Mapinduzi Niger: Ecowas yalaani shinikizo la kumshitaki Bazoum kwa uhaini
Viongozi wa mapinduzi wanamtuhumu Mohamed Bazoum anayezuiliwa kwa kuhujumu usalama wa taifa.
Moja kwa moja
Ecowas yalaani shinikizo la kumshitaki Bazoum kwa uhaini

Chanzo cha picha, PA Media
Maelezo ya picha, Mohamed Bazoum aliondolowe mamlakani kama rais zaidi ya miaka miwili baada ya kuchukua uongozi Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS imelaani hatua ya viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Niger kumfungulia mashitaka Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kwa uhaini mkubwa, na kueleza kuwa ni "uchochezi" ambao unakinzana na ripoti za Jumamosi iliyopita za nia ya utawala wa kijeshi kutatua kwa amani mzozo wa kisiasa nchini humo. nchi.
Katika taarifa, Jumatatu, ECOWAS inasema Rais Bazoum anasalia kuwa Rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia wa Niger anayetambuliwa na jumuiya huyo na zaidi ilitaka kuachiliwa kwake mara moja kutoka kizuizini na kurejeshwa kazini.
Jumapili usiku utawala wa kijeshi wa Niger ulitangaza mipango ya kumfungulia mashitaka Rais Bazoum kwa "uhaini mkubwa" na "kudhoofisha usalama wa nchi" baada ya kukusanya ushahidi dhidi ya kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani na "wasaidizi wake wa ndani na nje".
Viongozi wa mapinduzi hata hivyo hawakutoa ushahidi wa madai haya.
Kiongozi wa mapinduzi na aliyejitangaza kuwa Mkuu wa Nchi, Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema mapinduzi hayo yalikuwa na nia njema, na yalilenga kuondoa tishio lililo karibu ambalo lingeathiri sio Niger pekee bali pia nchi jirani ya Nigeria.
Rais Bazoum, 63, mkewe na mwanawe bado wanazuiliwa katika ikulu ya rais tangu mapinduzi yaliyomuondoa madarakani mwezi uliopita.
Maelezo zaidi:
- Je Afrika Magharibi inaweza kutumia mbinu gani kubadilisha mapinduzi ya Niger?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
- Mapinduzi Niger: Muda unayoyoma kwa maamuzi ya mwisho Afrika magharibi
Sarafu ya Urusi yashuka thamani kwa kiwango kikubwa dhidi ya dola ya Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Sarafu ya Urusi Ruble imeshuka hadi thamani yake ya chini kabisa kwa muda wa miezi 16, ikishuka hadi 100 kwa kila dola ya Kimarekani.
Kudorora kwa thanani ya Ruble kunakuja huku shinikizo likiongezeka dhidi ya uchumi wa Urusi, huku uagizaji kutoka nje ukiongezeka kwa kasi zaidi kuliko mauzo ya nje na matumizi ya kijeshi kuongezeka kufuatia vita vya Ukraine.
Urusi imekuwa chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine mnamo Februari 2022.
Ruble ilishuka baada ya vita kuzuka kwa mara ya kwanza, lakini iliimarishwa na udhibiti wa mtaji na usafirishaji wa mafuta na gesi.
Thamani ya sarafu hiyo imeshuka tangu kuzuka kwa vita, lakini imepoteza takriban robo ya thamani yake kwa jumla dhidi ya dola tangu Ukraine ilipovamiwa.
Mapema Jumatatu, ruble ilikuwa 101.04 dhidi ua dola ya Marekani.
Rubles nyingi kwa kila dola inamaanisha kuwa sarafu inadhoofika, kwani itachukua zaidi ya hiyo kununua dola moja ya Marekani, ambayo kwa kawaida huonekana kuwa sarafu yenye nguvu zaidi duniani.
Benki kuu ya Urusi imesema kuwa ongezeko muhimu la kiwango cha riba linawezekana, lakini inashikilia kuwa haioni ikiwa tishio kwa uthabiti wa kifedha wa nchi hiyo.
Pia unaweza kusoma
Bunge la Ethiopia laidhinisha hali ya dharura katika jimbo la Amhara
Bunge la Ethiopia limeidhinisha hali ya dharura iliyotangazwa kuhusiana na ghasia zinazoendelea katika eneo la Amhara nchini humo.
