Trump na Zelensky wazozana Ikulu, mkutano wavunjika, Zelensky aondoka kwa hasira

Mkutano wa pamoja wa wanahabari waahirishwa baada ya Trump kumwambia Zelensky "amemkosea heshima" na kusema "tufanye makubaliano au tuondoke".

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu na Martha Saranga & Mariam Mjahid

  1. Viongozi Ulaya wamuunga mkono Zelensky kufuatia mzozo wake na Trump Ikulu

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Macron

    Muda mfupi baada ya mkutano kati ya Donald Trump na Volodymyr Zelensky kuvunjika kwa kurushiana maneno makali, viongozi wa Ulaya wazungumza.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Waziri Mkuu wa Polandia na rais wa zamani wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, alimuandikia Zelensky na kusema, "Marafiki wapendwa wa Ukraine, hamko peke yenu."

    Akiulizwa kuhusu mvutano huo alipokuwa Ureno, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aliviaambia vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa Urusi ndiyo anayeshambulia na kwamba watu wa Ukraine ndio wanaoshambuliwa.

    Ameongeza kuwa nchi za Ulaya na washirika wengine walikuwa sahihi kwa kuisaidia Ukraine miaka mitatu iliyopita, kuwapatia vikwazo Urusi na kuendelea kufanya hivyo.

    Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu "kuheshimu" wale ambao wamekuwa wakipigania tangu mwanzo kwa ajili ya heshima, haki na usalama wa Ulaya.

  2. Trump amwambia Zelensky: 'Unacheza na Vita ya tatu ya Dunia'

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Zelensky akiondoke Ikulu ya Marekani, bila kuagwa na mwenyeji wake Trump kama ilivyo kwa viongozi wakuu wanapotembeleana

    Moja ya maneno waliorushiana Trump na Zelensky katika Ikulu ya Marekani ni kwamba kiongozi huyo wa Ukraine anacheza na vita ya tatu ya dunia. Trump alisema ' 'Unacheza na Vita ya tatu ya dunia'.

    Alisema hivyo baada ya zelensky kuonekan kutounga mkono mazungumzo ya Trump na makamu wake, JD Vance kuhusu namna Ukraine unavyoshughulika na mzozo wake na Urusi.

    Kwa upande wake Zelensky alimwambia Trump ' usimchekee muuaji', akimrejea Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Marekani inataka Ukraine ikubaliane na Urusi kumaliza mzozo huo kwa namna ambayo Zelensky hakubaliano nayo.

    Awali kwa mujibu wa mshirika wetu wa Marekani, CBS, wawakilishi wa Ukraine waliondoka kutoka Ikulu ya Marekani kupitia “chumba kilichotengwa.” mshauri wa usalama wa taifa, Mike Waltz, na Waziri wa Nje, Marco Rubio, waliwaambia waondoke katika Ikulu ya White House.

    Mkutano uliopangwa wa waandishi wa habari ambapo Zelensky na Trump wangezungumza kwa pamoja ulifutwa muda mfupi baada ya mzozo wa Ikulu.

    Trump aliwahi kumwambia Zelensky kwamba anapaswa kuwa “mwenye shukrani” kwa msaada wa Marekani, wakati Naibu Rais JD Vance alimlaumu kwa kutoshukuru wakati wa mkutano.

    Kujibu hiylo Zelensky alichapisha kwenye mtandao wa X:

    "Asante Marekani, asante kwa msaada wenu, asante kwa ziara hii."

    "Asante @POTUS, Congress, na watu wa Marekani. Ukraine inahitaji amani ya haki na ya kudumu, na tunafanya kazi hasa kwa ajili ya hilo."

    Ingawa baadhi ya wabunge wa Republican wamewakosoa Trump na Vance kwa kushambuliana na Zelensky, washirika wengine wamewmuunga mkono. Mwakilishi Rick Scott wa Florida anaandika kwenye X: "Asante Rais Trump kwa kusimama kwa ajili ya Marekani."

    Waziri wa Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, anasema kwamba Volodymyr Zelensky "ana ujasiri na nguvu ya kusimama kwa ajili ya kilicho sawa," katika chapisho kwenye X, baada ya kuondoka kwa haraka kwa rais kutoka Ikulu ya White House.

  3. Trump na Zelensky wazozana Ikulu, mkutano wavunjika, Zelensky aondoka kwa hasira

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameondoka Ikulu ya White House baada ya majibizano makali na Rais wa Marekani Donald Trump na Makamu wake JD Vance.

    Baada ya tukio hilo lililoonyeshwa moja kwa moja kutoka White House, Rais wa Ukraine anaonekana akitoka nje ofisi na kuingia kwenye gari nyeusi aina ya SUV, ambayo iliondoka kwa kwa haraka.

    Muda mfupi baadaye, Trump alichapisha ujumbe mmtandao wake wa Kijamii wa Truth Social akidai kwamba Zelensky "aliidharau Marekani katika Ofisi yake ya Oval inayopendwa. Anaweza kurejea akiwa tayari kwa mazungumzo ya amani."

    Huku hayo yakijiri Ikulu ya White House inasema Trump na Makamu wake JD Vance "hawatakubali watu wa kutumiwa vibaya".

    Katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baada ya mkutano wao na Zelensky, Ikulu ya White House inasema wawili hao "daima watazingatia maslahi ya Wamarekani na wale wanaoheshimu nafasi ya Marekani duniani"

    Soma pia;

  4. Afya ya Papa yaimarika ingawa analazwa hospitalini

    gg

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa kanisa la Katoliki Papa Francis, ambaye amekuwa akiugua homa ya mapafu kwa wiki mbili sasa, ameanza kupata nafuu , kwa mujibu wa Vatican.

    Hata hivyo atabaki hospitali kutokana na mifumo ya kliniki.

    Kulingana na taarifa ambayo BBC imeiona ni kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 88 alipata usingizi mnono na sasa amepumzika katika hospitali ya Gemelli ya Roma.

    Kufikia sasa Papa hali yake ya afya sio ya dharura kama hapo awali, vyanzo vya Vatican vyasema.

    Papa alilazwa hospitalini tarehe 14 Februari baada ya kupata matatizo ya kupumua kwa siku kadhaa.

    Alitibiwa mara ya kwanza kwa ugonjwa wa mkamba kabla ya kugundulika kuwa na homa ya mapafu.

    Kisha tarehe 22 Februari, Vatican ilisema kwamba Papa alikuwa na tatizo la kupumua na alikuwa katika hali "mbaya", lakini baadaye siku ya Jumapili ilitoa sasisho kwamba "hakuwa amewasilisha matatizo yoyote zaidi ya kupumua".

    Siku iliyofuata Papa alitoa taarifa akiwaomba Wakatoliki wamwombee baada ya kushindwa kusali sala ya Malaika ana kwa ana kwa wiki ya pili.

    Kiongozi wa Kanisa Katoliki la Roma amelazwa hospitalini mara nyingi katika kipindi chake cha miaka 12, ikiwa ni pamoja na kutibiwa ugonjwa wa mkamba katika hospitali hiyo hiyo mnamo Machi 2023.

    Kutoka Argentina, Papa Francis ni wa kwanza wa Amerika Kusini, na Mjesuti wa kwanza, kuongoza Kanisa Katoliki la Roma.

    Soma zaidi:

  5. Trump atangaza ushuru mwingine dhidi ya China

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema anapanga kutoza kodi mpya ya 10% bidhaa za kutoka China kama sehemu ya mkakati wa kiuchumi unaoendelezwa na utawala wake.

    Bidhaa zinazotoka China tayari zinatozwa ushuru wa asilimia 10%, baada ya Trump kuagiza hilo na kuanza utekelezwaji wake mapema mwezi huu.

    Wizara ya masuala ya kigeni ya China imesema '' haijaridhishwa'' na mipango hiyo.

    Trump pia amesema kuwaanakusudia kuendelea kutekeleza vitisho vyake vya kutoza ushuru wa asilimia 25% bidhaa zinazotoka mataifa ya Canada na Mexico - agizo ambalo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza tarehe 4 mwezi Machi.

    Bi McDaniel alisema agizo la Trump dhidi ya China haliko wazi, na hivyo kuongeza uwezekano kwamba hatua hizo zitaanza kutekelezwa.

    Awamu ya kwanza ya Trump ya kutoza ushuru kwa China ilizidiwa na vitisho vyake dhidi ya Canada na Mexico.

    Lakini uwezekano wa ushuru zaidi unaibua maswali kuhusu jinsi biashara zitakavyojibu.

    Bi McDaniel alisema anatarajia athari za ushuru huo zishuhudiwe zaidi nchini Uchina.

    "Sio hasara kwa Marekani, lakini hadi sasa inaonekana kuwa ni ghali zaidi kwa Uchina," alisema.

    Athari za ushuru, ikiwa zitaanza kutumika, zinatarajiwa kuhisiwa zaidi katika uchumi wa Canada na Mexico, ambao huhesabu Marekani kama soko kuu la kuuza nje.

    Lakini wachambuzi wameonya kuwa tishio la tozo hizo, hata kama hazitozwi kamwe, bado kuna uwezekano wa kuwa na athari mbaya kwa uwekezaji, ikiwa ni pamoja na Marekani.

    China tayari imejibu awamu ya kwanza ya ushuru kutoka kwa Marekani na ushuru wake kwa bidhaa za Marekani, ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe na mashine za kilimo.

    Trump amepuuzilia mbali hofu kuhusu uharibifu wa uchumi wa Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Wafanyakazi wetu walimhudumia 'vyema' abiria aliyefariki akiwa safarini - Qatar Airways

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la ndege la Qatar Airways limesema kuwa uchunguzi umebaini kuwa na wafanyikazi wake walishughulikia kwa haraka tukio la mwili wa abiria aliyefariki kwenye ndege kuwekwa karibu ya wanandoa wa Australia.

    Shirika hilo limewaomba radhi wanandoa hao wawili walioelezea kituo cha Channel 9, jinsi walivyopatwa na 'mshtuko' walipokuwa safarini kutoka Melbourne Australia kuelekea Doha Qatar.

    Tukio hilo lilizua mjadala na hisia mseto kuhusu utaratibu wa kushughulikia abiria akifariki kwenye ndege.

    Shirka hlio la ndege limeiambia ameiambia Channel 9 kwamba wafanyakazi wake walimhudumia kwa haraka mwanamke huyo alipoanguka kati kati ya viti lakini "kwa bahati mbaya alifariki."

    Amesema wafanyakazi hao walijaribu kuuhifadhi mwili wa mwanamke huyo katika kitengo cha abiria wa daraja la pili "lakini hawakuweza kuupitisha kwenye njia baina ya viti kwa kuwa marehemu alikuwa mnene."

    Ring anasema wahudumu waliona viti vitupu kando yake wakamuuliza: 'Je, unaweza kutumia kiti kingine, tafadhali?' na nikasema, 'Ndio, haina neno'. "Ndipo wakauweka mwili wa mwanamke huyo kwenye kiti nilichokuwa nimekalia."

    Bi Colin aliweza kuhamia kiti cha karibu ambacho hakikikuwa na abiria, lakini Ring anasema hakupewa nafasi ya kubadili kiti ingawa kulikuwa na viti ambavyo havikuwa na watu.

    Wanasema ipo haja ya kuwa na utaratibu maalum wa kuhakikisha abiria walio ndani ya ndege hawajipati katika mazingira kama hayo dharura ikitokea.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mexico yaikabidhi Marekani watuhumiwa wa uhalifu wa kimataifa

    Mlanguzi wa dawa za kulevya kutoka Mexico Rafael Caro Quintero alikamatwa hapo awali huko San Simon mnamo Julai 2022

    Chanzo cha picha, Government of Mexico

    Maelezo ya picha, Mlanguzi wa dawa za kulevya kutoka Mexico Rafael Caro Quintero alikamatwa hapo awali huko San Simon mnamo Julai 2022

    Mexico imeikabidhi Marekani watu 29 wanaodaiwa kuwa wanachama wa magenge ya dawa za kulevya, akiwemo Rafael Caro Quintero ambaye allikuwa akisakwa kwa mauaji ya afisa wa Marekani miaka 40 iliyopita.

    Hatua hii, inayoonekana kama moja ya makabidhiano makubwa zaidi katika historia ya Mexico, ni muhimu katika ushirikiano wa usalama kati ya nchi hizo mbili.

    Uamuzi huu umejiri baada ya Rais Trump kutishia kutekeleza ushuru kwa bidhaa za Mexico kwa kushindwa kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na uhamiaji haramu.

    “Kama alivyoeleza Rais Trump, magenge ni maakundi ya kigaidi, na Idara hii ya Sheria imejizatiti kuvunja magenge haya ya wahalifu wa kimataifa,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, katika taarifa usiku wa Alhamisi.

    Polisi wa Texas walithibitisha kukabidhiwa kwa ndugu Miguel na Omar Treviño, ambao walihusika na shughuli haramu mbalimbali.

    Baada ya hatua hiyo polisi wa Mexico wametoa wito kwa Wamarekani kutovuka mpaka wa Mexico kwa hofu ya kulipiziwa kisasi.

    Soma pia:

  8. Mwanamke ajipata mashakani baada ya kumbusu msanii wa Korea Kusini

    Jin alifanya hafla ya kukumbatiana bila malipo ambapo aliwakumbatia mashabiki 1,000 mwaka jana baada ya kuachiliwa kutoka jeshi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jin alifanya hafla ya kukumbatiana bila malipo ambapo aliwakumbatia mashabiki 1,000 mwaka jana baada ya kuachiliwa kutoka jeshi

    Mwanamke Mjapani anachunguzwa na maafisa wa polisi wa Korea Kusini kwa kumbusu Jin wa BTS katika tafrija la mashabiki huko Seoul mwaka jana.

    Mwanamke huyo badala ya kumkumbatia Jin kama mashabiki wengine wa BTS alimbusu msanii huyona Jin alionekana kutoridhishwa na hatua hiyo.

    Tukio hilo lilisababisha hasira kwa mashabiki wengine, na mmoja wao alilalamika kwa polisi baada ya video hiyo kuenea mitandaoni.

    Polisi wa Korea Kusini wamemuita mwanamke huyo, ambaye kwa sasa yuko Japan, kujitokeza kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kumnyanyasa kijinsia Jin wakati wa tukio hilo la hadhara.

    Baadaye, mwanamke huyo aliandika kwenye blogu yake na kukiri kumbusu Jin kwenye shingo yake.

    BBC ilijaribu kuwasiliana na wakala wa BTS, HYBE, kwa maoni kuhusu tukio hilo.

    Jin ni mshiriki wa kwanza wa BTS kutolewa kutoka huduma ya kijeshi.

    Alifuatiwa na J-Hope ambaye alikamilisha huduma yake mwezi Oktoba.

    Wengine wanne – V, RM, Jimin, Jungkook, na Suga – bado wanaendelea na huduma zao, na kundi linatarajiwa kuungana tena mwezi Juni 2025.

    Wasanii wa K-pop wanajulikana kwa kuwa na uhusiano wa karibu na mashabiki wao kupitia njia mbalimbali za mawasiliano na matukio ya ana kwa ana.

    Ni kawaida kwa wasanii kuwasiliana na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na matukio ya moja kwa moja ili kujenga uaminifu wa mashabiki.

    Hata hivyo, mashabiki na mashirika yanaendelea kutambua baadhi ya tamaduni hatarishi za mashabiki, kama vile “sasaeng fans”, ambao mara nyingi hujishughulisha na unyanyasaji kwa wasanii wao.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marekani yafuta ghafla ufadhili wa shirika la UNAids

    gg

    Chanzo cha picha, XINHUA

    Utawala wa Trump umeondoa ufadhili shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi (UNAids), katika hatua inayoweza kudhoofisha mapambano ya Afrika dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

    Marekani ilikuwa ikitoa theluthi mbili ya ufadhili wa kimataifa wa kinga dhidi ya VVU, na mataifa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Côte d’Ivoire, na Afrika Kusini yalikuwa yakitegemea msaada huu kwa kiwango kikubwa.

    Utafiti umeonya kuwa Afrika Kusini pekee inaweza kushuhudia vifo vya takriban watu 500,000 na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi kutokana na hatua hii.

    UNAids imeripoti kukabiliwa na misukosuko katika nchi 55, hali inayoweza kusababisha kurudi nyuma kwa hatua zilizopigwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

    Wataalamu wanahofia kuwa kukatwa kwa misaada kutavuruga mipango ya matibabu, huku mamilioni ya watu wakiwa hatarini katika maeneo yaliyoathirika zaidi duniani.

    Wakati huo huo Waziri wa Afya wa Afrika Kusini ameiambia BBC kwamba hatua ya Marekani kuondoa ghafla ufadhili wa shirika hilo inatoa “tahadhari” kwa sekta ya afya ya nchi hiyo.

    Shirika la Desmond Tutu HIV Foundation limeonya kuwa kuondolewa kwa msaada wa kifedha wa Marekani kwa miradi ya Ukimwi kunaweza kusababisha vifo 500,000 Afrika Kusini katika kipindi cha muongo ujao.

