Israel ilishambulia hospitali ya Nasser kuharibu kamera ya Hamas, IDF yasema

Wanajeshi wa Israel wamesema "walitambua kamera ambayo iliwekwa na Hamas katika eneo la Hospitali ya Nasser".

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Israel ilishambulia hospitali ya Nasser kuharibu kamera ya Hamas, IDF yasema

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Jeshi la Israel limechapisha taarifa yake hivi punde kufuatia "uchunguzi wa awali" kuhusu mashambulizi ya jana kwenye hospitali ya Nasser huko Khan Younis.

    IDF imesema katika uchunguzi wake wa awali kuhusu mashambulizi ya jana kwamba wanajeshi "walitambua kamera ambayo iliwekwa na Hamas katika eneo la Hospitali ya Nasser".

    Kamera hiyo, inasema, "ilikuwa ikitumika kutazama shughuli za wanajeshi wa IDF".

    "Kutokana na hali hiyo, wanajeshi waliondoa tishio hilo kwa kushambulia na kuharibu kamera na uchunguzi ulionyesha kuwa wanajeshi walikabiliana na tishio hilo," inaendelea taarifa hiyo.

    Mashambulizi yao yaliua takriban watu 20, wakiwemo waandishi wa habari watano.

    Soma zaidi:

  3. Miili zaidi yapatikana karibu na eneo linalodhaniwa kuwa madhehebu ya kufunga hadi kufa Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka nchini Kenya imepata miili mingine minne iliyokuwa imefukiwa eneo moja katika kijiji cha Kwa Binzaro, Kaunti ya Kilifi katika pwani ya Mombasa.

    Miili hii ya watoto wawili na watu wazima wawili ilikuwa imefukiwa katika kaburi lenye kina kifupi.

    Siku ya Jumatatu, wataalamu walipata viungo vya mwili vipatavyo 18 katika zoezi la kutafuta miili lililoanza wiki iliyopita, baada ya taarifa za kupotea kwa watoto kadhaa zilizoripotiwa katika kijiji cha Kwa Binzaro.

    Waendesha mashtaka wanasema tayari watuhumiwa 11 wanashikiliwa kuhusiana na matukio ya kupotea kwa watoto.

    Wakati uchunguzi ukiendelea, Mkuu wa Mkoa wa Kaunti ya Kilifi Rhoda Onyancha amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa kuna uhusiano kati ya miili hii iliyopatikana hivi sasa na madhehebu ya kidini inayofahamika kama Shakahola, ambalo waumini wake wanaamini kufunga na kuomba hadi kufa.

    Imani sawia na hiyo ilipelekea vifo vya watu takribani 400 miaka miwili iliyopita.

    "Tulichogundua hadi hivi sasa katika eneo hili lenye miili ni kwamba watu wanaorudi au watu waliokuwepo hapa, ni wale wale tuliowaokoa mwaka 2023 na wengine waliokwenda nyumbani. Tumegundua kwamba hawa ni watu ambao hawakukaribishwa aidha na familia zao au jamii zao," Onyancha alisema.

    Taarifa hizi za uchunguzi wa awali zimeibua maswali mapya juu ya changamoto ya jitihada za kuwarudisha waumini wa imani hii kwa familia na jamii zao.

    Wanaharakati kutoka eneo hilo pia wamezungumzia wasiwasi uliopo miongoni mwa wananchi wanaoishi katika eneo hilo, ambao wengi wao wanasita kujitokeza na kutoa taarifa muhimu kusaidia uchunguzi wa mamlaka.

    Inasemekana kuwa wananchi wanaogopa kusaidia katika uchunguzi wakiwa na wasiwasi wa kugeuzwa kuwa watuhumiwa wa matukio hayo ya mauwaji.

    Soma zaidi:

  4. Shirika la Kenya Airways lapata hasara ya Ksh. bilioni 12 kipindi cha nusu mwaka

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la ndege la Kenya Airways PLC (KQ) leo limetangaza kuwa limepata hasara ya Ksh. bilioni 12 kwa kipindi cha miezi sita iliyokamilika Juni 30, 2025 ikilinganishwa na faida ya shilingi milioni 634 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

    Katika nusu ya kwanza ya 2025, Kenya Airways ilisema ilikabiliwa na changamoto kubwa, haswa kutokana na kusitishwa kwa muda kwa huduma za ndege tatu za Boeing 787-8 Dreamliner.

    Ndege hizi ambazo huchangia theluthi ya safari zote za ndege, zilisitishwa kutoa huduma kwa sababu ya matatizo yaliyoibuliwa ya injini duniani kote.

    Mkurugenzi Mtendaji Allan Kilavuka alisema shirika la Kenya Airways linakusudia kukamilisha mipango ya kuongeza angalau dola milioni 500 katika mtaji wa ziada ili kupanua na kuboresha safari zake kufikia robo ya kwanza ya mwaka ujao.

    "Tumesema kiwango cha chini ambacho tunakusanya ni karibu nusu ya dola bilioni, ambazo tunaamini (ni) kiwango cha chini kitakachoshughulikia upanuzi ambao (tunataka)," Kilavuka alisema.

    Kilavuka alimwambia mwekezaji akielezea kwamba moja ya ndege hizo zilianza tena huduma mnamo mwezi Julai, na akasema shirika hilo lilikuwa linajitahidi kuhakikisha ndege zote zinaanza kutoa huduma kufikia mwaka ujao.

  5. Ufaransa yarudisha fuvu la kichwa la mfalme aliyeuawa nchini Madagascar

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mfalme wa Madagascar aliyeuawa na wanajeshi wa Ufaransa wakati wa vita vya enzi za ukoloni amerudishwa rasmi Madagascar.

    Makabidhiano ya fuvu la Mfalme Toera - na ya washiriki wengine wawili - yalifanyika katika hafla kwenye wizara ya utamaduni huko Paris.

    Mafuvu hayo yaliletwa Ufaransa mwishoni mwa Karne ya 19 na kuhifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Historia ya Asili katika mji mkuu wa Ufaransa.

    Ni mara ya kwanza ya kutekelezwa kwa sheria mpya iliyokusudiwa kuharakisha urejeshaji wa mabaki ya binadamu kutoka Ufaransa.

    "Mafuvu haya yaliingia kwenye makumbusho ya kitaifa katika mazingira ambayo yalikiuka wazi utu wa binadamu na katika mazingira ya ghasia za kikoloni," Waziri wa Utamaduni wa Ufaransa Rachida Dati amenukuliwa na shirika la AFP akisema kwenye hafla hiyo.

    Mnamo mwezi Agosti 1897 wakati wa ukoloni, kikosi cha Ufaransa kilichotumwa kuchukua udhibiti wa ufalme wa Menabé wa watu wa Sakalava magharibi mwa Madagaska waliua jeshi la wenyeji.

    Mfalme Toera aliuawa na kukatwa kichwa: kichwa chake kilitumwa Paris ambapo kiliwekwa kwenye kumbukumbu ya Makumbusho ya Historia ya Asili.

    Takriban miaka 130 baadaye shinikizo kutoka kwa wazao wa mfalme pamoja na serikali ya taifa hilo la Bahari ya Hindi wamechochea kurejeshwa kwa fuvu hilo.

    Si mara ya kwanza mabaki ya binadamu kutoka enzi ya ukoloni kurejeshwa na Ufaransa.

    Maarufu zaidi alikuwa mwanamke wa Afrika Kusini aliyepewa jina la utani la kikatili "Hottentot Venus" ambaye aliwahi kuwekwa kwenye maonyesho huko Ulaya na ambaye mwili wake ulirejeshwa nyumbani mnamo 2012.

    Inakadiriwa kuwa katika Jumba la Makumbusho la Historia ya Asili pekee kuna mabaki zaidi ya 20,000 ya binadamu yaliyoletwa Ufaransa kutoka duniani kote kwa sababu zinazodaiwa kuwa za kisayansi.

    Pia unaweza kusoma:

  6. UN yataka haki itendeke baada ya Israel kufanya mashambulizi mawili katika hospitali huko Gaza

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasisitiza kuwa "kuna haja ya kupatikana kwa haki" baada ya takriban watu 20 - ikiwa ni pamoja na wanahabari watano - kuuawa katika shambulizi kwenye hospitali kusini mwa Gaza Jumatatu.

    Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa uchunguzi kuhusu mashambulizi katika hospitali ya Nasser umeanzishwa, na kusema kuwa Israel "inajutia sana" kile anachokiita "bahati mbaya".

    Lakini akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva leo asubuhi, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa "uchunguzi huu unahitajika kuleta mabadiliko".

    "Waandishi hawa wa habari ni macho na masikio ya dunia nzima na lazima walindwe," amesema Thameen Al-Kheetan katika mkutano na waandishi wa habari.

    "Kuna haja ya haki kupatikana. Bado hatujaona hatua zikichukuliwa au uwajibikaji."

    Soma zaidi:

  7. Maelfu ya watu wauawa na mamia kujeruhiwa kwa saa 24 zilizopita - Hamas

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema watu 75 wamefariki katika Ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 62,819 tangu Oktoba 2023.

    Wizara hiyo inaongeza kuwa watu 370 wamefika hospitalini kutoka kote Gaza wakiwa na majeraha na kwamba "waathiriwa bado wako chini ya vifusi na mitaani".

    Takwimu za hivi punde pia zinajumuisha watu watatu ambao wizara inasema walikufa kutokana na utapiamlo na njaa.

    Katika picha: Waandamanaji wakusanyika katika Jiji la Gaza kwa mshikamano na waandishi wa habari waliouawa

    ,

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Kama tulivyokufahamisha katika taarifa za awali mauaji ya watu wasiopungua 20 yalitokea Gaza - ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari watano - katika mashambulizi mawili ya Israel kwenye Hospitali ya Nasser huko Gaza na kusababisha shutuma duniani kote.

    Katika mji wa Gaza, waandamanaji walikusanyika wakielezea mshikamano wao na wanahabari waliouawa katika mashambulizi ya jana, Jumatatu.

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Soma zaidi:

  8. Ujerumani yaondoa uwezekano wa kulitambua taifa la Palestina - Merz

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kansela wa Ujerumani asema hana mpango wa kujiunga na washirika wa Magharibi kutambua taifa la Palestina katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi ujao.

    Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari pamoja na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, Friedrich Merz alisema: "Msimamo wa serikali uko wazi juu ya uwezekano wa kutambuliwa kwa taifa la Palestina, Canada inajua hili."

    Aliongeza kuwa: "Hatutajiunga na mpango huu. Hatujaona ikiwa mahitaji yametimizwa."

    Mwezi uliopita, Carney alitangaza kuwa Canada itakuwa taifa la tatu la G7 kutambua rasmi taifa la Palestina. Hatua hiyo ilikuja baada ya taarifa kama hizo kutoka kwa Ufaransa na Uingereza, ambazo zilibainisha kwamba itasonga mbele na hatua hiyo labda Israel itimize masharti fulani.

    Hivi sasa, nchi 147 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatambua rasmi taifa la Palestina.

    Soma zaidi:

  9. Kisa cha kwanza cha binadamu kushambuliwa na vimelea vya inzi chathibitishwa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kisa cha kwanza cha binadamu kushambuliwa na vimelea vya inzi wanaokula tishu zilizo hai kimethibitishwa nchini Marekani, mamlaka zilisema.

    New World screwworm (NWS) Myiasissi ambavyo ni vimelea vya inzi vilipatikana kwa mgonjwa aliyerejea Marekani kutoka El Salvador, Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ilisema Jumatatu. Kisa hicho kilithibitishwa tarehe 4 Agosti.

    NWS myiasis ni vimelea vinavyovamia vyenye mabuu ya inzi, au funza, wenye kusababishwa na inzi.

    Wadudu hao kimsingi huathiri mifugo, na mamlaka zinasema kuwa hatari kwa afya ya umma Marekani kwa sasa "iko chini sana".

    Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vilishirikiana na idara ya afya ya Maryland kuchunguza kisa hicho.

    Vimelea hao waharibifu, ambao hula tishu hai, mara nyingi hupatikana Amerika Kusini na Caribbean.

    Licha ya juhudi za kukomesha kuenea kwake kaskazini, sasa visa vya ugonjwa huo vimethibitishwa katika kila nchi ya Amerika ya Kati, pamoja na Mexico.

    Binadamu, haswa wale walio na jeraha la wazi, wanaweza kushambuliwa na vimelea hivyo na wako katika hatari kubwa zaidi kama watasafiri kwenda katika maeneo hayo au kama wako karibu na mifugo katika maeneo ya vijijini ambako kuna inzi, CDC inasema.