Kikao cha bunge, kwa njia isiyo ya kawaida, hakikuonyeshwa kwenye televisheni lakini kulingana na ripoti iliyotumwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Bunge hilo, amri hiyo iliidhinishwa kwa kura nyingi.
Makundi ya kutetea haki za binadamu zunasema hatua kama hizo zilizopita zilikumbwa na tuhuna za unyanyasaji na kuwekwa kizuizini kwa watu wengi.
Maelezo zaidi:
Silaha za Urusi 'zinaonyesha ufanisi nchini Ukraine' - Waziri wa ulinzi wa Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, amekuwa akizungumza katika Maonyesho ya Kijeshi ya 2023 - tukio lililofanyika katika mkoa wa Moscow, iliyoandaliwa ili kuonyesha mifumo ya silaha ya Urusi.
"Katika hali halisi, silaha zetu zinaonyesha kuwa ni za kutegemewa na zina ufanisi," alisema, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Aliongeza kuwa "silaha za Magharibi" zilizotumiwa sana zimejionyesha kuwa "mbali na ukamilifu" wakati wa mapigano nchini Ukraine.
"Sekta ya kutengeneza silaha ya Urusi sio tu ilibadilika kwa haraka kufanya kazi chini ya shinikizo kali la vikwazo, lakini pia, nguvu zake zilikua mara nyingi zaidi katika baadhi ya maeneo," anasema.
Akiongea awali katika hotuba iliyorekodiwa, rais wa Urusi Vladimir Putin alisema Urusi iko tayari kushirikiana na nchi zingine kwenye teknolojia ya kijeshi - na "kila mtu anayetetea masilahi yake ya kitaifa" na wale "wanaofikiria ni muhimu kimsingi kuunda mfumo ambao utalinda kila nchi."
Pia unaweza kusoma:
Waumini wavamiwa katika kanisa la Bushiri Afrika Kusini
Waumini katika kanisa la Afrika Kusini linaloendeshwa na mhubiri mwenye utata kutoka Malawi Shepherd Bushiri waliibiwa wakati wa mkesha wa usiku kucha mwishoni mwa juma.
Washiriki wa Enlightened Christian Gathering (ECG) katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Mpumalanga nchini Afrika Kusini waliambia polisi kwamba majambazi watatu waliokuwa na bunduki walivamia kanisa hilo, huku wakisubiri waumini wengine wajiunge nao.
Majambazi hao walitoroka na baadhi ya vitu vya waumini hao, zikiwemo simu 14, pesa taslimu na kadi za benki.
Pia waliiba gari jeupe la mmoja wa waumini, lakini walitelekeza umbali wa kilomita 7. Polisi walisema kuwa majambazi walitaka nambari za siri za kadi za benki za waumini kabla ya kutoroka.
Mkuu wa polisi wa Mpulamanga alisema kuwa vikosi hivyo vimeanza uchunguzi wa tukio hilo.
Watu 30 hawajulikani walipo baada ya mgodi kuporomoka Myanmar

Chanzo cha picha, TARLIN MG
Takriban watu 30 wameripotiwa kupotea baada ya maporomoko ya udongo kwenye mgodi wa jade kaskazini mwa Myanmar.
Mji wa milimani wa Hpakant katika jimbo la Kachin una migodi mikubwa na yenye faida kubwa zaidi ya madini ya jade.
Wengi wa walioathiriwa wanaaminika kuwa wenyeji wanaochimba matope kando ya miamba,
Baadhi yao ni wanafanya kazi na kuishi katika mashimo yaliyotelekezwa baada ya shughuli ya uchimbaji madini.
Maporomoko ya udongo yanayosababisha vifo ni jambo la kawaida katika eneo hilo wakati mvua kubwa ya monsuni inaponyesha Myanmar kati ya Mei na Oktoba.
Takriban watu 162 walikufa katika maporomoko ya ardhi katika eneo hilo hilo mnamo Julai 2020, wakati ajali iliyotokea mnamo 2015 ilisababisha vifo vya zaidi ya 110.
Shughuli za uchimbaji madini zilikuwa zimesitishwa kwa sababu ya msimu wa mvua. Hata hivyo,wengi wa wale walionaswa katika ajali hiyo, iliyotokea siku ya Jumapili, walikuwa wachimbaji wa kujitegemea waliokuwa wakitafuta kupata jade.