    Waziri Aaron Motsoaledi amekiri kuwa kuna hofu kwamba kukatwa kwa fedha kutasababisha ongezeko la vifo, lakini amesisitiza kuwa idara yake inaendelea kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha pengo hili linazibika.

    Maelfu ya miradi inayofadhiliwa na Marekani kote Afrika Kusini imeagizwa kufungwa kufuatia tangazo la White House la kutangaza kujitoa kwa msaada huo kwa kudumu.

    Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi nyingi za Afrika zitakazokumbwa na upungufu mkubwa wa fedha za afya baada ya tangazo hili.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mfumuko wa bei waongezeka Kenya kwa mwezi wa nne mfululizo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mfumuko wa bei wa kila mwaka nchini Kenya (KECPI=ECI), unafungua orodha mpya ya ongezeko kwa mwezi wa nne mfululizo hadi 3.5% mwezi Februari kutoka 3.3% mwezi Januari, ofisi ya takwimu ilisema Ijumaa.

    Mfumuko wa bei wa kimsingi ulisalia kwa 2.0% mwezi wa Februari, bila kubadilika kutoka Januari, wakati mfumuko wa bei usio wa msingi ukipanda hadi 8.2% mnamo Februari kutoka 7.1% mwezi uliopita, Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya ilifafanua katika taarifa.

    Benki kuu ya Kenya ilipunguza kiwango chake kikuu cha riba(KECBIR=ECI), na kufungua nafasi kwa mfululizo wa nne wa 10.75% mnamo February 5,na kusema ililenga kusaidia utoaji wa mikopo na kuimarisha uchumi.

    Benki kuu ilisema mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki chini ya kiwango cha kati cha 2.5% -7.5% lengo katika kipindi cha hivi karibuni.

    Soma pia;

  11. Licha ya kutetewa na Drogba, Mourinho afungiwa na TFF kwa ubaguzi

    a

    Chanzo cha picha, ge

    Meneja wa Fenerbahçe, José Mourinho, amefungiwa michezo minne na kupigwa faini ya jumla ya £35,194 kutokana na kauli alizozitoa za 'kibaguzi' baada ya mchezo wa wa debi ya Jiji la Istanbul dhidi ya Galatasaray.

    Mourinho alituhumiwa na Galatasaray kwa kutoa kauli za kibaguzi baada ya mchezo huo wa siku ya Jumanne. Hata hivyo Fenerbahçe ilitoa taarifa ikisema kuwa kauli za kocha huyo zilichukuliwa "vibaya kutoka katika muktadha wake".

    Mechi hiyo ya sare ya 0-0 ilichezeshwa na mwamuzi kutoka Slovenia, Slavko Vincic, baada ya vilabu vyote viwili kukubaliana na kuomba achezeshe mwamuzi wa kigeni.

    Hata hivyo, mwamuzi wa nne alikuwa Mturuki na Mourinho alirudia tena kutoa lawama zake kuhusu waamuzi wa Kituruki wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo.

    Kocha huyo wa Kireno, mwenye umri wa miaka 62, alisema alikwenda katika chumba cha kubadilishia nguo cha waamuzi baada ya mchezo wa Jumatatu, akimwambia mwamuzi wa nne kwamba "kama ungekua mwamuzi, mchezo huu ungekuwa janga kabisa".

    Alhamisi, Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) lilithibitisha kuwa litamchukulia hatua Mourinho kwa masuala mawili tofauti ya kinidhamu.

    TFF ilisema itamwadhibu kwa "kauli zake za kudhalilisha na kuudhi kwa mwamuzi wa Kituruki" na kwa kauli za dhihaka na kuudhi kwa jamii ya soka ya Kituruki na waamuzi wa Kituruki".

    Kocha huyo wa zamani wa vilabu vya Chelsea, Manchester United, na Tottenham amepigwa marufuku ya kucheza michezo miwili kuwa uwanjani na amepigwa faini ya 117,000 lira za Kituruki (takriban £2,543).

    Mourinho pia amepigwa marufuku ya michezo mingine miwili kwa "kitendo cha kutoupa heshima mchezo" wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo na kupigwa faini nyingine ya £32,651.

    Muafrika Didier Drogba, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea aliyewahi kufundishwa na mourinho, alimtetea kupitia mtandao wa kijamii kusema kocha huyo si mbaguzi.

