Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022:Raila Odinga apinga matokeo ya uchaguzi

Raila Odinga

Chanzo cha picha, Various

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Muungano wa Azimio Raila Odinga
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Kiongozi wa Muungano wa Azimio nchini Kenya Raila Odinga amepinga matokeo ya uchaguzi uliomtangaza naibu wa rais William Ruto kuwa ndiye rais Mteule.

Raila amesema kwamba hakubaliani na matokeo hayo kwasababu mwenyekiti wa tume hiyo alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi

Amesema kwamba makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliompatia ushindi William Ruto.

''Takwimu zilizotangazwa na Chebukati ni batili kwa maoni yetu, hakuna mshindi kisheria, aliyetangazwa kihalali wala rais mteule''.

Hatahivyo Raila Bw Odinga aliwataka wafuasi wake kudumisha amani na utulivu huku muungano huo ukifuata njia za kikatiba za kubatilisha matamshi ya Bw Chebukati.

''Jana, demokrasia yetu changa ilikumbwa na msukosuko mkubwa, kwa sababu hiyo, Kenya inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisheria na kisiasa kutokana na matendo ya Wafula Chebukati''.

''Tunafuatilia njia za kisheria na za amani. Tuna hakika kwamba haki itatendeka. Tunaelewa kuwa ni Bw Chebukati pekee ndiye aliyepata kujumlisha kura za urais. Aliwanyima makamishna wote kupata taarifa hizo'', aliongezea Raila akizungumza na vyombo vya habari jijini Nairobi.

Ruka Facebook ujumbe

Haipatikani tena

Tazama zaidi katika FacebookBBC haihusiki na taarifa za kutoka mitandao ya nje.

Mwisho wa Facebook ujumbe

Matamshi yake yanajiri muda mfupi tu baada ya makamishna wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi kujitenga na matokeo wakidai kwamba yalikumbwa na 'kiza kinene'.

Makamishna hao wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera wamesema kwamba hawakukubaliana kuhusu matokeo yaliotangazwa na Wafula Chebukati.

Walisema kwamba hesabu iliotolewa na Chebukati ya asilimia 100.1 haikuingiliana na jumla ya matokeo ya urais ya wagombea wote wanne.

Akizungumza na waandishi wa habari Raila aliongezea kwamba mwenyekiti huyo hakujadiliana na makamishna wenzake kuhusu matokeo hayo kabla ya kuyatangaza.

.
.