Warusi wawili wazuiliwa Poland kwa kueneza propaganda za kundi la Wagner
Poland inawazuilia raia wawili wa Urusi ambao "wanatuhumiwa kusambaza nyenzo za propaganda kutoka kwa kundi la Wagner huko Krakow na Warsaw," Waziri wa Mambo ya Ndani Mariusz Kaminski alisema.
"Wote wawili wameshtakiwa kwa kufanya ujasusi," Kaminsky alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X. (zamani wa Twitter), bila kutoa maelezo kuhusu nyenzo zilizopatikana na kuchukuliwa kutoka kwao.
Baada ya wapiganaji wa kundi la Wagner kupelekwa Belarus, mamlaka ya Poland iliamua kuweka jumla ya askari 10,000 kwenye mpaka wake na na Belarusi.
Katika mkutano na Vladimir Putin mnamo Julai 23, Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, alisema kwamba mamluki wa kikundi cha Wagner walikuwa wakiomba kwenda magharibi "katika safari ya Warsaw", ambayo "ilianza kumsumbua".
Lukashenka alidai kwamba Wagner wanadaiwa kutaka kulipiza kisasi Poland kwa vita vya Bakhmut, ambapo vifaa vya nchi hiyi vilitumiwa.
Pia unaweza kusoma:
- ''Putin ndiye rais wetu, Wagner ni mashujaa:" Kwa nini Waserbia wanaipenda Urusi?
- Uasi wa Wagner: 'Hatukuwa na habari kabisa'
- Wagner Group: Kwanini EU ina wasiwasi kufuatia kuwepo mamluki wa Urusi Afrika ya Kati?
Wasaidizi wa rais wa Madagascar washtakiwa kwa kuomba rushwa ya £225,000 nchini Uingereza

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa utumishi wa Ikulu ya rais wa Madagascar ameshtakiwa nchini Uingereza kwa kutaka rushwa kutoka kwa kampuni ya madini ya Vito.
Romy Andrianarisoa na mshirika wake wanatuhumiwa kwa kuomba rushwa ya takriban £225,000 kutoka kwa kampuni ya Uingereza ya Gemfields ili kuipa leseni ya madini nchini Madagascar.
Yeye na mshirika wake, Philippe Tabuteau, wameshtakiwa kwa kuomba, kukubali kupokea au kupokea rushwa. Hata hivyo haikubainishwa ni leseni zipi zinazodaiwa kuhusishwa na makosa hayo.
Walikamatwa katika eneo la Victoria katikati mwa London mnamo Alhamisi alasiri katika mkutano ambapo walishukiwa kujaribu kuomba rushwa.
Bi Andrianarisoa na Bw Tabuteau walifikishwa kortini Jumamosi na wote wawili wamerudishwa rumande hadi watakapofikishwa tena katika Mahakama ya Southwark tarehe 8 Septemba.
Ukosefu wa usalama walazimu ujumbe wa UN kuondoka mapema kaskazini mwa Mali

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Vikosi vya Umoja wa Mataifa vyaondoka mapema kaskazini mwa Mali huku kukiwa na ukosefu wa usalama Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) umesema kuwa umeamua kuondoka mapema katika mji wa Ber kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama.
Katika taarifa kwenye mtandao wa X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter, Ujumbe huo ulizitaka pande zote zinazohusika kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kutatiza shughuli hiyo.
Lakini baadaye ulisema kuwa msafara wake wa kuondoka ulishambuliwa mara mbili, na watu watatu waliojeruhiwa walihamishwa hadi Timbuktu kwa matibabu.
Umoja wa Mataifa pia ulibainisha kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani huenda yakajumuisha uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.
Ilikuja baada ya Jeshi la Mali (FaMa) kusema kuwa wanajeshi wake saba wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika mapigano na waasi wa zamani chini ya Uratibu wa Harakati za Azawad (CMA).
Katika taarifa yake, wanajeshi wa Mali pia walisema jeshi lake liliwaua waasi 28 na kuchukua udhibiti wa Ber kama sehemu ya uhamisho wa maeneo yanayokaliwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo haikutaja waasi wa zamani wanaolishutumu jeshi la Mali kwa kutaka kushika nyadhifa za Minusma katika maeneo yanayodhibitiwa na CMA, kinyume na makubaliano ya amani ya Algiers ya Mei 2014.
