Mfahamu Ovidio Guzmán López, mtoto wa El Chapo aliyezuiliwa huko Culiacán

Chanzo cha picha, GOVERNMENT OF MEXICO
Si hali ngeni kwa wakazi wa Culiacán, mji mkuu wa jimbo la Sinaloa, kaskazini mwa Mexico. Asubuhi ya Alhamisi hii, waliamka na wimbi la vurugu katika mitaa yao, vizuizi na mapigano ya risasi kati ya vikosi vya usalama na wahalifu, wakati mamlaka ilipomkamata Ovidio Guzmán López, mtoto wa Chapo.
Operesheni hiyo ilitokea karibu miaka minne baada ya Guzmán, ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa genge la Sinaloa, kuzuiliwa katika sehemu hiyo hiyo, na kuachiliwa huru saa chache baadaye kutokana na vurugu zililowakabili Wanajeshi wa Mexico, na kusababisha mji kuwa katika machafuko.
Tukio hilo la ghasia la saa 24 lililotokea mwaka 2019 linakumbukwa kama "Culiacanazo".
Alhamisi hii, magari na malori yaliyoungua yaliripotiwa karibu na Culiacán, na hata ndege ya Aeroméxico ilipigwa risasi, bila kusababisha watu kujeruhiwa.
Katika video za mitandao ya kijamii, ilionekana jinsi, wakiwa wamejihami kwa meno, wakiwa na fulana za kuzuia risasi na silaha za hali ya juu, washiriki wa kikundi cha wahalifu walitawala mitaa ya jiji kujibu operesheni ya kijeshi.
Serikali ya Mexico ilithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari kukamatwa kwa Guzmán na kuhamishwa hadi ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Jiji la Mexico anayehusika na uhalifu uliopangwa.
Ovidio Guzmán Lopez, ambaye ana jina la utani la Panya au Panya Mpya, anachukuliwa kuwa mhalifu hatari, ambaye ameshutumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na mamlaka ya Marekani.

Chanzo cha picha, US STATE DEPT.
Hapendi anasa
El Ratón ni miongoni mwa watoto wanne kutoka kwa uhusiano wa El Chapo na mke wake wa pili, Griselda López Pérez.
El Chapo, ambaye anatumikia kifungo katika gereza lenye ulinzi mkali nchini Marekani, anakadiriwa kuwa na watoto wasiopungua 10 kutoka katika ndoa zake mbalimbali.
Mnamo mwaka wa 2018, Ovidio - ambaye sasa ana umri wa miaka 32 - alishtakiwa na Idara ya Sheria ya Marekani kwa kula njama ya kusambaza dawa za kulevya kuingiza Marekani, akishirikiana na kaka yake Joaquín Guzmán López.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, kuanzia Aprili 2008 hadi Aprili 2018, wawili hao walipanga njama ya kusambaza Cocaine, bangi na methamphetamine kutoka Mexico hadi Marekani.
Kwa mujibu wa mtandao wa Televisa wa Mexico, Ovidio ni kaka wa Joaquín, Griselda na Édgar Guzmán, ambaye inadaiwa aliuawa na wanachama wa genge la Beltrán Leyva.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ovidio na kaka zake wana sifa ya kuwa vijana wakatili, wenye jeuri kupita kiasi na wasio na ujuzi mkubwa wa kimkakati kama baba yao.
Ilikuwa mwaka 2012 wakati Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) ya Idara ya Hazina ya Marekani ilimuongeza Guzmán kwenye orodha ya watu wanaohusishwa na uhalifu uliopangwa wa kimataifa, hivyo kuamuru kufungiwa kwa mali yake nchini humo.
Inajulikana pia kwamba alizaliwa Badiguarato, Sinaloa. Vyombo vya habari vya Mexico vinaripoti kwamba anajielezea kama mtu ambaye hapendi sana anasa au magari ya michezo.
Ray Donovan, wakala maalum wa DEA ambaye aliongoza juhudi za mashirika 22 yaliyopelekea kukamatwa kwa Chapo Guzmán, aliiambia CNN mwezi Februari kwamba genge la Sinaloa bado linasambaza idadi kubwa ya dawa katika masoko ya Marekani. .
"Kiukweli, watoto wa Chapo sasa wamepanda ngazi hadi kwenye genge la Sinaloa na wamechukua shirika zima la Chapo," alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Watoto wengine wa El Chapo
El Chapo alikuwa na watoto 10 kutoka kwa wanawake watatu: Alejandrina Salazar, Griselda López na Emma Coronel. Sio wote wana taarifa za umma, lakini baadhi yao, kama Ovid, amehusishwa na shughuli za uhalifu.
Kwa Alejandrina alikuwa na watoto wanne, na kutengeneza ukoo wa Guadalajara. Wakati kwa Griselda alikuwa na wengine wanne, akiwemo Ovidio, ambaye alikulia Culiacán.
Mke wake wa kwanza, Estela Peña, hakuwa na watoto. Na kwa Emma Coronel alikuwa na watoto wa kike wawili mapacha ambao ni wadogo bado.
"El Chapo ni mtu mwenye elimu ndogo sana, wakati watoto wake wana wasifu tofauti sana na yeye," Francisco Jiménez, daktari wa Sheria, mtafiti na mwanachama wa Usalama na Haki wa Chuo Kikuu cha Guadalajara, aliiambia BBC Mundo mwaka 2019.
"Watoto waliokulia Guadalajara walikuwa na fursa kubwa ya kupata elimu na walijitosa katika ulimwengu wa biashara."
Lakini wale wa Culiacán mazingira yalikuwa magumu na maisha ilibidi yapatikane siku baada ya siku, mtafiti aliongeza.
Miongoni mwa watoto waliokulia Guadalajara ni Jesús Alfredo, ambaye yuko kwenye orodha ya walanguzi wa dawa za kulevya wanaosakwa na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Marekani, DEA.
Na pia Ivan Archivaldo, alikamatwa mwaka 2005 kwa madai ya utakatishaji fedha kwa ajili ya shirika la Sinaloa.
Baada ya kukaa kwa miaka mitatu katika gereza la Puente Grande lenye ulinzi mkali la Mexico - lilelile ambalo baba yake alitoroka miaka iliyopita - aliachiliwa kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Chanzo cha picha, US DEPT.STATE
alipokuwa katika kituo cha maduka, na Joaquín, ambaye pia ameshutumiwa na Marekani kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Uwezo walio nao watoto wa El Chapo ambao wanahusiana na genge la Sinaloa haujulikani.
Huko nyuma kumekuwa na mazungumzo kwamba walikuwa wakipigania udhibiti wa shirika na Ismael "El Mayo" Zambada .
"Kinachotokea ni kwamba mashirika haya hayako wima. Hayafanyi kazi kana kwamba ni udikteta," Alejandro Hope, mchambuzi wa masuala ya usalama, alieleza BBC Mundo mwaka 2019.
"Uongozi wao unasambazwa," aliongeza mtaalamu huyo.