    Viongozi wa Fenerbahçe walithibitisha kwa BBC Alhamisi kuwa klabu itakata rufaa dhidi ya adhabu zilizotolewa kwa Mourinho.

  12. Jeshi la Israel lakiri kushindwa kulinda raia wake

    CVB

    Chanzo cha picha, EPA

    Jeshi la Israel limetoa ripoti rasmi ya kwanza kuhusu dosari zilizochangia kushindwa kwake wakati wa shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023, ambalo lilipelekea vita vya Gaza.

    Ripoti hiyo inahitimisha kwamba Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) "limeshindwa katika jukumu lake la kulinda raia wa Israel."

    Ripoti hiyo yenye kurasa 19 ina mambo mengi ambayo tayari yanajulikana kuhusu kile kilichosababisha kupoteza maisha kwa takriban watu 1,200 wakati wapiganaji karibu 5,000 kutoka Hamas na vikundi vingine vya Palestina walipovamia Israel, na pia kuchukua mateka 251 katika mchakato huo.

    Hakuna hoja ya kushangaza katika taarifa hiyo, lakini bado ni jambo la kutisha kuona hitimisho la jeshi kuhusu namna lilivyoshindwa kutambua nia ya Hamas na kupuuza uwezo wake.

    Ripoti hiyo inasema jeshi lilichukulia Gaza kama tishio la pili la usalama, na kipaumbele kikipewa Iran na Hezbollah.

    Sera yake kuhusu Gaza, inasema, ilikuwa "ya kitendawili: Hamas haikuwa halali, lakini hakukuwa na juhudi za kubuni njia mbadala".

    Ushahidi wa 2018 na kuendelea unaoonyesha kuwa kundi la Hamas - ambalo limetangazwa kuwa kundi la kigaidi na Israel, Marekani, Uingereza na nchi nyingine - lilikuwa likiandaa mpango kabambe uliotafsiriwa kuwa "usio halisi au usiotekelezeka", ukiakisi "matarajio ya muda mrefu ya Hamas badala ya tishio linaloweza kutekelezeka".

    Soma Pia;

  13. Mkutano wa G20 wahitimishwa bila muafaka

    cvx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Afrika Kusini imesikitishwa na kitendo cha kumalizika kwa mkutano wa G20 kuhusu uchumi wa dunia bila kupatikana muafaka baada ya maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi kadhaa kukwepa na wajumbe wengine kujiweka mbali na masuala ya kufadhili mabadiliko ya tabianchi.

    Mkutano wa siku mbili wa G20 uliokutanisha mawaziri wa fedha na benki kuu mjini Cape Town ulishindwa pia kutoa taarifa ya pamoja.

    Hata hivyo "taarifa fupi ya mwenyekiti" iliyotolewa na mwenyeji wa mkutano huo ilisema washiriki "walisisitiza kupinga sera ya kiuchumi inayozuia uagizaji bidhaa kutoka nje.

    Muhtasari huo uliongeza kuwa waliunga mkono mfumo wa biashara wa kimataifa unaozingatia kanuni, usio na ubaguzi, wa haki, shirikishi, endelevu na wazi," wakitumia maneno ambayo utawala wa Trump tayari umepinga vikali.

    Afrika Kusini ilikuwa na matumaini ya kutumia mkutano huu wa G20 kuwa jukwaa la kushinikiza nchi tajiri kuongeza nguvu zaidi fanya katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kusaidia zaidi nchi maskini katika mabadiliko ya kuelekea matumizi ya nishati safi na kufanya mageuzi katika mfumo wa kifedha unaopendelea uwekezaji wa kibenki kwa kukopesha mataifa maskini.

    Lakini mazungumzo yaligubikwa na kukosekana kwa wadau muhimu wa fedha - kama vile Marekani, China, India na Japan - na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni kutoka kwa taifa lenye uchumi mkubwa kama Marekani na Uingereza, huku kukiwa na hali ya ongezeko la mivutano ya kisiasa duniani.

    Waziri wa fedha wa Afrika kusini Enock Godongwana alisema hakufurahishwa na mkutano wa G20 kutoweza kutoa taarifa ya Pamoja.

    "Sitaki (kutaja jina la) ... nchi fulani, lakini masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanakuwa na changamoto kwa mara ya kwanza," aliiambia Reuters baada ya kutoa muhtasari wa G20.