'Wasiwasi mkubwa' juu ya ghasia za Amhara -Tume ya kutetea haki za binadamu Ethiopia
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia (EHRC) imeelezea "wasiwasi mkubwa" juu ya "uhasama mbaya kati ya Jeshi la Ulinzi la Ethiopia (ENDF) na kundi la waasi la Fano katika Jimbo la Amhara".
Katika wiki za hivi karibuni jeshi la taifa na Fano wamehusika katika mapigano makali huko Amhara.
Hii imesababisha hatua kali, kama vile serikali ya Israeli kuwahamisha raia wake na Wayahudi kutoka eneo hilo wiki iliyopita.
EHCR imetoa wito kwa "pande zinazozozana kukomesha mara moja" madai yote ya ukiukaji wa sheria za haki za binadamu.
Iliongeza kuwa "inaendelea kufuatilia" hali hiyo. Kama tulivyoripoti awali, kulikuwa na ripoti kwamba makumi ya waandamanaji waliuawa katika eneo hilo na ndege isiyo na rubani ya jeshi - ingawa BBC haikuweza kuthibitisha hili kwa uhuru.
EHCR pia inataja matumizi ya "silaha nzito" na kusababisha "vifo na majeraha" ya raia na uharibifu wa mali.
Shambulio la anga la Ethiopia laua makumi ya waandamanaji - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Vyombo vya habari vya eneo la Amhara nchini Ethiopia vimeripoti kuwa ndege ya jeshi la Ethiopia imewashambulia kwa mabomu waandamanaji na kuwauwa takriban watu 70.
Mashambulizi ya anga yanaripotiwa kuwakumba waandamanaji, ambao walikuwa wamekusanyika katika mji wa Finote Selam kupinga mipango ya vikosi vya serikali kuingia eneo hilo.
BBC haijaweza kuthibitisha madai hayo na bado hakuna maoni yoyote kutoka kwa serikali mjini Addis Ababa.
Jeshi na kundi la wanamgambo, linaloitwa Fano, wamehusika katika mapigano makali katika eneo la Amhara katika wiki za hivi karibuni.
Wanamgambo walikuwa wamekataa kupokonya silaha, na kusababisha serikali ya shirikisho kupeleka jeshi.
Serikali ya kijeshi Niger kumshtaki rais aliyeondolewa madarakani kwa 'uhaini mkubwa'

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Jeshi la Niger liliiondoa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia katika mapinduzi mwezi uliopita Jeshi la Niger linasema litamfungulia mashitaka Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kwa uhaini, saa chache baada ya kundi la wanazuoni waandamizi wa Kiislamu kusema viongozi wa mapinduzi ya nchi hiyo wako tayari kwa diplomasia kutatua mzozo wao na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi. Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa jana Jumapili, msemaji wa jeshi la Niger alitaja mashtaka dhidi ya Bazoum kama "uhaini mkubwa na kudhoofisha usalama wa ndani na nje" wa nchi.
Bazoum, 63, na familia yake wamezuiliwa katika makazi rasmi ya rais huko Niamey tangu mapinduzi ya Julai 26, huku wasiwasi wa kimataifa ukiongezeka juu ya hali zao kizuizini.
Rais aliyeondolewa madarakani amesema kwamba matibabu ambayo yeye na familia yake wamepokea ni "ya kikatili'' lakini serikai ya kijeshi ilisema baada ya daktari kumtembelea Bazoum kwamba hakukuwa na matatizo yoyote kuhusu afya yake.
Kanali Maj Abdramane, ambaye alisoma taarifa hiyo, pia alishutumu "vikwazo haramu, vya kinyama na vya kufedhehesha vya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas)".
Maelezo zaidi:
- Je Afrika Magharibi inaweza kutumia mbinu gani kubadilisha mapinduzi ya Niger?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
- Mapinduzi Niger: Muda unayoyoma kwa maamuzi ya mwisho Afrika magharibi
Polisi Tanzania wanamshikilia Dkt Slaa kwa tuhuma za uchochezi

Chanzo cha picha, Dkt Slaa
Dk Willibrod Slaa, mwanansiasa maarufu nchini Tanzania na mmoja wa wakosoaji kinara wa makubaliano ya uwekezaji wa bandari baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi na uhaini, wakili wake amethibitisha. Dk Slaa amekamatwa siku ya jumapili jijini Dar es Salaam huku msako mkali dhidi ya wakosoaji wa mpango huo ukionekana kushika kasi nchini Tanzania.
