Liz Truss:Kwa nini Waziri Mkuu wa Uingereza alijiuzulu?

Liz Truss amejiuzulu kama waziri mkuu wa Uingereza baada ya wiki sita. Haya ndiyo unayohitaji kujua kumhusu ikiwa hufuatilii siasa mara kwa mara.

Alikuwa waziri mkuu wa Uingereza aliyehudumu kwa muda mfupi zaidi
Liz Truss alichukua nafasi ya Boris Johnson kama kiongozi na kuwa Waziri Mkuu mnamo 6 Septemba kisha akajiuzulu siku 45 baadaye. Rekodi ya hapo awali iliwekwa kwa siku 119 na George Canning ambaye aliaga dunia akiwa ofisini mnamo 1827.


Alikumbana na matatizo haraka sana
Kwa msaada wake, waziri wa fedha Kwasi Kwarteng alizindua mpango wa £45bn ya kupunguzwa kwa kodi katika wiki yake ya tatu, katika kile walichokiita "bajeti ndogo".
Lakini ililaumiwa pakubwa kwa kusababisha matatizo makubwa ya kiuchumi.
Licha ya Truss kusisitiza wakati huo ilikuwa "jambo sahihi kufanya", karibu yote sasa yamebadilishwa - na Kwarteng alifukuzwa kama kansela.

Baadhi ya wabunge wake walianza kumkosoa waziwazi
Makumi ya wanachama wa Tories walimtaka ajiuzulu na Katibu wake wa Mambo ya Ndani Suella Braverman alijiuzulu. Ilimbidi kuajiri wapinzani wake wa zamani Grant Shapps na Jeremy Hunt ili kuziba mapengo katika timu yake kuu.

Alisema hangeweza kutimiza kile alichoahidi
Katika hotuba yake ya kujiuzulu nje ya Downing, alisema: "Ninatambua kwamba siwezi kutimiza ahadi ambayo nilichaguliwa na Chama cha Conservative."

Alimshinda Kansela wa zamani Rishi Sunak na kuwa Waziri Mkuu
Wabunge wa Conservative pekee na wanachama wa chama ndio waliopata kupiga kura ili kumfanya kiongozi wake.
Sunak alikuja mbele katika kura za wabunge lakini katika kura ya mwisho kutoka kwa wanachama zaidi ya 80,000 walimchagua badala ya Sunak, na kumfanya kuwa mshindi.

Hatujui nani atachukua nafasi yake
Kutakuwa na shindano la uongozi ndani ya wiki ijayo. Ataendelea kuwa kiongozi hadi atakapotangazwa mrithi wake.

Alikuwa Wazirim Mkuu wa mwisho kuteuliwa na Malkia Elizabeth II
Malkia alimteua Liz Truss siku chache kabla ya kifo chake na uongozi wake ulianza na kipindi cha maombolezo cha siku 10.

Aliwahi kufanya kazi kama mchumi
Baada ya chuo kikuu alifanyia Shell na Cable & Wireless, na aliolewa na mhasibu Hugh O'Leary mwaka wa 2000. Wana binti wawili.
Familia hiyo inaishi Thetford, Norfolk.