    Soma pia;

  14. 'Mazungumzo ya kumaliza vita Ukraine yanaendelea Vizuri'

    XYZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mazungumzo ya kumaliza uvamizi wa Urusi nchini Ukraine "yanaendelea vizuri sana," lakini akaonya kuwa kuna dirisha dogo la fursa la kufanikisha makubaliano ya kumaliza vita hivyo vya muda mrefu.

    Trump alitoa matamshi hayo wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo, ambapo kiongozi huyo wa Uingereza alisisitiza kuwa uongozi wa Marekani utakuwa muhimu katika kudumisha amani nchini Ukraine endapo vita vya miaka mitatu vitamalizika.

    "Ikiwa haitatokea haraka, huenda isitokee kabisa," Trump alionya. Kwa upande wake, Starmer alisema:

    "Umetengeneza fursa kubwa ya kihistoria kufanikisha makubaliano ya amani, makubaliano ambayo nadhani yatashereheshwa nchini Ukraine na duniani kote. Hicho ndicho tunacholenga. Lakini ni lazima tukifanikishe hilo kwa njia sahihi."

    Ziara ya Starmer inafuatia ile ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aliyefika Washington mapema wiki hii akitoa ombi kama hilo kwa Trump.

    Pia inakuja siku moja kabla ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, kutembelea Ikulu ya White House.

    Trump atakutana na kiongozi wa Ukraine leo huku, Waziri Mkuu wa Uingereza akisisitiza kwamba, Trump ndiye mhimili wa kudumisha amani nchini Ukraine endapo vita vya miaka mitatu vitamalizika.

    Soma pia;

  15. Trump kukutana na Zelensky leo Ikulu ya Marekani

    TZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema ana "heshima kubwa" kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ikiwa ni masaa kadhaa kabla ya mazungumzo yao katika Ikulu ya White House.

    Mazungumzo haya yanakuja baada ya utawala wa Trump kushangaza washirika wake wa Magharibi kwa kufanya mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu na Moscow tangu Urusi ilipoivamia Ukraine zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

    Awali, Trump alionekana kumlaumu Zelensky kwa vita hivyo na kumkosoa kwa kushindwa kuanzisha mazungumzo ya amani mapema.

    "Umekuwa hapo kwa miaka mitatu," Trump alisema Jumanne iliyopita. "Ulipaswa kumaliza vita hivyo... Hukupaswa kuwa umevianzisha hata kidogo. Ungeweza kufanikisha makubaliano."

    Hata hivyo, Alhamisi hii, baada ya kukutana na Waziri mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake yanayokuja na Zelensky: "Nadhani tutakuwa na mkutano mzuri sana kesho asubuhi. Tutashirikiana vizuri sana."

    Alipoulizwa na mwandishi wa BBC, Chris Mason, kama bado anadhani Zelensky ni "dikteta", Trump alijibu: "Nilisema hivyo? Siwezi kuamini kama niliyasema hayo."

    Zelensky anatarajia kupata aina fulani ya dhamana ya usalama kwa ajili ya Ukraine ambayo itasaidia katika makubaliano yoyote ya amani yanayoweza kufikiwa.

    Alipoulizwa kuhusu dhamana hizo Alhamisi, Trump alisema tu kuwa yuko "tayari kwa mambo mengi", lakini anataka Urusi na Ukraine zikubaliane kwanza kabla ya kuamua hatua zitakazowekwa ili kutekeleza makubaliano hayo.

    Wakati wa ziara yake Ijumaa, Zelensky anatarajiwa kusaini makubaliano yatakayowapa Marekani rasilimali adimu za madini za Ukraine.

    Trump alipendekeza kuwa uwepo wa makampuni ya madini ya Marekani nchini Ukraine utakuwa kama kinga dhidi ya mashambulizi ya baadaye kutoka kwa Urusi.

    Alipoulizwa na BBC kama angeomba msamaha kwa kumwita Zelensky "dikteta" hivi karibuni, Trump alisema haamini kama alitamka maneno hayo. Pia alimsifu Zelensky kama mtu "shujaa sana".

    Trump alizungumza baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, kuhusu kumaliza vita kati ya Ukraine na Russia.

    Alitabiri kuwa atakuwa na "mkutano mzuri sana" na Zelensky siku ya leo Ijumaa, akisema juhudi za kufanikisha amani "zinaendelea kwa kasi kubwa."

    Soma pia;

  16. Habari, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja