CHAN 2024: Wenyeji wana chakujivunia baada ya kutolewa?

j

Chanzo cha picha, CAF

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Wikiendi iliyomaliza, mechi za robo fainali ya African Nations Championship (CHAN 2024) zilichezwa katika majiji manne (Dar es Salaam, Kampala, Nairobi na Zanzibar) katika nchi tatu na timu zote waandaaji, ikiwa na maana Kenya, Tanzania na Uganda zimetolewa katika mashindano hayo.

Kenya imefungishwa virago na Madagascar katika mikwaju ya penalti ya 4-3, katika uwanja wa nyumbani wa Karasani siku ya Ijumaa. Kenya ilianza kwa ushindi wa goli moja, kabla ya goli hilo kurudishwa kwa mkwaju wa penalti, na kushindwa kuongeza goli jingine hadi dakika 90 na 30 za nyongeza.

Tanzania imetolewa na mshindi mara mbili wa kombe hilo Morocco, kutoka Afrika ya Kaskazini, baada ya kufungwa goli moja katika kipindi cha pili katika mechi iliyochezwa siku ya Ijumaa, na kushindwa kurudisha goli hilo katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Uganda ilifungwa goli moja katika kipindi cha pili mbele ya maelfu ya mashabiki katika uwanja wa Nelson Mandela jijini Kampala siku ya Jumamosi. Robo fainali yao ilikuwa ni dhidi ya bingwa mtetezi Senegal kutoka Afrika Magharibi.

Pia unaweza kusoma

Robo fainali ya kwanza

Wakiwa wameshiriki michuano hiyo kwa mara ya saba, Uganda Cranes hawakuwahi kufanikiwa kuendelea zaidi ya hatua ya makundi. Uganda imeshirika CHAN mwaka 2011, 2014, 2016, 2018, 2020, 2022 na sasa mara ya nane 2024.

Hatua ya Uganda kucheza robo fainali, ni historia mpya kwa timu hiyo baada ya kushiriki michuano hiyo mara nyingi zaidi kuliko waandaaji wenzake. Kwa maana hiyo Uganda imeondoa gundu walilokuwa nalo kwa miaka mingi.

Fainali za mwaka huu ni za tatu kwa Tanzania kushiriki baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 iliposhirika katika kundi 'A' na kuishia makundi, ikimaliza nafasi ya tatu na pointi nne. Tanzania ikashiriki tena mwaka 2020 na kuishia tena makundi, ilipomaliza nafasi ya tatu kundi 'D' na pointi nne.

Timu hiyo imeweka historia mwaka huu, sio tu kwa kucheza fainali kwa mara ya kwanza, pia kushinda michezo yao yote katika makundi na kutoa suluhu mchezo mmoja. Ushindi ambao unaonyesha kukuwa kwa soka la timu hiyo.

Kenya imepata nafasi ya kushiriki michuano ya CHAN 2024 kwa mara ya kwanza, kama mojawapo ya mataifa matatu waandaaji. Wameandika historia ya kufika robo fainali, pia kuifunga Morocco katika makundi, mshindi wa CHAN 2018 na 2020.

Maandalizi ya AFCON

K

Chanzo cha picha, CAF

Maelezo ya picha, Patrice Motsepe, rais wa Shirikisho la soka barani Afrika (Caf)
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ifikapo mwaka 2027, nchi ya Kenya, Uganda na Tanzania zitakuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika, ambalo litashirikisha nchi nyingi zaidi na wachezaji wanaocheza katika vilabu vilivyo nje ya bara la Afrika.

Mashindano hayo ya 36 yatakayofanyika mwezi Juni na Julai, yatahitaji maandalizi zaidi kwa sababu ya ukubwa wake, viwanja vingi zaidi vya mpira na mazoezi, na miundombinu yote muhimu, zikiwemo barabara, usafiri, hoteli kwa kuyataja machache.

Itakuwa ni mara ya kwanza AFCON kuchezwa katika mataifa matatu, na itakuwa ni mara ya pili kuletwa katika ukanda wa CECAFA baada ya Ethiopia kuwa mwenyeji mwaka 1976.

AFCON inatarajiwa kufanyika katika viwanja 12 (vinne Tanzania, vitano Kenya na vitatu Uganda) katika miji 10 ya nchi tatu, huku zaidi ya timu 20 kutoka pembe zote za Afrika zikitarajiwa kushiriki.

Kwa kuzingatia hayo, mashindano ya CHAN ni kipimo kizuri kwa nchi hizi kuangalia fursa na changamoto kuelekea AFCON. Kwa kuzingatia ukweli kwamba nusu na robo ya viwanja ambavyo vitatumika kwa AFCON bado havijakamiliki.