    Soma zaidi:

  10. CHAN 2024: Morocco, Senegal, Sudan na Madagascar zasaka tiketi ya fainali

    gg

    Chanzo cha picha, CAF

    Kipute cha CHAN kitaingia nusu fainali Jumanne ya leo tarehe 26 kwa mechi kati ya Madagascar dhidi ya Sudan kuanzia saa kumi na moja unusu jioni jijini Kampala.

    Madagascar imekuwa ikijifua zaidi katika dimba la mwaka huu baada ya kuwekwa katika kikundi B kilichokuwa na Tanzania , Mauritania,Burkina Faso na kujizatiti na kumaliza duru ya muondoano na pointi saba.

    Ingawa ina ointi sawia na Mauritania, iemjipata katika ngarambe ya nusu fainali kutokana na kuwa na mabao mengi zaidi ukilinganisha na Mauritania.

    Tanzania waliibuka kidedea na pointi kumi lakini waliingia kwa fungu la kukosa baada ya kucharazwa bao moja mtungi na Morocco katika mchuano wa robo fainali.

    Katika mechi yao ya robo fainali Madagascar iliwazidia ujuzi Harambee stars katika awamu ya matuta katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

    Kocha wa Madagascar Michel Ramandimbozwa anaamini timu yake ina kila ujuzi na makeke ya kuipiga Sudan.

    ''Hii ni mechi muhimu kwetu na tunapaswa kujitoa kimasomaso. Sudan ni timu iliyojipanga na tunapaswa kuwa makini kila wakati.Lakini nina imani tutashinda . asema Michel.

    Safari ya Sudan kuingia nusu fainali imechochewa na kujiamini kwao na kumakinika wakiwa uwanjani.

    Nao mabingwa watetezi Senegal kumaliza udhia na mabingwa mara mbili Morocco jijini Dar es Salaam.

    Simba wa Atlas wa Morocco wanaendelea kuonyesha kuwa wao ni moto wa kuotea mbali kwenye michuano hii, wakiendeleza rekodi ya asilimia mia moja kwa kushinda mechi zao zote nne hadi sasa.

    Ushindi wao wa hivi punde ulikuwa ni wa mtaani, wakitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania katika robo fainali iliyojaa ushindani mkali.

    Iwapo Morocco wataitoa Senegal, itakuwa ni mara ya tatu katika historia yao kushinda mechi tano katika toleo moja la CHAN, baada ya kufanya hivyo pia mwaka 2018 na 2020 jambo ambalo litazidi kuthibitisha ukubwa wao kwenye ardhi ya Afrika.

    Wana rekodi ya kuvutia kwenye hatua ya muondoano wakishinda mechi saba kati ya nane, huku kipigo chao pekee kikitokea mwaka 2014 dhidi ya Nigeria.

    Cha kuvutia zaidi, Morocco hawajawahi kwenda kwenye mikwaju ya penalti, na wameingia muda wa nyongeza mara moja tu, ambapo waliichapa Libya 3-1 kwenye nusu fainali ya mwaka 2018.

    Kufuzu kwa fainali mwaka huu kutakuwa ni mara yao ya tatu (2018, 2020, 2024) rekodi ambayo inawafanya kuwa timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika kipindi hiki cha CHAN, wakiwa mbele ya mataifa kama DR Congo, Ghana na Mali, ambayo kila moja imefika fainali mara mbili.

    Mashabiki wa Morocco wana kila sababu ya kutabasamu, huku ndoto ya kutwaa taji jingine ikizidi kuota mizizi.

    Jumla ya mechi 40 kati ya 44 zimesakatwa tangu kuanza kwa makala ya nane ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa nyumbani CHAN zinazoandaliwa kwa pamoja na Kenya,Uganda na Tanzania. Magoli 80 yamefungwa huku mshambulizi wa Morocco Oussama Lamlioui, anaongoza kwa kupachika magoli manne kufikia sasa.

    Kombe la kifahari la CHAN liko jijini Nairobi tayari kukabidhiwa mshindi Jumamosi hii katika uwanja wa Kasarani wakati wa fainali. Pia unaweza kusoma:

  11. Tunachojua kuhusu waandishi wa habari waliouawa katika shambulizi la Israel siku ya Jumatatu

    Mohammed Salama alikuwa mpiga picha aliyefanya kazi na Al Jazeera na Middle East Eye, vyombo vya habari vilisema

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mohammed Salama alikuwa mpiga picha aliyefanya kazi na Al Jazeera na Middle East Eye, vyombo vya habari vilisema

    Waandishi wa habari watano waliuawa katika shambulizi la Israel kwenye hospitali moja kusini mwa Gaza jana, vyombo vyao vya habari vilisema.

