Je Boris Johnson atafanikiwa kuingia tena kwenye kinyang’anyiro cha Waziri Mkuu mpya

Sunak and Johnson

Chanzo cha picha, Reuters

Boris Johnson na Rishi Sunak wamefanya mazungumzo huku wakikaribia siku ya mwisho ya kuteuliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya waziri mkuu kuchukua nafasi ya Liz Truss.

Vyanzo viwili tofauti viliiambia BBC mkutano huo ulifanyika, lakini hakuna kambi iliyofichua walichojadili.

Rishi Sunak anaendelea kusonga mbele katika kinyang’anyiro hicho, akipata uungwaji mkono wa wabunge 128 kutoka mirengo yote ya chama chake, wakiwemo washirika wa zamani wa Johnson.

Bw Johnson yuko katika nafasi ya pili akiwa na watu 53 wanaomuunga mkono, kulingana na ripoti ya BBC.

Hata hivyo kampeni yake inadai kuwa anaungwa mkono na wabunge 100 - idadi inayohitajika kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rishi Sunak amepata kuungwa mkono na wabunge 128, kwa mujibu wa ripoti ya BBC

Wafuasi wa Bw Sunak waliibua shaka juu ya hili na kumtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani aonyeshe uthibitisho.Penny Mordaunt ndiye mgombea pekee aliyetangaza rasmi kuwa yuko kwenye kinyanganyiro hicho, lakini anaungwa mkono na wabunge 23.

Mwandishi wa BBC Laura Kuenssberg alisema kuwa Bw Sunak na Bw Johnson walikutana Jumamosi jioni, lakini hakuwa na uhakika ‘’kama hitimisho lolote au habari zinaweza kutolewa usiku wa leo’’.

BBC imekuwa ikihifadhi jumla ya wabunge ambao wameingia kwenye rekodi kwa kuungwa mkono.

Nia ya kupiga kura ya wabunge 204 pekee kati ya 357 ya Conservative ndiyo inayojulikana kwa sasa na imethibitishwa na BBC, na kuwaacha wengi wakiwa bado hawatangaza nia yao.

Wanaotarajia wana hadi saa 14:00 BST siku ya Jumatatu kupata uugwaji mkono wa kutosha ili kuwawezesha kufuzu kwa hatua inayofuata.

Ikiwa wabunge wa chama watakubali kumuunga mkono mgombea mmoja tu, tunaweza kuwa na waziri mkuu mpya kufikia Jumatatu mchana.

Lakini ikiwa sivyo, basi itaenda kwa kura ya mtandaoni ya uanachama wa chama cha Conservative, na matokeo yatatangazwa Ijumaa.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Boris Johnson akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Gatwick baada ya likizo katika Visiwa vya Caribbean
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Siku nzima ya Jumamosi, wabunge walikuwa wakitangaza hadharani kumuunga mkono mgombeaji wanaompendelea.

Bw Sunak alipata uungwaji mkono kutoka mirengo yote ya chama chake, ikiwa ni pamoja na mrengo wa kulia, na kutoka kwa watu kama aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi wa Bw Johnson Steve Barclay, Waziri wake wa zamani wa Brexit Lord Frost na Kemi Badenoch, Katibu wa Biashara ya Kimataifa.

Bi Badenoch, ambaye alichangia pakubwa katika kinyang’anyiro cha mwisho cha uongozi wa wachama lakini amejitenga wakati huu, alisema katika gazeti la The Times kwamba Bw Sunak alikuwa ‘’kiongozi makini na mwaminifu tunayemhitaji.’’

Bw Sunak, ambaye bado hajatangaza rasmi kuwa anawania nafasi hiyo, pia anaungwa mkono na kansela wa zamani na katibu wa afya Sajid Javid, Waziri wa Usalama Tom Tugendhat, naibu waziri mkuu wa zamani Dominic Raab.

Akionyesha uchunguzi wa bunge unaomkabili Bw Johnson, Bw Raab aliambia BBC: ‘’Hatuwezi kurudi nyuma. Hatuwezi kuwa na kipindi kingine cha Siku ya Groundhog, kipindi cha maigizo cha Partygate’’.

Alisema ana uhakika sana Bw Sunak atasimama, akiongeza:’’Nadhani suala muhimu hapa litakuwa uchumi. Rishi alikuwa na mpango sahihi wakati wa ule na nadhani ni mpango sahihi sasa.’’

Waziri Mkuu huyo wa zamani hadi sasa amepata kuungwa mkono na mawaziri sita wa Baraza la Mawaziri: Ben Wallace, Jacob Rees-Mogg, Simon Clarke, Chris Heaton-Harris, Alok Sharma na Anne-Marie Trevelyan.

Pia miongoni mwa wafuasi wa Boris Johnson ni katibu wa zamani wa mambo ya ndani Priti Patel ambaye alisema anaweza kuleta pamoja timu iliyoungana na kuiongoza Uingereza kwenye mustakabali wenye nguvu na ustawi zaidi.

Wakati huo huo, mshirika wa katibu wa zamani wa mambo ya ndani Suella Braverman aliambia shirika la habari la PA kwamba ‘’yuko makini sana’’ na Bw Johnson na Bw Sunak na kuna uwezekano wa kuamua ni nani wa kumuunga mkono Jumapili.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Penny Mordaunt alikuwa wa kwanza kutangaza kwamba anataka kazi hiyo ya ngazi ya juu

Wakati huo huo Andrea Leadsom, katibu wa zamani wa biashara, alisema Bi Mordaunt alikuwa mgombea anayeunganisha;

waziri mwenye uzoefu na ‘’imara katika masuala ua Brexit’’.

Akiandika katika gazeti la Express siku ya Jumapili, Bi Mordaunt aliweka mpango wake wa ‘’kuunganisha chama na nchi’’ na akasema ‘’wanachama wameruhusu kukosa mwelekeo kwa mizozo ya ndani’’.

Alisisitiza haja ya ‘’kuhakikisha mpango wa Brexit ufanye kazi’’, ‘’kuzingatia uwezo wa raia wetu wote’’ na ‘’kutetea Muungano wetu na uadilifu wa eneo lake’’.

Mbunge wa chama cha Conservative Bob Seely alisema ‘’Nadhani tuna deni la taifa la kuomba msamaha’’ na kusema anaamini Bi Mordaunt ana nafasi nzuri zaidi ya kuhakikisha ‘’umoja na uongozi bora’’ ndani ya chama.

Jitihada zinazowezekana za Bw Johnson kurejea mamlakani zinakuja wiki saba tu baada ya siku yake ya mwisho mamlakani.

Mrithi wake, Liz Truss, ndiye waziri mkuu aliyekaa muda mfupi zaidi nchini Uingereza, akijiuzulu baada ya siku 45 madarakani.

Alijiuzulu Alhamisi, baada ya mfululizo wa matukio ya kufedhehesha ya kwenda mbele na kurejea nyuma kulikotokana na kutopokelewa vizuri kwa sera zake za ushuru katika masoko ya kifedha.