Mkataba huo ambao utaiwezesha kampuni ya kimataifa ya uchukuzi ya DP World yenye makao yake makuu Dubai kuchukua baadhi ya shughuli katika bandari ya Dar es Salaam, umeibua shutuma kali kutoka kwa wahusika kadhaa wanaodhani utainufaisha zaidi kampuni hiyo kuliko Tanzania na watu wake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Slaa, ambaye aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden kati ya 2017 na 2021, alikamatwa nyumbani kwake, kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Kawe kwa mahojiano.
Wakili wake, Bw. Dickson Matata amethibitisha kukamatwa kwa Dkt Slaa hapo jana na kuwa polisi walikuwa wakifanya upekuzi nyumbani kwake.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Siku ya Jumamosi Polisi walimkamata mwanasheria na mwanasiasa wa upinzani kwa tuhuma za uchochezi na kupanga maandamano ya nchi nzima yenye lengo la kuiangusha serikali.
Polisi waliwakamata wakili Boniface Anyasile Mwabukusi na Mpaluka Nyagali siku ya Jumamosi, msemaji David Misime alisema katika taarifa.
Philip Mwakilima, wakili anayewawakilisha wawili hao, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa anafanya juhudi za kuwapata wakiwa kizuizini na kwamba mashtaka dhidi yao ni "uongo na uzushi".
Mkuu wa polisi wa Tanzania Camillus Wambura alisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba anachukua hatua dhidi ya kundi linalopanga kufanya maandamano nchini kote ili kuiangusha serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya mwaka 2025.
Meli ya kivita ya Urusi yafyatua risasi za onyo kwa meli ya mizigo katika Bahari Nyeusi

Chanzo cha picha, Reuters
Meli ya kivita ya Urusi siku ya Jumapili ilifyatua risasi za onyo kwa meli ya mizigo kusini-magharibi mwa Bahari Nyeusi ilipokuwa ikielekea kaskazini, ikiwa ni mara ya kwanza Urusi kufyatulia meli za wafanyabiashara nje ya Ukraine tangu kuondoka katika mkataba wa kihistoria wa nafaka ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.
Mnamo Julai, Urusi ilisitisha ushiriki katika mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi ambao uliruhusu Ukraine kuuza nje mazao ya kilimo kupitia Bahari Nyeusi.
Moscow ilisema kwamba iliona meli zote zinazoelekea kwenye maji ya Ukraine zinaweza kubeba silaha.
Siku ya Jumapili, Urusi ilisema katika taarifa kwamba meli yake ya doria ya Vasily Bykov ilifyatua silaha za kiotomatiki kwenye meli yenye bendera ya Palau ya Sukru Okan baada ya nahodha wa meli hiyo kushindwa kujibu ombi la kusimamishwa kwa ukaguzi.
Urusi ilisema meli hiyo ilikuwa ikielekea katika bandari ya Izmail ya Ukraine. Data ya meli ya Refinitiv ilionyesha meli hiyo kwa sasa ilikuwa karibu na pwani ya Bulgaria na kuelekea bandari ya Sulina ya Romania.
Mshauri mkuu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema tukio hilo ni "ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za baharini, kitendo cha uharamia na uhalifu dhidi ya meli za kiraia za nchi ya tatu katika maji ya mataifa mengine.
" Mshauri huyo, Mykhailo Podolyak, aliongeza kwenye X, jukwaa la mtandao wa kijamii ambalo zamani lilijulikana kama Twitter, kwamba "Ukraine itatoa hitimisho zote muhimu na kuchagua jibu bora zaidi."
Viya vya Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Chelsea wamekubali kutoa £115m kumnunua kiungo wa Brighton Moises Caicedo

Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea wamekubali dili la kumnunua kiungo wa kati wa Brighton Moises Caicedo kwa ada ya rekodi ya Uingereza ya £115m.
Liverpool walikubali mkataba wa £111m kwa mchezaji huyo wa Ecuador mwenye umri wa miaka 21 siku ya Ijumaa. Lakini upendeleo wa Caicedo ni Chelsea na hatimaye wamefanikiwa kwa ofa hiyo baada ya kuwa na msururu wa mapendekezo yaliyokataliwa na Brighton msimu huu wa joto.
Ada hiyo inamaanisha Chelsea itavunja rekodi ya Uingereza mara mbili mwaka wa 2023, kufuatia ununuzi wa pauni milioni 107 mwezi Januari wa kiungo wa kati wa Argentina Enzo Fernandez.
Caicedo alijiunga na Brighton akitokea Independiente del Valle ya Ecuador kwa £4m Februari 2021, ingawa hakucheza mechi yake ya kwanza ya Premier League hadi Aprili 2022.
Aliomba kuondoka Brighton katika dirisha la usajili la Januari mapema mwaka huu na Arsenal walikataliwa ofa nyingi kwa kiungo huyo kabla ya kusaini mkataba mpya hadi 2027 mwezi Machi.
Caicedo atakuwa mchezaji wa nane kusajiliwa na Chelsea msimu huu wa kiangazi, akifuata Axel Disasi, Christopher Nkunku, Nicolas Jackson, Lesley Ugochukwu, Angelo Gabriel, Robert Sanchez na Diego Moreira.
Meneja mpya Mauricio Pochettino amepewa jukumu la kukibadilisha kikosi na kuboresha pakubwa kufuatia kumaliza katika nafasi ya 12 msimu uliopita kwenye Ligi Kuu.
Vita vya Ukraine: Mtoto wa wiki tatu na familia yake kati ya waliouawa katika mashambulizi ya Urusi

Chanzo cha picha, UKRAINE GOVERNMENT
Mtoto mwenye umri wa siku 22 tu, kaka yake mwenye umri wa miaka 12 na wazazi wao walikuwa miongoni mwa watu saba waliouawa na makombora ya Urusi kusini mwa Ukraine siku ya Jumapili.
Mabomu yalipiga nyumba ya familia yao katika kijiji cha Shyroka Balka huko Kherson, Waziri wa Mambo ya Ndani Igor Klymenko alisema.
Waliokufa pia ni pamoja na mkazi mwingine wa kijiji na wanaume wawili katika eneo jirani la Stanislav.
"Magaidi lazima wakomeshwe. Lazima wakomeshwe kwa nguvu," alisema Bw Klymenko.
"Hawaelewi kitu kingine chochote." Waziri huyo alishiriki picha za matokeo ya shambulio la Shyroka Balka, zikionyesha moshi mwingi ukitoka kwenye majengo, na miili iliyofichwa kidijitali ya baadhi ya waliofariki.
Wengine 13 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, aliongeza.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitumia hotuba yake ya kila siku kwa taifa kulaani shambulio la "kinyama" huko Shyroka Balka.
"Watu watano waliuawa," alisema. "Miongoni mwao alikuwemo mtoto wa kike, mwenye umri wa siku 22 pekee. Kaka yake, mwenye umri wa miaka 12 tu. Mama Olesia... 39 pekee, pia aliangamia." Aliongeza kuwa kumekuwa na ripoti 17 za makombora ya Urusi huko Kherson pekee, na mengine mengi zaidi.
"Hakuna siku ambapo uovu wa Kirusi haupati majibu yetu ya haki," alisema. "Hatutaacha uhalifu wowote wa Urusi bila majibu."
Kherson ilikuwa moja ya mikoa minne nchini Ukraine ambayo Rais wa Urusi Vladimir Putin alidai kunyakua mwaka jana.
Jeshi la Ukraine lilirejesha eneo la magharibi mwa eneo hilo mwezi Novemba. Wanajeshi wa Urusi wameendelea kulivamia eneo hilo kutoka ng'ambo ya mto Dnipro.
Mashambulizi hayo yametokea siku moja baada ya Moscow kuishutumu Kyiv kwa "ugaidi" kwa kile ilichosema ni jaribio la kushambulia kwa makombora kwenye daraja la Crimea linalounganisha peninsula hiyo na Urusi.
Ukraine haijathibitisha shambulio hilo, ingawa Bw Zelensky alishawahi kusema kuwa daraja hilo linatumika kama njia ya kijeshi na ni shabaha halali.
