Mkusanyiko wa habari za michezo: Messi, Suarez, Havertz, Sanchez

Chanzo cha picha, Reuters
Mgombea wa wadhfa wa urais katika klabu ya Barcelona Victor Font anasema kwamba itakuwa hatua ya kushangaza lakini nzuri iwapo Lionel Messi atasalia na mabingwa hao wa Uhispania.
Messi mwenye umri wa miaka 33 wiki iliopita aliambia Barcelona kwamba anataka kukamilisha hudumu zake za miaka 20 katika klabu hiyo msimu huu.
Ripoti za hivi karibuni zimesema kwamba mchezaji huyo wa Argentina huenda akasalia katika klabu hiyo , lakini Font anasema kwamba uwezekano ni mchache.
''Atatushangaza kwasababu inaonekana tayari ameafikia uamuzi'', alisema Font.
Messi na Barcelona wapo katika mzozo kuhusu kifungu cha kandarasi yake na iwapo hana haki ya kuondoka katika klabu hiyo kama mchezaji huru.
Klabu zinazomuhitaji zinaitaka Barcelona kukubali dau lililo chini ya kifungu hicho cha kandarsi yake kinachotaka Barcelona ilipwe Yuro milioni 700 ilio kuondoka.
Luis Suarez ajiunga na Juventus

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez amekubali kujiunga na Juventus , kulingana na ripoti za mwandishi wa BBC radio 5 Live Guillem Balague.
Suarez atajiunga na mabingwa hao wa Serie A kwa uhamisho wa bila malipo au dau la kawaida iwapo ataweza kuondoka kutoka klabu hiyo.
Raia huyo wa Uruguay ana mwaka mmoja katika kandarasi yake aliosaini 2016 lakini iwapo alicheza asilimia 60 ya mechi zote katika msimu wa 2020-21 ataongezwa mwaka mmoja zaidi.
Suarez atafurahi kuondoka akiwa na msimu mmoja uliosalia.
Sanchez: Sikufurahia kuichezea Man United

Mchezaji wa zamani wa Manchester United Alexis Sanchez amesema kwamba hakufurahia katika siku yake ya kwanza katika klabu yake baada ya kujiunga na Arsenal.
Sanchez ambaye amejiunga na Inter Milan baada ya msimu mmoja akihudumu kwa mkopo kutoka United, anasema kwamba alimuomba ajenti wake iwapo angeweza kuvunja kandarasi yake ili kurudi London baada ya kuhamia Old Trafford katika uhamisho wa kubadilishana wachezaji mwezi Januari 2018.
''Mara nyengine kuna vitu ambavyo hutavijua hadi unapowasili'', alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 katika kanda ya video ya Instagram.
''Kuna kitu ambacho sikuelewa na hakikuwa vizuri''.
Haverts kukamilisha uhamisho wa Chelsea

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Bayer Leverkusen Kai Havertz anakaribia kutia saini kandarasi na klabu ya Chelsea baada ya kupewa ruhusa kuondoka kambi ya mazoezi ya timu ya Ujerumani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anakaribia kuwa mchezaji wa sita kusajiliwa na Lampard msimu huu.
Leverkusen imesema kwamba mchezaji huyo ana thamani £90m. Havertz atasafri hadi mjini London huku uhamisho huo ukitarajiwa kukamilishwa katika kipindi cha saa 24.












