kusafiri kutoka el-Fasher, Mohamed aliwasili katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, tarehe 3 Julai. Anaishi na mjomba wake.

"Kwa kweli sijui ni wapi maisha yatanipeleka kutoka hapa," anasema.

Kipaumbele chake kwa sasa ni kutunza familia yake na kujaribu kuunganisha tena jamaa zake. Kando na mama yake na kaka zake watatu nchini Chad, kuna kaka yake nchini Uturuki na dada yake nchini Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ndoto yake kwa siku zijazo ni kurejea Sudan katika nyakati za amani zaidi na kuanzisha chuo kikuu huko Darfur kufundisha uundaji wa filamu, upigaji picha na masomo ya vyombo vya habari.

"Kazi yangu haikuisha baada ya kuondoka el-Fasher," anasema. “Naamini hiyo ilikuwa ni awamu ya kwanza ya safari yangu ya maisha na sasa nimeanza tena kupanga awamu ya pili kwa kufanya kazi ili kuangazia ukweli wa hali ilivyo huko.

"Natumai kwamba juhudi zangu, hata kama kidogo, zitasaidia kufupisha muda wa vita na kuwaokoa watu huko El-Fasher."

Ramani

Maelezo zaidi kuhusu vita vya Sudan:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Seif Abdalla