    Shambulio hilo tangu wakati huo limelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

    Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza amesema "ametiwa hofu", huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiita mashambulizi hayo "yasiyovumilika", akisisitiza kwamba raia na waandishi wa habari lazima walindwe.

    Waziri Mkuu wa Israel amesema ni "msiba mbaya" na kwamba mamlaka za kijeshi "zinafanya uchunguzi wa kina".

    Vile vile, iliongeza kuwa Israeli "inathamini kazi ya waandishi wa habari, wafanyikazi wa matibabu, na raia wote" na kusema jeshi lilikuwa likifanya "uchunguzi wa kina".

    Waandishi wa habari waliouawa siku ya Jumatatu ni pamoja na:

    • Ahmed Abu Aziz, ambaye alifanya kazi kama mfanyakazi huru wa Middle East Eye na alikuwa na makazi yake Khan Younis, chombo cha habari kilisema.
    • Hussam al-Masri alikuwa mpiga picha anayefanya kazi na Reuters. Aliuawa katika mgomo wa kwanza hospitalini, kulingana na ripoti ya shirika hilo.
    • Mariam Dagga, 33, alikuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea anayefanya kazi na Associated Press (AP), shirika hilo lilisema.
    • Mohammed Salama alifanya kazi Al Jazeera na Middle East Eye, mashirika hayo yalisema.
    • Moaz Abu Taha alikuwa mpiga picha wa kujitegemea ambaye kazi yake ilikuwa ikichapishwa mara kwa mara na Reuters, shirika hilo lilithibitisha

    Israel hairuhusu mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, kuingia Gaza kuripoti kwa uhuru.

    Waandishi wa habari nchini humo wanategemewa kutoa habari kwa vyombo vya habari duniani.

    Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) inasema zaidi ya waandishi wa habari 190 wameuawa katika miezi 22 ya vita, idadi kubwa ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel.

    Wiki mbili zilizopita, Israel iliwaua waandishi sita wa habari katika shambulio lililolenga mmoja wao karibu na hospitali ya Shifa katika mji wa Gaza, na kusababisha hasira.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Waandamanaji wafunga barabara kuu kote Israel huku familia za mateka zikitaka kusitishwa kwa mapigano

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waandamanaji wamekusanyika katika makutano na maandamano kote Israel asubuhi ya leo, wakishinikiza kusitishwa kwa kampeni ya kijeshi ya Israel huko Gaza na kurejeshwa kwa mateka waliosalia wanaoshikiliwa na Hamas.

    Maandamano hayo yameandaliwa na Jukwaa la Hostages and Missing Families Forum - kundi ambalo kwa muda mrefu limeitaka serikali ya Israel kuweka kipaumbele cha kuachiliwa kwa mateka hao na kumaliza vita mara moja.

    Kundi hilo pia linamtolea wito, tena, Rais Donald Trump kwa usaidizi wa kukamilisha makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwarudisha nyumbani wale wote waliofungwa. Mateka 20 wanaoshikiliwa na Hamas bado wanaaminika kuwa hai.

    Einav Zangauker, mama wa Matan Zangauker ambaye alitekwa nyara na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, amesema 'Netanyahu anaogopa jambo moja - shinikizo la umma’

    "Kwa siku 690, serikali imekuwa ikiendesha vita bila lengo bayana," anasema wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mjini Tel Aviv.

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Picha zilizochapishwa mtandaoni zinaonyesha moto mkubwa ukiwashwa kwenye sehemu za barabara inayounganisha Tel Aviv na Jerusalem . Kwingineko, viungani mwa sehemu za Tel Aviv kando ya Barabara Kuu ya Pwani pia zimefungwa.

    Maandamanao haya yanafanyika wakati Israel imekuwa ikiimarisha mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, ikifanya mashambulizi katika mji wa Gaza kabla ya uvamizi wake uliopangwa katika eneo kubwa zaidi la mijini katika eneo hilo.

    Israel imelaaniwa na watu wengi jana baada ya mashambulizi yake katika hospitali moja kusini mwa Gaza kuwaua takriban watu 20, wakiwemo waandishi wa habari watano na wahudumu wa afya wanne.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Botswana yatangaza hali ya dharura ya kitaifa ya afya ya umma

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Botswana imetangaza hali ya dharura ya afya ya umma huku ikikabiliwa na uhaba wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu.

    Rais Duma Boko alitoa tangazo hilo katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni siku ya Jumatatu, akiweka mpango wa mamilioni ya pauni kurekebisha mlolongo wa mgawo wa huduma za afya utakaosimamiwa chini ya uangalizi wa kijeshi.

    Kudhibiti uhaba huo litakuwa jambo "nyeti sana kwa bei kutokana na hazina yetu ndogo", aliliambia taifa.

    Uchumi wa nchi hiyo umekumbwa na mdororo katika soko la kimataifa la almasi, kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa almasi duniani.

    Tatizo hili lililochochewa zaidi na upunguzaji wa misaada ya Marekani,limewaacha Wabotswana wengi kati ya raia 2.5m wakikabiliwa na ukosefu wa ajira na viwango vya juu vya umaskini, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

    "Kazi hiyo itasalia bila kukoma hadi mlolongo mzima wa manunuzi utakapowekwa," Boko alisema katika hotuba yake, akitangaza kwamba wizara ya fedha imeidhinisha pula milioni 250 za Botswana (sawa na £13.8m) kwa ufadhili wa dharura.

    Mapema mwezi huu, wizara ya afya ya nchi hiyo ilitoa tahadhari kwamba inakabiliwa na "changamoto kubwa", ikiwa ni pamoja na uhaba wa matibabu na madeni ya zaidi ya pula bilioni moja (£ 55.2m).

    Sehemu kubwa ya madeni hayo yalitokana na wagonjwa kulazwa katika hospitali za kibinafsi kwa huduma ambazo hazikupatikana kwa umma.

    Uhaba uliotajwa na Waziri wa Afya Dk Stephen Modise ni pamoja na ule wa dawa na vifaa vya kudhibiti saratani, matibabu ya VVU na kifua kikuu miongoni mwa mengine.

    Kabla ya kupunguzwa kwa misaada ya Marekani iliyotolewa na Rais Donald Trump, Marekani ilifadhili theluthi moja ya udhamini wa VVU nchini Botswana, kulingana na UNAIDS .

  14. Australia yailaumu Iran kwa mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi Sydney na Melbourne

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu Anthony Albanese

    Australia inasema itamfukuza balozi wa Iran baada ya kudai kuwa serikali ya nchi hiyo ilielekeza mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi huko Sydney na Melbourne.

    Waziri Mkuu Anthony Albanese amesema mashambulizi hayo ni "vitendo vya ajabu na vya hatari vya uchokozi vilivyopangwa na taifa la kigeni". Hakuna aliyejeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyotokea mwaka jana.

    Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Australia (Asio) Mike Burgess amesema shirika lake lilikuwa na taarifa za kijasusi kwamba Iran "huenda" ilikuwa nyuma ya mashambulizi zaidi dhidi ya walengwa wa Kiyahudi katika matukio ya Australia.

    Balozi Ahmad Sadeghi na maafisa wengine watatu wa Iran wameagizwa kuondoka Australia ndani ya siku saba. Iran bado haijasema lolote kuhusu tuhuma hizo.

    Burgess alisema: "Iran imejaribu kuficha kuhusika kwake, lakini Asio anakadiria kuwa ilihusika na mashambulizi ya Lewis Continental Kitchen huko Sydney tarehe 20 Oktoba mwaka jana, na Sinagogi ya Adass Israel huko Melbourne tarehe 6 Desemba."

    Waziri wa Mambo ya Nje Penny Wong alisema ni mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia kwamba Australia imemfukuza balozi.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Vikosi vya Marekani vyakamilisha operesheni ya kijeshi dhidi ya ISIS Somalia

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kamandi ya Marekani inayohusu Afrika (AFRICOM)

    Kamandi ya Marekani inayohusu Afrika (AFRICOM), kwa ushirikiano na Serikali ya Shirikisho ya Somalia, imekamisha operesheni ya wiki mbili dhidi ya kundi la Islamic State tawi la Somalia,kulingana na kamandi ya jeshi la Marekani

    Taarifa ya jesi la Marekani imesema opresheni hizo zililenga kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya maficho ya uongozi wa ISIS yaliyopo kwenye Milima ya Golis .

    "Mashambulizi haya mabaya yanaonyesha azimio na kujitolea kwetu kuhakikisha Wamarekani na washirika wetu wanabaki salama kutokana na tishio la ugaidi wa ulimwengu," alisema Jenerali Dagvin Anderson, Kamanda, anayehusika na kikaosi hicho cha Marekani kinachohusika na opresheni za Marekani barani Afrika.

    "Ninawapongeza wachezaji wenzetu wa kijeshi na kiraia, pamoja na washirika wetu nchini Somalia, ambao walifanya kazi katika kila nyanja ya mageuzi haya magumu. Waliweka kiwango cha kutekeleza operesheni iliyopangwa vizuri, ya Amri ya Wapiganaji dhidi ya shirika ambalo linataka kusafirisha ugaidi wao kwa Marekani na washirika wetu, alisema.

    AFRICOM, kwa uratibu na Serikali ya Shirikisho ya Somalia na Vikosi vya Wanajeshi wa Somalia, itaendelea kutathmini matokeo ya operesheni hiyo.

    Maelezo mahususi kuhusu operesheni hayatatolewa ili kuhakikisha usalama wa operesheni, taarifa hiyo imesema.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Muathiriwa wa unyanyasaji wa kingono wa watoto amuomba Elon Musk kuondoa 'links' za picha zake

    h

    Muathiriwa wa unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto amemsihi Elon Musk kusitisha utendaji wa mitandao inayotoa picha za unyanyasaji wake zinazotumwa kwenye mtandao wake wa kijamii wa X.

    "Kusikia kwamba unyanyasaji wangu - na unyanyasaji wa wengine wengi - bado unasambazwa inatia hasira," anasema "Zora" (si jina lake halisi) ambaye anaishi Marekani na alinyanyaswa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 20 iliyopita.

    "Kila wakati mtu anapouza au kushiriki nyenzo za unyanyasaji wa watoto, huchochea moja kwa moja unyanyasaji wa asili na wa kutisha."

    X anasema "haina uvumilivu kabisa kwa nyenzo za unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto" na kukabiliana na wale wanaowadhulumu watoto bado ni "kipaumbele kikuu".

    BBC ilipata picha za Zora wakati ikichunguza biashara ya kimataifa ya nyenzo za unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, zinazokadiriwa kuwa na thamani ya mabilioni ya dola na Childlight, Taasisi ya Global Child Safety.

    Nyenzo hii ilikuwa kati ya akiba ya maelfu ya picha na video zinazofanana zinazotolewa kwa ajili ya kuuza kwenye akaunti ya X. Tuliwasiliana na mfanyabiashara huyo kupitia programu ya kutuma ujumbe ya Telegram, na hii ilituongoza kwenye akaunti ya benki iliyounganishwa na mtu huko Jakarta, Indonesia.

    Zora alidhulumiwa kwanza na mwanafamilia. Mkusanyiko wa picha za unyanyasaji wake umekuwa maarufu miongoni mwa watoto wanaolala na watoto wanaokusanya na kuuza maudhui kama hayo.

    Waathiriwa wengine wengi wanakabiliwa na hali hiyo hiyo, huku picha za unyanyasaji zikiendelea kusambaa hadi leo.

    Zora amekasirishwa na biashara hiyo inaendelea hadi leo.

    Unaweza pia kusoma:

  17. Trump aviita vita nchini Ukraine 'mgogoro wa kibinafsi'

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vita nchini Ukraine vimegeuka kuwa "mzozo mkubwa wa kibinadamu," Rais wa Marekani Donald Trump alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

    Baadaye kidogo, akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu kwa nini Rais wa Urusi Vladimir Putin hataki kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Trump alijibu: "Kwa sababu yeye [Putin] hampendi yeye [Zelensky]."

    Trump pia alisema kuwa bado hajajadili kuhusu dhamana maalum ya usalama kwa Ukraine, lakini Marekani iko tayari kuunga mkono Kyiv.

    Kwa kuongezea, Trump alisema kuwa Marekani "haitumii pesa tena Ukraine," na mazungumzo yote juu ya ununuzi wa silaha kwa Kyiv hufanywa kupitia NATO.

    Soma zaidi:

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara tukikuletea habari za kikanda na kimataifa.