Crimea imekuwa chini ya udhibiti wa Moscow tangu majeshi ya Urusi kutwaa rasi hiyo mwaka 2014 - hatua ambayo ililaaniwa kimataifa.
Moto Hawaii: 93 wauawa huku gavana akionya kuhusu kuongezeka kwa idadi ya vifo

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu 93 wamethibitishwa kufariki katika ajali ya moto ya Maui iliyoteketeza mji wa kihistoria wa Lahaina, ukiwa ni moto mbaya zaidi Marekani kuwahi kutokea katika karne moja.
Idadi ya vifo inaweza kuongezeka "kwa kiasi kikubwa", Gavana wa Hawaii Josh Green alionya Jumamosi, huku kazi ya uchunguzi ikiendelea kuwatambua waathiriwa.
Mamia hawajulikani waliko huku mamia ya wengine wakijaza makazi katika eneo la Maui baada ya kuukimbia moto huo.
"Ni siku isiyowezekana," Bw Green alisema. Moto huo "hakika utakuwa janga mbaya zaidi la asili kuwahi kutokea Hawaii", alisema.
"Tunaweza tu kusubiri na kusaidia wale wanaoishi. Lengo letu sasa ni kuwaunganisha watu tunapoweza na kuwapatia makazi na kuwapatia huduma za afya, na kisha kugeukia kujenga upya."
Wakati huo huo, bado haijulikani ikiwa mifumo ya tahadhari ya mapema ilitumiwa au ikiwa iliharibika, huku watu wengi wakiambia BBC hawakutahadharishwa kuhusu moto huo.
Mwanasheria mkuu wa serikali anafanya "uhakiki wa kina" juu ya jinsi mamlaka ilijibu.
Kiongozi wa serikali ya kijeshi Niger yupo tayari kwa mazungumzo na ECOWAS

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyejitangaza kuwa kiongozi wa Niger na mkuu wa serikali ya kijeshi, Jenerali Abdourahamane Tchiani amesema yuko tayari kuzingatia mazungumzo ya kidiplomasia na jumuiya ya kikanda, ECOWAS, mkuu wa ujumbe wa kidini alisema, Jumapili.
Hii inafuatia mizozo kadhaa na wajumbe wa kikanda na kimataifa ambao walijaribu kupatanisha mzozo wa kisiasa nchini humo ambao ulishuhudia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum mwezi uliopita.
Viongozi wa kidini wa Nigeria wakiongozwa na Sheikh Abdullahi Bala Lau, kiongozi wa Harakati ya Izala Salafist ya Nigeria, dhehebu la Kiislamu, walikutana na viongozi wa mapinduzi, Jumamosi baada ya kuidhinishwa na Rais wa Nigeria na Mwenyekiti wa ECOWAS, Bola Tinubu.
Jenerali Tchiani alisema, "Milango yao ilikuwa wazi kuegema diplomasia na amani katika kutatua suala hilo," Sheikh Bala Lau alisema katika taarifa.
Taarifa hiyo pia ilisema Jenerali Tchiani aliomba radhi kwa kuwaepuka wajumbe wa awali wa ECOWAS akisema ni kwa hasira, pia alisema ni "uchungu" kwamba ECOWAS ilitoa makataa ya kurejeshwa rais Bazoum bila kusikia "upande wao wa suala hilo".
Wakuu wa ECOWAS walipaswa kukutana Jumamosi iliyopita ili kujadili uwezekano wa kuingilia kijeshi nchini Niger jambo ambalo Umoja huo ulisema lingekuwa "suluhisho la mwisho" iwapo chaguzi zote za kisiasa na kidiplomasia zitashindwa lakini ililazimika kuahirisha mkutano huo kutokana na "sababu za kiufundi".
Rais Bazoum, 63, mkewe na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 20 wamezuiliwa katika ikulu ya rais kwa karibu wiki tatu tangu mapinduzi ya kijeshi huku kukiwa na wasiwasi wa kimataifa juu ya afya na usalama wake
Maelezo zaidi:
- Je Afrika Magharibi inaweza kutumia mbinu gani kubadilisha mapinduzi ya Niger?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
- Mapinduzi Niger: Muda unayoyoma kwa maamuzi ya mwisho Afrika magharibi
