Mwanamke aliyempokonya bunduki mwanajeshi Korea Kusini na kuwa ishara ya kukataa sheria ya utawala wa kijeshi

Usiku wa vurugu nchini Korea Kusini ulishudia matukio ambayo wengi waliamini kuwa yalikwisha sahaulika katika enzi zilizopita za taifa hilo.
Moja haswa imevutia hisia za wengi: mwanamke akikabiliana na wanajeshi waliotumwa kuwazuia wabunge kuingia bungeni baada ya Rais Yoon Suk Yeol kutangaza sheria ya kijeshi siku ya Jumanne.
Picha za Ahn Gwi-ryeong, 35, msemaji wa chama cha upinzani cha Democratic Party, akinyakua bunduki ya mwanajeshi wakati wa ghasia hizo zimesambazwa sana mtandaoni.
"Sikufikiri... nilijua tu tulipaswa kukomesha jambo hili," aliiambia Idhaa ya Kikorea ya BBC.
Ahn alielekea katika jengo la bunge huku wanajeshi wakiwa wamekusanyika katika eneo hilo, muda mfupi baada ya Rais Yoon kutangaza sheria hiyo tata ya kijeshi.
Kama wengi katika kizazi kipya cha Korea Kusini, neno "sheria ya kijeshi" lilikuwa geni kwake. Ilitekelezwa mara ya mwisho mnamo 1979.
Ahn aliposikia habari hizo kwa mara ya kwanza, alikiri kwamba "hisia ya hofu ilimjia".

Chanzo cha picha, Reuters
Sheria ya kijeshi inapotangazwa, shughuli za kisiasa kama vile mikutano ya hadhara na maandamano hupigwa marufuku, migomo na mambo y akufanana na hayo hupigwa marufuku, na shughuli za vyombo vya habari na machapisho yanadhibitiwa na mamlaka.
Wakiukaji wanaweza kukamatwa au kuzuiliwa bila amri ya mahakama.
Muda mfupi baada ya hatua hiyo tata kutangazwa, kiongozi wa upinzani Lee Jae-myung alitoa wito kwa wabunge kukutana katika Bunge la Kitaifa na kupiga kura ya kuibatilisha.
Akiwasili katika jengo la kutunga sheria muda mfupi baada ya saa 11 jioni saa za huko Ahn alikumbuka kuzima taa katika ofisi yake ili kuepuka kuzuiliwa huku helikopta zikizunguka katika eneo hilo.

Alipofika kwenye jengo kuu, askari hao walikuwa wakikabiliana na viongozi na wananchi.
Alisema: "Nilipowaona askari wenye silaha ... nilihisi kama ninashuhudia hatua ya kurudi nyuma katika historia."
Ahn na wenzake walikuwa na shauku ya kuwazuia wanajeshi wasiingie kwenye jengo kuu, ambako kura zingepigwa.
Walifunga milango inayozunguka kutokea ndani na kuweka samani na vitu vingine vizito mbele ya milango.
Jeshi lilipoanza kusonga mbele, Ahn alisonga mbele.
"Kwa kweli niliogopa mwanzoni," alisema. "Lakini nilipoona makabiliano kama hayo, niliamini, 'Siwezi kunyamaza,'" aliongeza.

Chanzo cha picha, Reuters
Bunge lilipitisha azimio la kutaka sheria ya kijeshi iondolewe mwendo wa saa 1:00 asubuhi kwa saa za huko. Wabunge wote 190 waliohudhuria walipiga kura ya kuunga mkono.
Saa 4:26 asubuhi, Rais Yoon alitangaza kwamba alikuwa akibatilisha uamuzi wake.
Baada ya fujo kutulia, Ahn alilala kwa muda ndani ya jengo la Bunge.
"Kwa kweli niliogopa kidogo kuondoka kwenye mkutano asubuhi kwa sababu haikuonekana kuwa na teksi yoyote karibu na baada ya ghasia kama jana usiku, ilikuwa vigumu kurejea," alisema.
Wakati wa mazungumzo yake na BBC, Ahn alikuwa amevalia nguo nyeusi na koti moja la ngozi aliloonekana kwenye picha za usiku uliopita.
Nyakati fulani, alizungumza kwa hisia.
"Inasikitisha na kukatisha tamaa kwamba haya yanatokea katika karne ya 21 nchini Korea," alisema.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla












