Rais Ruto kukomesha ruzuku ya mafuta na mahindi: Je gharama ya maisha itakuwaje?

Na Charles Gitonga

.

Chanzo cha picha, William Ruto/Facebook

Maelezo ya picha, Rais William Ruto

Kenya imesitisha ruzuku kwa petroli na kupunguza ruzuku za bidhaa zingine za mafuta ambazo zimekuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia mwezi Septemba.

Hii inaashiria kupanda kwa kasi kwa gharama ya maisha katika uchumi mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki.

Kupanda kwa bei ya mafuta kumejiri siku moja tu baada ya rais mpya wa taifa hilo William Ruto kutangaza kuwa Kenya itaondoa ruzuku hizo. Alisema mpango huo ulikuwa wa gharama kubwa na umeshindwa kufikia lengo lililokusudiwa la kushusha gharama za maisha.

th

"Pamoja na kuwa ghali sana, ruzuku ya bidhaa hupotosha soko na kuleta sintofahamu, ikiwa ni pamoja na uhaba wa bidhaa zinazotolewa ruzuku," alisema rais Ruto.

Jijini Nairobi lita moja ya petroli sasa itauzwa kwa KES 179 ($1.49) bila ruzuku yoyote. Serikali pia imepunguza ruzuku ya dizeli - inayotumiwa zaidi na wasafirishaji na viwanda, na mafuta ya taa - ambayo hutumiwa na jamii zenye uwezo mdogo wa kifedha.

Bidhaa ya dizeli sasa itauzwa kwa KES 165 ($1.37) na mafuta ya taa kwa KES 147.94 ($1.23) kwa kila lita moja baada ya ruzuku.

Bei hizo ndizo za juu zaidi kushuhudiwa nchini Kenya.

Wakati huo huo Rais Ruto pia alitangaza kuondolewa kwa ruzuku ya mahindi, na badala yake ruzuku ya mbolea kwa wakulima itakayotekelezwa kuanzia Jumatatu, Septemba 19.

Je, kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta kutakuwa na athari zipi?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kupanda kwa bei ya Mafuta Kenya
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta kutapelekea gharama ya maisha kupanda hata zaidi huku bei za bidhaa zilizoongezwa thamani ikitarajiwa kupanda.

Vile vile, kwa gharama za usafirishaji na umeme zitapanda kwa sababu Kenya huongeza gharama ya mafuta kwenye bili za umeme.

Hata hivyo, serikali ya Ruto imedai kutumikwa kwa mamilioni ya dola kusitiri wananchi kutokana na bei ghali ya mafuta katika soko la kimataifa.

Katika mwaka mmoja uliopita, Kenya imetumia $1.2 bilioni kulipia ruzuku ya mafuta. Rais Ruto alidokeza kuwa ruzuku hiyo ingegharimu $2.3 bilioni ikiwa itaendelezwa hadi mwisho wa mwaka wa kifedha utakotimia mwezi Juni mwaka ujao.

"Hii ni sawa na bajeti nzima ya maendeleo ya serikali ya kitaifa," Ruto aliongeza.

Sio rais Ruto tu ambaye ameshindwa kuona umuhimu wa ruzuku ile. Baadhi ya wataalamu wameunga mkono kauli sawa.

"Haifanyi kazi," Nikhil Hira, mtaalam wa ushuru huko Nairobi aliambia BBC.

"Lazima tuamue, je, sisi ni uchumi huria usio na udhibiti wa bei au tutachagua na kusema...sawa, tunahitaji udhibiti wa bei hapa."

Mafuta

Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, pia limetaja ruzuku ya mafuta kuwa "yenye kurudisha uchumi nyuma".

Mkurugenzi wa bara Afrika wa Shirika hilo alisema kuwa “faida za ruzuku hizi zinaelekea kupatikana kwa jamii tajiri zaidi kuliko wale maskini.”

Bei ya mafuta imechangia pakubwa mfumuko wa bei nchini hivi karibuni. Gharama ya maisha sasa ndiyo ya juu zaidi kuweza kushuhudiwa na Wakenya katika kipindi cha miaka mitano.

Shirika la Kitaifa la Takwimu, KNBS, liliripoti kuwa gharama ya maisha iliongezeka kwa 8.5% mwezi Agosti.

Aidha, takwimu za shirika la kudhibiti bei ya mafuta na kawi, EPRA, zilionyesha kuwa tozo za kodi kwa bidhaa za mafuta zimebaki kuwa juu na kuchangia 40% ya bei anayolipa mteja.

Kwa nini ruzuku ya mahindi iliondolewa?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ugali unaotengenezwa kutokana na Unga wa mahindi ni chakula muhimu nchini Kenya

Ilipotangazwa na rais wa zamani Uhuru Kenyatta wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wa Agosti, mpango wa kupunguza gharama ya unga wa mahindi ulikosolewa vikali na wapinzani wa kisiasa, haswa naibu wake wa wakati huo, William Ruto.

Wakati sasa yeye ni rais, Ruto ameweka wazi kwamba ruzuku hiyo haitarudi tena, akisema ilikuwa "inayotumiwa vibaya."

Serikali ya Kenyatta ilipunguza gharama ya unga wa mahindi kwa nusu; pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi iliuzwa kwa $0.84 kutoka bei ya awali ya takriban dola mbili.

Lakini, Rais Ruto amesema kuwa ruzuku hiyo ilimgharimu mlipa ushuru $58 milioni katika wiki nne ilipokuwa inaendeshwa na mamlaka za serikali.

Mpango huo ulifikia kikomo muda mfupi tu baada ya uchaguzi wa Agosti 8, ukihitimisha kipindi ambacho wakenya wengi walisumbuka kupata unga huo wa bei nafuu.

Baadhi ya wasagaji nafaka walihofia kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya chini iliyoamrishwa na serikali kwa hofu ya kutolipwa. Kennedy Nyagah, Mwenyekiti, Umoja wa Wasagaji Nafaka hivi karibuni (UGMA) aliiambia BBC kuwa serikali bado inadaiwa na wasagaji kiasi cha $25 milioni.

Ruzuku ya mbolea- kwa nini inatekelezwa?

Mbolea
Maelezo ya picha, Mbolea

Mpango wa ruzuku ya mbolea uliotangazwa na rais Ruto unalenga hasa wakulima wa mahindi nchini katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa nafaka.

Mahindi ni chakula nafaka muhimu sana nchini Kenya lakini katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshindwa kukidhi hitaji la ndani.

"Utabiri wa uzalishaji wa mahindi mwaka huu uko chini ya magunia milioni 30 dhidi ya uzalishaji wa kawaida wa magunia milioni 40," Ruto alisema katika hotuba yake kwa taifa.

Ili kuongeza uwezo wa udongo kuzalisha mazao, wakulima nchini Kenya wanahitaji mbolea ambayo huagizwa kutoka nje ya nchi.

Na baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari, na usumbufu wa usambazaji wa bidhaa katika soko la kimataifa, bidhaa ya mbolea imekuwa adimu na yenye be ghali zaidi kwa wakulima wengi.

Utawala mpya wa Ruto umetangaza kutoa mifuko milioni 1.4 ya mbolea ya kilo 50 kwa kila mfuko kwa $29 kutoka bei ya sasa ya $54, kuanzia Septemba, 19.

"Mkakati wetu wa kupunguza gharama ya maisha unategemea kuwawezesha wazalishaji," Ruto alieleza.

Serikali imeahidi kutoa mbolea hiyo ya bei nafuu kabla ya mwisho wa mwezi Septemba, lakini itachukua miezi kadhaa manufaa yake kufikia Wakenya kwani inachukua kati ya miezi 4 hadi 10 kwa zao la mahindi kukomaa.

Wakati huo huo, Kenya imekuwa ikitegemea uagizaji kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda.